Bi Amina akiwasilisha nakala ya risala aliyoisoma kwa Mhe. Waziri Mulamula alipokutana na Watanzania wanaoishi nchini Saudi Arabia nyumbani kwa Balozi wa Tanzania jijini Riyadh |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Watanzania wanaoishi nchini Saudi Arabia na kuwataka kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania nchini humo.
Balozi Mulamula amekutana na Watanzania hao jijini Riyadh katika kikao kilichofanyika nyumbani kwa Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Ali Mwadini.
Akizungumza na Watanzania hao Balozi Mulamula amesisitiza juu ya umuhimu wa Watanzania hao kuishi kwa kufuata sheria na kanuni za nchi hiyo kwani kufanya hivyo kutaendelea kulinda taswira nzuri ya nchi yao.
Balozi Mulamula pia amewahahakishia watanzania hao juu ya nia ya Serikali ya kufanyia kazi mawazo na maoni yao ili kuwa kuwa na amani.
‘’Niwahakikishieni ndugu zetu mlioko huku, serikali yenu ni sikivu inathamini na kujali maoni mnayoyatoa na inayafanyia kazi, na muda si mrefu mtaona tulipofikia,” alisema Balozi Mulamula.
Awali katika risala yao kwa mhe. Waziri Watanzania hao walielezea changamoto na mafanikio yaliyopatikana kupitia umoja wao na kuiomba serikali kufanyia kazi changamoto wanazozipata hasa wakati wa kuondoka nyumbani.
Waziri Mulamula yuko nchini Saudi Arabia kwa ziara ya kikazi kufuatia mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mwana Mfalme, Mtukufu Faisal bin Farhan Al Saud, alioutoa mwezi Machi 2021 alipotembelea Tanzania.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.