Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba leo tarehe 12 Julai 2024 jijini Lusaka, Zamba amekutana kwa mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Elias Mpedi Magosi.
Katika mazungumzo yao ambayo yamefanyika pembezoni mwa Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa SADC uliomalizika leo jijini hapa, Mhe. Makamba amempongeza Mhe. Magosi kwa kazi kubwa inayofanywa na Sekretarieti hiyo katika kusimamia utekelezaji wa mipango, itifaki, na mikataba mbalimbali iliyopitishwa au kuridhiwa na nchi wanachama wa SADC.
Kadhalika viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Sekretarieti hiyo ikiwemo masuala ya uratibu na usimamizi wa Kituo cha SADC cha Kupambana na Ugaidi chenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam na matayarisho yanayoendelea wakati Tanzania ikijiandaa kuchukua Unyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama kuanzia mwezi Agosti 2024.
Akizungumza kuhusu usimamizi wa Kituo hicho, Mhe. Magosi amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Tanzania ya kukisimamia kikamilifu Kituo hicho tangu kianzishwe mwezi Februari 2022 na kwamba kwa mujibu wa makubaliano, Sekretarieti ya SADC inajiandaa kupokea jukumu hilo la kuendelea kukisimamia hapo mwezi Oktoba 2024 ili kutimiza malengo yaliyokusudiwa kwa nchi wanachama na kanda kwa ujumla.
Viongozi wengine kutoka Tanzania walioambatana na Mhe. Makamba kwenye kikao hicho ni pamoja na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jen. Mathew Mkingule na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri.
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Elias Mpedi Magosi akizungumza na Mhe. Makamba (hayupo pichani) |
Mkutano ukiendelea |
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri akishiriki mazungumzo |
Mhe. Makamba akiwa na Mhe. Magosi baada ya mazungumzo kati yao kumalizika |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.