Mtanzania anayeishi
nchini Canada Bw. Joseph Katallah ameonesha nia ya kuja kuwekeza nchini katika sekta ya
miundombinu kwa kushirikiana na kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya nchini Marekani hususan kwenye ujenzi wa barabara za lami kwa
kutumia teknolojia mpya iliyogunduliwa na kampuni hiyo.
Wawekezaji hao
wanaoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wapo
nchini kwa ziara ya wiki moja ambapo wanatumia fursa hiyo kukutana na wataalamu
wa sekta ya barabara
kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Wakala wa Barabara
Vijijini na Mijini Tanzania - TARURA, Wakala wa Barabara Tanzania -
TANROADS, na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Lengo la ziara ya wawekezaji hao pamoja na mambo
mengine ni kuitangaza teknolojia mpya ya utengenezaji wa barabara za lami
zisizotumia saruji ya kiwandani na badala yake zitatumia udongo mwekundu ambao
pia unapatikana nchini.
Wawekezaji hao wameeleza
kuwa Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kupewa kipaumbele katika uwekezaji wa
teknolojia hiyo kufuatia
uwepo wa rasilimali za kutosha hapa nchini zitakazowezesha matumizi ya teknolojia hiyo yenye gharama nafuu na rafiki kwa mazingira ili
iweze kutumika kuchochea maendeleo chanya kwa Taifa.
Wakati huo huo,
wataalamu kutoka sekta ya barabara wameeleza kuwa ni vema uwekezaji wa aina
hiyo ukafuata taratibu zilizowekwa katika mfumo wa Serikali na kuruhusu
kufanyika kwa tafiti inayopimika ili kujiridhisha na ufanisi wake katika ardhi
na hali ya hewa ya Tanzania.
Vilevile, wakaeleza
umuhimu wa teknolojia hiyo kufanyiwa majaribio katika maeneo korofi kufuatia
wawekezaji hao kueleza ufanisi wa teknolojia hiyo katika maeneo mengi korofi
ambayo kampuni zenye teknolojia nyingine zimeshindwa
kukidhi na kudhibiti changamoto hiyo.
Hivyo, kikao hicho
kiliazimia wawekezaji
hao wakutane na wataalamu wanaoshughulikia viwango vya ubora wa barabara nchini
ili kujihakikishia ubora na ufanisi wa teknolijia hiyo mpya kabla ya kufikia
hatua ya kukubaliana na uwekezaji huo. Pia
uhakiki huo utasaidia kufahamu unafuu wa gharama, uokoaji wa muda, sambamba na
upekee na uwezo wa teknolojia hiyo mpya ukilinganishwa na teknolojia
inayotumika sasa.
Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC inauzoefu wa
kufanya kazi katika nchi za Canada, Marekani na Uingereza. Kwa upande wa nchi za Bara la Afrika, pamoja
na kutoa kipaumbele kwa Tanzania pia nchi ya Ghana imeonesha kuhitaji kujifunza
teknolojia hiyo mpya.
Wajumbe wengine kutoka sekta za Ujenzi wakifuatilia kikao hicho. |
Kikao kikiendelea. |
Bi. Mwakawago akizungumza na Mhandisi John ngowi na Dkt. Philemon Msomba kutoka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TATURA) mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.