Wednesday, March 2, 2022

RAIS WA TCCIA NCHINI AFANYA ZIARA YA KIKAZI OMAN


Rais wa Chama Cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA), Bw. Paul Faraji Koyi,  amefanya ziara ya kikazi nchini Oman hivi karibuni.  Akiwa nchini Oman amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na wenye Viwanda ya Oman, Mhandisi Redha Jumaa Al Saleh.


Katika mazungumzo yao, ambayo yalihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Abasi Kilima, viongozi hao walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo kukuza biashara na uwekezaji baina ya pande hizo mbili ili kuzitumia kikamilifu fursa nyingi za kiuchumi zinazopatikana katika nchi hizi mbili na hatimaye kukuza kiwango cha biashara kati ya nchi hizi ambacho kwa sasa kinaonekana bado kipo chini.


Wakati wa mazungumzo hayo, Bw. Koyi aliueleza ujumbe wa Oman kuwa, zipo fursa nyingi nchini Tanzania ambazo Oman inaweza kunufaika nazo zikiwemo za uwekezaji wa Viwanda vya kuchakata mazao ya Kilimo, Utalii, Uzalishaji Umeme, Kilimo, Ujenzi wa nyumba na sekta ya usafirishaji wa anga na baharini. Kadhalika aliwajulisha kuwa, Serikali ya Tanzania inachukua hatua mbalimbali za kuboresha miundombinu ya umeme, barabara, reli na viwanja vya ndege Ili kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara.

Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Oman, Mhandisi Al Saleh aliwaeleza wajumbe kuwa, nchi hiyo imefungua milango ya uwekezaji katika Maeneo Huru ya Uwekezaji (EPZ) ya Salala, Duqm na Sohar. Aidha, Serikali ya Oman imetoa fursa kwa wawekezaji kutoka nje kutolazimika kuwa na ubia na mwekezaji mwenyeji.


Akizungumzia suluhisho la changamoto za ufanyaji biashara kati ya Tanzania na Oman, Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdalah Kilima amesema tayari Ubalozi huo umewasilisha pendekezo hapa nchini la kuanzisha safari za ndege ya mizigo kwenda Oman kupitia Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL). Pia Ubalozi umezungumza na mashirika ya meli nchini Oman ili kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya nchi hizi mbili

Wakati huohuo, Ujumbe wa Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima ya Tanzania walikutana na Viongozi wa Baraza la Biashara kati ya Oman na Tanzania wa upande wa Oman ambapo walikubaliana kufufua mikakati ya ushirikiano kupitia Kampuni ya Uwekezaji ya Oman na Tanzania (OTIC) iliyoanzishwa mwaka 2016.

Mbali na kushiriki mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Oman, Ujumbe wa TCCIA ulifanya ziara katika Kiwanda cha Taifa cha Chai cha Oman, wazalishaji wa chai ya MUMTAZ jijini Muscat na kupata maelezo ya utendaji wa kiwanda hicho ambapo pamoja na mambo mengine, Kampuni hiyo imeahidi kufuatilia fursa zilizopo nchini, ikiwemo upatikanaji wa chai.

Kwenye ziara hiyo, Rais wa TCCIA nchini alifuatana na Bw. Abdul Mwilima, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara Mkoa wa Kigoma; Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Nerbat Mwapele na Afisa Masoko Mwandamizi, Bi. Fatma Khamis.

 Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA), Bw. Paul Faraji Koyi (mwenye barakoa nyeupe) akiwa kwenye mazungumzo na  Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na wenye Viwanda ya Oman, Mhandisi Redha Jumaa Al Saleh (wa kwanza kulia).  Bw. Koyi alikuwa nchini Oman kwa ziara ya kikazi ya kuimarisha ushirikiano kati ya TCCIA na Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Oman. Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Abasi Kilima (mwenye suti nyeusi).

Viongozi wa Jumuiya za Wafanyabiashara wa Tanzania na Oman wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Abdallah Kilima ( wa nne kushoto) mara baada ya mazunungumzo  ya kuimarisha ushirikiano wa Taasisi zao.

Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA) akiwa kwenye mazungumzo na Ujumbe wa Kampuni ya Uwekezaji ya Oman na Tanzania (OTIC). Bw. Koyi alikuwa nchini Oman kwa ziara ya kikazi ya kuimarisha ushirikiano kati ya TCCIA na Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Oman.

Mhe. Balozi Kilima (wa pili kushoto) akiwa na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA), Bw. Paul Faraji Koyi (kushoto) walipotembelea kiwanda cha Chai cha Taifa cha Oman kinachozalisha chai ya MUMTAZ jijini Musact hivi karibuni. Bw. Koyi alikuwa nchini Oman kwa ziara ya kikazi.


 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.