Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya ziara ya kikazi katika Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (IRMCT) tarehe 21 Mei 2022 katika eneo la Lakilaki, jijini Arusha.
Pamoja na mambo mengine dhumuni
la ziara hiyo lilikuwa kukutana na Uongozi wa IRMCT na kujadili utekelezaji wa
majukumu mbalimbali ya kimsingi unaofanywa na taasisi hiyo sambamba na yale ya
kimahakama.
Waziri Mulamula alitumia
nafasi hiyo kueleza kuwa Tanzania inathamini imani inayotolewa na mashirika ya
kimataifa pamoja na kikanda ya kuifanya kuwa mwenyeji wa mashirika hayo na
kutoa nafasi za ajira kwa Watanzania.
‘’ Serikali inafuatilia kwa
karibu utendaji kazi wa Mahakama hii, hivyo ni vema mkatekeleza kwa tija
malengo mahsusi ya kuanzishwa kwake,” alisema Balozi Mulamula.
Pia akasisitiza kuwa Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano wa kiutendaji
wakati wowote itakapohitajika ili kuiwezesha Mahakama kutekeleza majukumu yake
ya msingi ikiwemo kukamilisha taratibu za kesi zilizosalia na lile la kuwa
kituo cha kumbukumbu kwa kesi hizo linatekelezwa kwa ufanisi.
Naye Msajili wa Mahakama hiyo Bw.
Abubaccar Tambadou amemshukuru Mheshimiwa Waziri Mulamula kwa kuthamini Mahakama
hiyo na kutenga muda wake kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji.
Pia akaeleza kuwa kikao hicho
kimewezesha kupatikana kwa ufumbuzi wa papo kwa papo katika baadhi ya mambo na
kuleta uelewa wa pamoja kati ya uongozi wa Mahakama na Serikali mwenyeji juu ya
masuala ya kiutendaji wa taasisi hiyo.
Naye Jaji wa Mahakama hiyo
Mheshimiwa William Sekule alifafanua kwa kina juu ya utekelezaji wa majukumu
mbalimbali ya kimahakama na pia akaeleza kuwa kufanikiwa kwa Mahakama hiyo
kunahitaji msaada kutoka kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na nchi mwenyeji
katika kutetea maslahi mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha uendeshaji wa shughuli
za taasisi.
‘’Naipongeza Tanzania kwa
kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kupigania upatikanaji wa bajeti ya uendeshaji
wa Mahakama, hivyo ni vema tukatambua thamani ya mahakama hii kuendelea kuwepo
nchini na kukamilisha majukumu yake,” alisema Jaji Sekule.
Tangu Baraza Kuu la Usalama la
Umoja wa Mataifa lipitishe Azimio Nambari 1966 mwaka 2010 la kuanzisha Mahakama
hiyo nchini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisimamia hatua
mbalimbali za awali ili kuhakikisha ujenzi wa Mahakama hii unakamilika hususan upatikanaji
wa eneo la ujenzi, uwepo wa huduma ya umeme, barabara na maji katika eneo la
Lakilaki Jijini Arusha.
================================================
Uongozi wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (IRMCT) ukifatilia majadiliano ya kikao. |
Kikao kikiendelea |
Picha ya Pamoja Waziri Mulamula na Msajili wa Mahakama Bw. Tambadou na Mhe. Jaji Sekule. |
Picha ya pamoja ujumbe wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ukiongozwa na Mhe. Waziri Mulamula na Uongozi wa IRMCT. |
Waziri Mulamula akipata maelezo katika chumba cha Mahakama na taratibu nyingine za uendeshaji wa kesi katika mahakama hiyo. |
Muonekano wa chumba cha Mahakama. |
Waziri Mulamula akipata maelezo kutoka kwa afisa anayesimamia Makavazi (Archieve) ya mahakama hiyo. |
Picha ya pamoja Mheshimiwa Waziri na Watanzania wanaofanya kazi IRMCT |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.