Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambaye pia ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Dkt. Naledi Pandor amezipongeza Nchi Wanachama wa SADC zikiwemo zile zinazochangia vikosi nchini Msumbiji kwa kuendelea kujitolea kwenye masuala ya ulinzi wa amani kwa maslahi mapana ya wananchi wa Msumbiji na kanda ya SADC kwa ujumla.
Mhe. Pandor ametoa pongezi hizo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini tarehe 03 Aprili 2022.
Amesema Mkutano huo ni mwendelezo wa majadiliano yanayofanywa na Nchi Wanachama wa SADC kuhusu namna ya kuisadia Msumbiji katika kupambana na vitendo vya ugaidi na ukatili vilivyoripotiwa kwenye maeneo ya Kaskazini mwa Jimbo la Cabo Delgado.
“Nia ya dhati na msaada unaoendelea kutolewa kwa Msumbiji na Nchi Wanachama ni wa kupongezwa. Hii ni ishara kwamba sote tuna nia moja ya kupambana na ugaidi ambao unatishia jitihada zinazofanywa na jumuiya katika kukuza mtangamano wa SADC na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Hata hivyo niwahakikishie kuwa jitihada hizi si za bure zimezaa matunda” alisema Dkt. Pandor.
Kadhalika ameipongeza Misheni ya SADC nchini Msumbiji (SAMIM) kwa kazi nzuri wanayofanya ya kurejesha hali ya amani na utulivu na kuwawezesha wananchi wa Msumbiji hususan wale wanaoishi Kaskazini mwa nchi hiyo kwenye Jimbo la Cabo Delgado kuendelea na shughuli zao za maendeleo pasipo kuhofia vitendo vya ugaidi.
"Tumekutana hapa kwa niaba ya wakuu wetu wa Nchi na Serikali, kupokea na kujadili ripoti na mapendekezo kuhusu mwenendo wa Misheni ya SADC nchini Msumbiji. Niwajulishe tu Ripoti inatia moyo kwani mambo mengi mazuri yamefanyika tangu SAMIM ianze kazi nchini Msumbiji na hali ya usalama nchini humo hususan maeneo ya kaskazini mwa Jimbo la Cabo Delgado inaendelea kuimarika na wananchi wameanzaa kurejea katika shughuli zao za kawaida”, alisema Mhe. Pandor.
Pia alieleza umuhimu wa kufunguliwa kwa Kituo cha Kikanda cha Kupambana na Ugaidi ambacho kilizinduliwa rasmi tarehe 28 Februari 2022 jijini Dar Es Salaam, kwamba ni hatua muhimu katika kuimarisha usalama kwenye kanda ya SADC.
“Tumefurahishwa na uzinduzi wa Kituo cha Kikanda cha Kupambana na ugaidi nchini Tanzania tarehe 28 Februari 2022. Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa usalama wa kanda yetu ambao utafanya kazi kwa kushirikiana na Kituo cha Kanda cha Tahadhari za Mapema” alieleza Dkt. Pandor.
Vilevile alitumia nafasi hiyo kuushukuru Umoja wa Ulaya kwa kuendelea kuchangia kwenye maeneo mbalimbali ya Misheni hiyo na kutoa wito kwa washirika wengine wa maendeleo kuendelea kusaidia na kuunga mkono jitihada za SADC za kurejesha amani na usalama nchini Msumbiji na maeneo mengine.
Awali akimkaribisha Dkt. Pandor kuzungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Magosi alisema kuwa Sekretarieti ya SADC itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama wa SADC ili kuhakikisha lengo lilowekwa la kukomesha kabisa vitendo vya kigaidi nchini Msumbiji linatimia. Pia naye alizipongeza nchi wanachama na Misheni ya SADC iliyopo Msumbiji kwa kuendelea kujitolea kwa dhati na kueleza kuwa hali ya amani na utulivu imerejea kwa kiasi kikubwa nchini Msumbiji hususan kwenye maeneo ya kaskazini mwa Jimbo la Cabo Delgado.
Nchi Wanachama kumi (10) za Misheni ya SADC nchini Msumbiji ni Tanzania, Angola, Malawi, Lesotho,
Namibia, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Botswana, Zimbabwe na
Zambia.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo uliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe. Ujumbe huo unamjumuisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Gaudence Milanzi na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola.
|
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.