Serikali ya Tanzania imepokea tani 16 za Dawa, Vifaa Tiba na Vifaa Kinga
ikiwa ni msaada wenye thamani ya shillingi milioni 864 kutoka Serikali ya Misri.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali wakati wa hafla fupi ya kupokea shehena
ya dawa hizo iliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi
amesema Tanzania inaishukuru Serikali ya Misri kwa msaada huo muhimu kwa
wananchi wa Tanzania na kwamba itandelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya
Misri hususan katika kuboresha sekta ya afya na kuahidi kuusimamia kikamilifu msaada huo ili uwafikie walengwa kwa wakati.
Pia aliongeza kusema kuwa, msaada
huo umewasili wakati mwafaka ambao Tanzania inaendelea kuboresha sekta ya afya kwa
kusogeza huduma za afya kwa wananchi pamoja na kuongeza upatikanaji wa Dawa na
Vifaa Tiba katika maeneo ya mijini na vijijini.
Aidha, alipongeza ushirikiano wa kidiplomasia uliopo
kati ya Tanzania na Misri ambao umekuwa wa manufaa makubwa tangu kuanzishwa
kwake na kupongeza jitihada zinazofanywa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha Sekta ya Afya nchini ambapo
alisema msaada huo ni miongoni mwa matokeo ya ziara ya Mhe. Rais aliyoifanya
nchini Misri mwezi Novemba, 2021.
"Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na pia kwa
niaba ya Waziri wa Afya. Mhe. Ummy Mwalimu napokea msaada huu wa Dawa na Vifaa
Tiba wenye thamani zaidi ya shilingi milioni 800 kutoka Serikali ya Misri. Kama
Serikali, tunaendelea kuboresha na kusogeza huduma za afya kwa wananchi hivyo
msaada huu utachangia jitihada hizo. Ninakuomba Mhe. Balozi ufikishe salamu
zetu za shukrani kwa Mhe. Abdel Fattah Al-Sisi, Rais wa Misri kwa msaada huu
ambao tumeupokea kwa dhati na utatimiza lengo lilokusudiwa la kuwasaidia wananchi
wa Tanzania" alisema Dkt. Makubi.
Kwa upande wake, Balozi wa Misri hapa nchini. Mhe.
Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na
Tanzania na inaunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya
uongozi makini wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania za kuwaletea watanzania maendeleo kupitia sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.
Kadhalika, Mhe. Balozi Abulwafa alieleza kuwa,
mbali na ushirikiano wa Tanzania na Misri kwenye sekta ya afya, Nchi yake itaendelea
kushirikiana na Tanzania katika kutoa fursa za mafunzo ya kuwajengea uwezo watu
wa sekta ya afya na fani mbalimbali kwa watanzania.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Aifelo Sichwale, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Bw. Daudi Msasi, Kaimu Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Celestine Kakele na Maafisa Waandamizi kutoka Serikalini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi kwa pamoja na Balozi wa Misri nchini, Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abulwafa wakisaini Hati ya Makabidhiano ya Dawa na Vifaa Tiba vilivyopokelewa nchini kutoka Misri
Afisa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bibi Faith Masaka akibadilishana mawazo na Afisa kutoka Ubalozi wa Misri hapa nchini, Bw. Mahmoud Hamdy Khalifa wakati wa hafla ya makabidhiano ya Dawa na Vifaa Tiba kutoka Misri |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.