Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba
Mndeme amewataka Watanzania kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali zikiwemo za
ufadhali wa masomo zinazotangazwa na Serikali ili kunufaika nazo.
Balozi Mndeme ametoa rai hiyo leo tarehe 26 Mei
2022 jijini Dodoma alipokutana na wawakilishi wa vijana 26 wanaokwenda
nchini Marekani kushiriki mafunzo chini ya Program ya YALI kwa lengo
la kuwaaga.
Amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara mbalimbali
ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeendelea
kutangaza fursa mbalimbali zikiwemo za ajira na ufadhili wa masomo
zinazopokelewa nchini kutoka nchi mbalimbali lakini bado mwitikio wa Watanzania
wa kuchangamkia fursa hizo ni mdogo.
“Wizara imekuwa na utaratibu wa kutangaza fursa
nyingi za ufadhili wa masomo zinazopokelewa kutoka nchi mbalimbali
tunazoshirikiana nazo. Hata hivyo, bado fursa hizi hazijachangamkiwa ipasavyo.
Nawaomba Watanzania mzichangamkie fursa hizi pale zinapotangazwa ili
zitunufaishe” alisema Balozi Mndeme
Aidha, Balozi Mndeme aliwapongeza vijana hao kwa
kufanikiwa kuchaguliwa kushiriki program hiyo ambayo inaheshimika duniani
na kuwaeleza kuwa ni fursa nzuri kwao kuitumia kwa ajili ya kujifunza masuala
mbalimbali yakiwemo yanayohusu Uongozi ili kupitia wao vijana wengine wengi wa
Tanzania wanufaike. Pia aliwaasa kuwa Mabalozi wazuri wa Tanzania,
kuzingatia nidhamu na kutanguliza maslahi ya nchi mbele wakati wote wakiwa nchini
Marekani.
“Nawapongeza sana kwa kufanikiwa kupata fursa
hii. Wizara inafurahi kuona vijana wa Kitanzania mmepata fursa hii kwani pamoja
na kuwajenga pia ni ushahidi wa uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na
Marekani. Nawaasa mkawe mabalozi wazuri wa Tanzania mzingatie nidhamu ili
kulinda heshima na taswira nzuri ya nchi yetu” alisema Balozi Mndeme.
Kwa upande wao vijana hao waliishukuru na
kuipongeza Wizara kwa ushirikiano iliowapatia na kuahidi kuzingatia mafunzo
yote watakayoyapata wakiwa Marekani kwa maslahi mapana ya nchi.
Program ya YALI (Young African Leaders
Initiative) ilianzishwa na Serikali ya Marekani mwaka 2010 kwa lengo la
kuwawezesha vijana kutoka mataifa ya Afrika kwenda nchini humo kujifunza
masuala mbalimbali ya kuwajengea uwezo katika Uongozi. Vijana hao 26
wamechaguliwa kati ya Vijana wa Kitanzania 700 walioomba kujiunga na Program
hiyo kwa mwaka 2022.
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme akizungumza wakati wa kikao kifupi cha kuwaaga Vijana 26 wa Kitanzania (hawapo pichani) waliopata fursa ya kushiriki mafunzo nchini Marekani kupitia Program ya Young African Leaders Initiative (YALI) kwa mwaka 2022. Pamoja na mambo mengine aliwaasa vijana hao kuwa mabalozi wazuri wa Tanzania nchini Marekani ili kulinda heshima ya nchi. Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma tarehe 26 Mei 2022.
|
Mmoja wa vijana watakaoshiriki program ya YALI Bi. Victoria akizungumza wakati wa mkutano kati yao na Balozi Mndeme (hayupo pichani) |
|
Sehemu ya wawakilishi wa vijana 26 wa Kitanzania watakaoshiriki program ya YALI nchini Marekani wakimsikiliza Balozi Mndeme (hayupo (ichani) |
|
Sehemu nyingine ya vijana hao wakati wa mkutano kati yao na Balozi Mndeme |
|
Vijana watakaoshiriki program ya YALI nchini Marekani wakifuatilia mazungumzo kati yao na Balozi Mndeme |
|
Sehemu ya vijana hao wakati wa kikao cha kuwaaga |
|
Vijana watakaoshiriki program ya YALI nchini Marekani wakimsikiliza Balozi Mndeme alipozungumza nao kwa ajili ya kuwaaga |
|
Balozi Mndeme akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wawakilishi wa vijana 26 watakaoshiriki program ya YALI nchini Marekani |
|
Picha ya pamoja |
|
Picha ya pamoja |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.