Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati
ya Tanzania na Uganda umeanza leo tarehe 17 Januari 2022 katika ngazi ya
Wataalamu Jijini Kampala, Uganda.
Mkutano huu wa awali pamoja na mambo mengine utajadili masuala
ya ushirikiano yaliyokubaliwa baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Jamhuri ya Uganda. Mkutano huu utafuatiwa na mkutano katika ngazi
ya Makatibu Wakuu utaofanyika tarehe 18 Januari 2022 na utamalizika kwa Mkutano
ngazi ya Mawaziri utaofanyika tarehe 19 Januari 2022.
Lengo la Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ni kujadili na kutathmini hatua za utekelezaji zilizofikiwa katika masuala mbalimbali ya ushirikiano yaliyokubaliwa kwenye mkutano wa tatu uliofanyika mwezi Septemba 2019 jijini Dar es salaam, Tanzania.
Pia, kutathmini utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika ziara zilizofanywa na Marais wa pande zote mbili katika nyakati tofauti, tangu kumalizika kwa Mkutano wa Tatu wa Tume ya Kudumu ya Pamoja kati ya Tanzania na Uganda.
Vilevile, mkutano huu utashuhudia utiwaji saini wa mikataba takribani sita itakayohusisha sekta mbalimbali za ushirikiano pamoja na kuruhusu maeneo mapya ya ushirikiano. Kadhalika utajadili ushirikiano katika ujenzi wa miradi ya kimkakati unaofanywa na mataifa hayo hususan ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) unaofanywa na Serikali ya Tanzania ambao unatarajiwa kunufaisha nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tanzania na Uganda zinashirikiana katika sekta za Siasa
na Diplomasia, Mawasiliano, Fedha na Uchumi, Nishati, Maendeleo na ujenzi wa
Miundombinu, Elimu na Mafunzo, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Utalii, Kilimo
na Uvuvi, Maji na Mazingira, Afya na Elimu.
=====================================================
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Uganda, Mhe. Aziz Mlima akifafanua utaratibu wa majadiliano ndani ya mkutano huo. |
Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania wakifuatilia mkutano. |
Ujumbe kutoka Tanzania. |
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania |
Ujumbe kutoka Uganda ukifuatilia mkutano. |
Viongozi wakitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kumalizika kwa zoezi la ufunguzi wa Mkutano huo. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.