Tuesday, April 5, 2022

MKUU WA MAJESHI YA ULINZI ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI AFRIKA KUSINI

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amewataka Watumishi wa Serikali wanaopata fursa ya kuiwakilisha nchi nje kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa bidii huku wakijua wao ni wawakilishi wa nchi kwenye maeneo waliyopangiwa.


Jenerali Mabeyo ametoa rai hiyo hivi karibuni alipotembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kwa lengo la kuwasalimia Watumishi wa Ubalozi huo.


Mkuu huyo wa Majeshi amesema kuwa, watumishi wa kada mbalimbali wanaopangiwa kufanya kazi kwenye Balozi za Tanzania au Mashirika ya Kikanda na Kimataifa wanatakiwa kutumia fursa hiyo kuiwakilisha nchi vizuri kwa kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kuwa wazalendo kwa nchi yao kwa maslahi mapana ya Taifa.


“Nawapongeza kwa kuendelea kuiwakilisha nchi yetu vizuri hapa Afrika Kusini lakini nawahimiza mchape kazi kwa bidii na kuwa wazalendo kwa nchi yenu wakati wote”, alisisitiza Jenerali Mabeyo.


Kuhusu hali ya nchi, Jenerali Mabeyo amewaeleza Watumishi hao kwamba, hali ya nchi na mipaka yote ni salama na kuwahimiza kuendelea kuiombea nchi na Viongozi wote akiwemo Mhe. Rais ili hali ya amani na utulivu iliyopo iendelee kuwepo.


Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi amemshukuru Jenerali Mabeyo kwa kutenga muda wake na kuutembelea Ubalozi huo na kuielezea hatua hiyo kuwa ni heshima kubwa kwake binafsi na Watumishi wote wa Ubalozi.


Kadhalika, alimweleza kuwa hali ya ushirikiano wa Tanzania na Afrika Kusini ni nzuri ambapo nchi hizi zinaendelea kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo biashara, utalii, elimu, uwekezaji na ushirikiano katika kukuza lugha ya kiswahiili. 


Aliongeza kusema moja ya jukumu kubwa la Ubalozi ni kutekeleza Diplomasia ya Uchumi. Hivyo, Ubalozi unaendelea kukamilisha mpango mkakati wa kutekeleza dhana hiyo ili kuiwezesha Tanzania kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo nchini humo zikiwemo za biashara, uwekezaji na masoko kwa bidhaa za Tanzania.


Mhe. Jenerali Mabeyo alikuwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambao ulihusisha pia Jamhuri ya Msumbiji na Nchi Zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) ambao ulifanyika jijini Pretoria kuanzia tarehe 01 hadi 03 Aprili 2022.

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi akimpokea Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo alipotembelea Ubalozi huo hivi karibuni. Jenerali Mabeyo alikuwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambao ulihusisha pia Jamhuri ya Msumbiji na Nchi Zinazochangia Vikosi katika Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) ambao ulifanyika jijini Pretoria kuanzia tarehe 01 hadi 03 Aprili 2022. 

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi akizungumza kumkaribisha Jenerali Mabeyo (hayupo pichani) Ubalozini.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Mhe. Jenerali Venance Mabeyo akizungumza na Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini (hawapo pichani) alipoutembelea Ubalozi huo hivi karibuni. Kushoto ni ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola. Jenerali Mabeyo na wajumbe wengine kutoka Tanzania walikuwa nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa SADC
Mhe. Jenerali Mabeyo akizungumza
Mkutano kati ya Jenerali Mabeyo na Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ukiendelea
Sehemu ya Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini wakimsikiliza Jenerali Mabeyo (hayupo pichani) alipowatembelea Ubalozini hapo
Sehemu nyingine ya Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini
Mhe. Balozi Milanzi akimkabidhi Jenerali Mabeyo zawadi ya saa kama ukumbusho kwa kutembelea Ubalozini hapo
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Milanzi
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Milanzi na Mhe. Balozi Kayola
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini
Mhe. Jenerali Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Tanzania ulioshiriki Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika nchini humo hivi karibuni


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.