Na Mwandishi wetu, Dar
Serikali imeendelea kuwasisitiza Wawekezaji na Wafanyabiashara kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kuwa Tanzania ni salama kwa biashara na uwekezaji na kuwasihi kuendelea kuwekeza kwa wingi.
Akizindua Ripoti ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya nchini ya mwaka 2022 kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema kuwa Tanzania ni salama kwa uwekezaji na ufanyaji wa biashara na kuwasihi wawekezaji kutoka mataifa ya Ulaya kuendelea kuwekeza kwa wingi nchini.
“Tunapoendelea na juhudi za kuimarisha mazingira ya biashara na kukuza uwekezaji nchini Tanzania, napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wawekezaji zaidi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuwekeza nchini Tanzania. Tanzania ni nchi yenye amani na utulivu na imejaaliwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji hasa katika maeneo ya kimkakati yakiwemo mafuta na gesi, madini, viwanda, utalii, uchumi wa bluu, kilimo na mifugo, amesema Balozi Mulamula.
Balozi Mulamula ameongeza kuwa, ripoti hiyo inaonyesha kuendelea kwa uhusiano mzuri na imara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya kwa maslahi ya ustawi wa uchumi. Ripoti hii itatumika kama kielelezo cha uwezekano wa kuibua wa uwekezaji wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania.
Napenda kuwahakikishia wawezeji na wafanyabiashara kutoka Umoja wa Ulaya kuwa ripoti iliyozinduliwa leo tumeipokea vyema na Serikali tutaendelea kufanya kazi ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini ili kuwavutia zaidi wawekezaji na wafanyabiashara.
Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Mhe. Mafredo Fanti amesema kuwa Umoja wa Ulaya ni mshirika mkuu wa biashara na uwekezaji kwa Tanzania, na kuongeza kuwa makampuni ya nchi 10 za EU zilikuja kuwekeza Tanzania Dola za Kimarekani bilioni 1.5 kati ya 2013 na 2020.
“Tunaamini kuwa Tanzania inatoa fursa kubwa zaidi za uwekezaji hivyo EU inaunga mkono sera ya Tanzania ya kuunganisha mfumo wa kisheria na kiutawala ili kuweza kuwavutia zaidi wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza hapa nchini,” amesema balozi Fanti
Uzinduzi wa Ripoti ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya nchini, umehudhuriwa na Mabalozi wa nchi za Ulaya, Jumuiya ya wafanyabiashara wa Ulaya nchini, Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe Pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge – Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. David Kihenzile.
Katika tukio jingine, Waziri Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Nigeria nchini Mhe. Hamisu Umar Takamawa na kujadili mambo ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Nigeria katika sekta za uwekezaji, biashara, elimu, madini na uhusiano wa kimataifa.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Mulamula amemhakikishia Balozi wa Nigeria ushirikiano wa kutosha wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake hapa nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Nigeria nchini, Mhe. Hamisu Umar Takamawa |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.