Thursday, April 28, 2022

MAMLAKA YA MJI WA BUSAN KUSAIDIA KUENDELEZA UCHUMI WA BLUU NCHINI

Mamlaka ya mji wa Busan imeonesha utayari wa kuisadia Tanzania katika kuendeleza uchumi wa buluu na uvuvi.

Haya yamejili wakati wa mazumgumzo yaliyofanyika baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Mstahiki Meya Mhe. Park Heong Joon alipomtembelea ofisini kwake katika Mji wa Busan, Jamhuri ya Korea. 

Katika mazungumzo hayo Mhe. Park ameeleza kuwa mamlaka ya Mji wake imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza uchumi wa buluu na uvuvi na hivyo wameona ni wakati muafaka kwao wa kushirikiana na kuisaidia Serikali katika kuendeleza sekta hiyo. Mhe. Park aliainisha baadhi ya maeneo ambayo wanakusudia kusaidia ili kuiinua sekta hiyo ikiwemo kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wadau na wataalam wa sekta ya uchumi wa buluu na vifaa vya kisasa vya uvuvi. 

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukifuatilia na kuvutiwa na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza sekta ya uchumi wa bluu na uvuvi, tupotayari kutoa mchango wetu katika kuendeleza sekta hii muhimu kwa maendeleo ya wananchi na Serikali ya Tanzania” alisema Mstahiki Meya Mheshimiwa Park.

Kwa upande wake Waziri Mulamula alieleza kuwa Serikali ya Tanzania inatambua mafanikio makubwa ambayo Mamlaka ya mji wa Busan imeyapata kutokana na jitihada zao za kuendeleza sekta ya uchumi wa bluu, hivyo imekuwa ni nafasi hadhimu kwa Tanzania kupata fursa ya kushirikiana na kusaidiwa na mamlaka ya mji huo katika kundeleza uchumi wa buluu na uvuvi. 

“Kwa miaka 30 sasa tumeendelea kufurahia na kunufaika na matunda ya uhusiano mzuri wa kidiplomasia, leo hii ninayofuraha kubwa kuona uhusiano huu unafungua mlango mwingine mpya wa ushirikiano ambao utaleta manufaa makuwa kwa wananchi na Serikali yetu, nafurahi zaidi kuona hili linafanyika baina yetu na mamlaka ya Mji wa Busia ambao umepiga hatua kubwa katika sekta hii, kitu ambacho kinanipa matumaini kuwa tukitumia vyema uzoefu na maarifa tutakayopata kutoka kwenu tutapiga hatua kubwa ya maendeleo ndani ya muda mfupi” alieleza Balozi Mulamula. 

Sambamba na hayo Mstahiki Meya alieleza nia yake kushirikiana na Tanzania katika maeneo mengine mbalimbali ya kiuchumi na kijamii. Miongoni mwa vitu alivyovitaja katika maeneo hayo ni pamoja na kununua zao la kahawa ya Tanzania, kuanzisha ushirikiano na urafiki na mji mojawapo wa Tanzania, kuhimiza makampuni na wafanyabiashara wa Mji wake kuwekeza Tanzania na ushirikiano katika Utamaduni na Sanaa. 

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa mji wa Busan, Korea. 

Mazungumzo hayo yamefanyika sambamba na kongamano la biashara lililoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania kwa kushirikiana na mamlaka ya Mji huo. Kongamano hilo lililenga kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji na vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwa wafanyabiasha hao.

Akizungumza na wafanyabiashara hao Waziri Mulamula amewashawishi kuja nchini kuwekeza kwenye fursa zinazotokana na uchumi wa buluu, ambapo amewaeleza kuwa Tanzania ni sehemu salama kwa uwekezaji wao, vilevile, utashi na utayari wa kisiasa katika masuala ya uwekezaji kwa sasa umekuwa wa hali ya juu kuliko wakati mwingine wowote. Aliongeza kusema Serikali imefanya maboresho muhimu ya sera, sheria na kanuni za uwekezaji. 

“Tanzania tupo tayari na tunashauku kubwa ya kufanyakazi na sekta binafsi ya Busan katika kuendeleza sekta yetu ya uchumi wa buluu ambayo bado ipo chini kimaendeleo” Waziri Mulamula. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafanyabiashara hao wameonesha kuvutiwa na fursa walizoelezwa kupatikana katika sekta ya uchumi wa buluu na wameeleza nia na utayari wao wa kuwekeza katika sekta hiyo hapa nchini.

Katika tukio jingine Waziri Mulamula amekutana na kufanyamazungumzo na Mwenyekiti na Rais wa Eximbank ya Korea Bw. Moon Kyu, Bang katika Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Seoul, Korea.  

Waziri Mulamula yupo nchini Korea kwa ziara ya siku tano (5) kufuatia mwaliko wa Waziri wa Mambo ya Nje wanchi hiyo Mhe. Chung Eui-yong. Vilevile Waziri Mulamula atashiriki hafla ya maadhimisho ya miaka 30 ya uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea itayofanyika jijini Seoul tarehe 29 Aprili 2022. Tanzania na Korea zilianzisha uhusiano wa Kidiplomasia Aprili 29,1992.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akipokelewa na mwenyeji wake Mstahiki Meya wa Mji wa Busan Mhe. Park Heong Joon alipowasili ofisini kwake. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazunguzo na Mstahiki Meya wa Mji wa Busan, Korea Mhe. Park Heong Joon alipomtembelea ofisini kwake.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Mstahiki Meya wa Mji wa Busan, Korea Mhe. Park Heong Joon wakifurahia jambo walipokutana kwa mazungumzo 
Mazungumzo yakiendelea
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula na Mstahiki Meya wa Mji wa Busan, Korea Mhe. Park Heong Joon wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Serikali ya Tanzania na Mji wa Busan.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Rais wa Eximbank ya Korea Bw. Moon Kyu, Bang (wakwanza kulia) alipotembelea Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Seoul. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Balozi Liberata Mulamula na Rais wa Eximbank ya Korea Bw. Moon Kyu, Bang (wapili kushoto) wakiwa katika picha. Wengine ni Balozi wa Tanzania nchini Korea Mhe. Togolani Mavula (wapili kulia) Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia Balozi Caesar Waitara na baadhi ya watendaji wa benki hiyo. 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Balozi Liberata akimkabithi picha ya wanyama wa mbugani (yakuchorwa) Mstahiki Meya wa Mji wa Busan, Korea Mhe. Park Heong Joon

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.