Wednesday, June 29, 2022

WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA CUBA AWASILI NCHINI KWA ZIARA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Rodrieguez Parrilla amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 29 hadi 30 Juni 2022.

Akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Parrilla amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb).

Wakati wa mapokezi hayo, Mhe. Balozi Mulamula ameeleza madhumuni ya ziara hiyo ni kuimarisha na kukuza ushirikiano wa kihistoria ulioasisiwa na Wasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Fidel Castor aliyekuwa Rais wa kwanza wa Taifa la Cuba.

Tanzania na Cuba zimeendelea kushirikiana katika maeneo ya afya, elimu, viwanda, na biashara. Pamoja na maeneo hayo, serikali hizo mbili zinatarajia kufungua maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za Kilimo, utalii, ushirikiano katika usimamizi wa masuala ya zimamoto na uokoaji, utamaduni pamoja na michezo.

Aidha, akiwa nchini Mhe. Parrilla pamoja na mambo mengine, atakutana na kufanya  mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Liberata Mulamula na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Mhe. Bruno Rodriguez Parrilla mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 29 Juni 2022 jijini Dar es Salaam.

Mhe. Balozi Mulamula na Mhe. Parrilla wakiteta jambo wakati wa mapokezi, nyuma ya viongozi hao wa kwanza kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Valentino Mlowola na pembeni yake ni Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis Despaigne. 

Kulia ni  Balozi Mulamula akiongea na Mhe. Parrila ambao alieleza kuwa ziara yake ni muhimu kwakuwa ina lenga kuimarisha na kukuza uhusiano wa kihistoria baina ya mataifa hayo mawili.
Kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Valentino Mlowola, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na Afisa Mambo ya Nje, Bi. Salma Rajab wakifuatilia mazungumzo.

Mazungumzo yakiendelea.



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.