Na Mwandishi Wetu, Dar
Tanzania na
Uswisi zimekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta za afya,
elimu na uchumi kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa pande zote mbili.
Ahadi hiyo
imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi
Liberata Mulamula (Mb) alipokuwa katika maadhimisho ya miaka 40 ya Ushirikiano
wa Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi jana jioni jijini Dar es Salaam.
Balozi
Mulamula amesema kuwa katika miaka 40 ya Ushirikiano wa maendeleo kati ya
Tanzania na Uswisi, ushirikiano umeimarika na nchi hizi zimekuwa zikiufurahia
kwa kipindi chote, na kuongeza kuwa “Uhusiano
kati ya Tanzania na Uswisi ni mzuri na imara na umekuwa na manufaa kwa pande
zote mbili,” amesema Balozi Mulamula
“Tunapozindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Uswisi na Tanzania 2021-2024,
ambao pamoja na mambo mengine, umejikita katika kuimarisha taasisi za serikali,
kulinda na kuboresha afya na maisha ya vijana. Napongeza juhudi zinazofanywa na
Uswisi katika maandalizi na ukamilishaji wa mpango wa maendeleo ambao sasa
unatupeleka katika hatua nyingine ya utekelezaji,” ameongeza Balozi Mulamula.
Waziri Mulamula ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa
ikichukua hatua madhubuti katika kupitia na kuboresha mazingira ya biashara na
uwekezaji hapa nchini ambapo Serikali na sekta binafsi wanafanya kazi kwa
kutunga na kuboresha sera zitakazolinda na kuwezesha sekta binafsi kukua.
Pia Balozi Mulamula amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za
kurekebisha Sera ya Uwekezaji ya mwaka 1996. Utaratibu huu unafanywa kwa njia
shirikishi ambayo inahusisha sekta ya umma na binafsi. Mipango hii itachangia
katika kuweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji na biashara kwa wawekezaji na
biashara kutoka mataifa makubwa duniani na washirika wengine wa kibiashara.
Kwa upande wake, Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot amesema
kuwa ushirikiano wa Uswisi na Tanzania umelenga zaidi uboreshaji wa barabara za
vijijini, maendeleo ya kilimo, sekta ya afya na uwezeshaji wa asasi za kiraia.
Aliongeza kusema kuwa, miradi ya maendeleo ya Uswisi nchini Tanzania imepanuka
na kujumuisha shughuli mbalimbali katika nyanja za utawala, uvumbuzi, kuongeza
ujuzi, mafunzo ya ufundi stadi na utamaduni.
“Ushirikiano wetu umekuwa na mafanikio mengi na katika kipindi cha miaka
40 iliyopita ambapo Uswisi imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa katika sekta za
afya, ujenzi wa taasisi na mafunzo ya wafanyakazi wa afya,” amesema Balozi
Chassot
Balozi Chassot ameongeza kuwa, Uswisi itaendelea kushirikiana na Tanzania
katika kuimarisha utawala wa kidemokrasia, kutoa msaada wa kuimarisha taasisi
za serikali ili kuongeza mapato ya umma na kutoa huduma bora za umma, zenye
usawa na zinazofaa zaidi kwa wananchi wote, kupunguza vikwazo vya kijamii na
kiuchumi pamoja na kuimarisha matarajio ya kiuchumi kwa vijana.
Tunatazamia kuimarisha zaidi ushirikiano wetu na washirika wetu
serikalini na mashirika ya kiraia katika kutekeleza agenda ya kimataifa ya
kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Dazi
amesema kuwa wameridhishwa na hatua za maendeleo ambazo Tanzania imepiga na
kuahidi kuendelea kushirikiana zaidi katika kuwainua wananchi kiuchumi.
“Uswisi imekuwa ikishirikiana na Tanzania kwa zaidi ya miaka 40 na tutaendelea kuudumisha ushirikiano huu kuwainua vijana kiuchumi ili kuwawezesha kufikia malengo yao kijamii na kisiasa,” amesema Bi. Dazi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Liberata Mulamula akihutubia katika maadhimisho ya miaka 40 ya
Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi jana jioni jijini Dar es
Salaam
Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot akihutubia
katika maadhimisho ya miaka 40 ya Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Tanzania na
Uswisi jana jioni jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Uswisi
Bi. Patricia Dazi akihutubia katika maadhimisho ya miaka 40 ya Ushirikiano wa
Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier
Chassot katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la
Uswisi Bi. Patricia Dazi
Sehemu ya wageni waalikwa walioshiriki katika maadhimisho
ya miaka 40 ya Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi jana jioni
jijini Dar es Salaam
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.