Wednesday, July 10, 2024

WAZIRI MAKAMBA AZUNGUMZA NA WAZIRI MPYA ANAYESHUGHULIKIA USHIRIKIANO NA UHUSIANO WA KIMATAIFA WA AFRIKA KUSINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba leo tarehe 10 Julai 2024 akiwa jijini Lusaka, Zambia amezungumza kwa njia ya mtandao na Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Ronald Lamola.

 

Katika mazungumzo yao, Mhe. Makamba amempongeza Mhe. Lamola kwa kuteuliwa kwenye wadhifa huo hivi karibuni na kumuahidi ushirikiano kutoka kwake na Serikali ya Tanzania kwa ujumla ili kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kindugu uliopo baina ya nchi hizi mbili.

 

Vilevile viongozi hao wamejadili na kukubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ulinzi na usalama katika ukanda wa Kusini mwa Afrika pamoja na kuendelea kuwaunga mkono wagombea wa nafasi mbalimbali  wanaojitokeza kuwania nafasi kwenye mashirika ya  kikanda na kimataifa kutoka kwenye mataifa haya mawili.

 

Kupitia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ambayo wenyeviti wake ni Marais wa nchi hizi mbili, Mawaziri hao wamekubaliana  kuimarisha ushirikiano kwenye sekta za kimkakati ikiwemo biashara, uwekezaji na utalii ili kunufaika kiuchumi kupitia ushirikiano huo ambapo pia wamekubaliana kuandaa mkutano wa tume hiyo mapema mwaka 2025.

 

Katika kuimarisha sekta ya biashara na utalii, Mhe. Waziri Makamba pia alimjulisha Mhe. Lamola kwamba Shirika la Ndege la Tanzania  kuanzia mwezi Septemba 2024  litaanza kufanya safari zake mara nne kwa wiki nchini Afrika Kusini ikiwa ni ongezeko la safari tatu..

 

Kadhalika  viongozi hao wamezungumza na kukubaliana  kuendelea kushirikiana kwenye masuala yanayohusu ulinzi na usalama katika ukanda wa Kusini mwa Afrika na  katika masuala ya kikanda na kimataifa ikiwemo kuwaunga mkono wagombea wa nafasi mbalimbali  wanaojitokeza kuwania nafasi kwenye mashirika ya  kikanda na kimataifa kutoka kwenye mataifa haya mawili.

 

Aidha, Tanzania ikiwa mstari wa mbele wakati wa harakati za ukombozi kusini mwa Afrika, viongozi hao  wamekubaliana kushirikiana kwenye masuala ya utunzaji wa Historia na Urithi wa Ukombozi wa Afrika kwa vizazi vya sasa na vinavyokuja.

 

Mhe. Makamba pia alitumia nafasi hiyo kumkaribisha Mhe. Lamola kutembelea Tanzania na kumkubalia ombi lake la kumtafutia mwalimu wa kumfundisha Lugha adhimu ya Kiswahili.

 

Kwa upande wake, Mhe. Lamola alimshukuru Mhe. Makamba na Serikali ya Tanzania kwa ujumla kwa kuendeleza ushirikiano na nchi yake katika kipindi chote tangu enzi za harakati za ukombozi kusini mwa Afrika hadi sasa.

 

Katika hatua nyingine, Mhe. Lamola alimweleza Mhe. Makamba kuwa nchi yake inapongeza na kuunga mkono uamuzi wa Serikali ya Tanzania wa kuhamishia Makao makuu yake  jijini Dodoma na kwamba  nchi hiyo ipo katika hatua za upembuzi yakinifu ili kuitikia wito wa Serikali ya Tanzania wa kuzihimiza Balozi kuhamia katika jiji hilo.

 

Mhe. Makamba yupo nchini Zambia kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unatarajiwa kufanyika tarehe 11 na 12 Julai 2024.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza kwa njia ya mtandao na Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Mhe. Ronald Lamola ambapo pamoja na mambo mengine amempongeza kwa kuteuliwa katika wadhifa huo na kumwahidi ushirikiano. Mazugumzo hayo yamefanyika huku Mhe. Makamba akiwa jijini Lusaka, Zambia ambapo anatarajiwa kushiriki Mkutano wa 26 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC utakaofanyika tarehe 11 na 12 Julai 2024. Mkutano huo pia umehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (aliyeketi kushoto kwa Mhe. Waziri Makamba), Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ali Sakila na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mhe. James Bwana ambao walishiriki kwa njia ya mtandao.
Mhe. Waziri Makamba na ujumbe aliofuatana nao akiendelea na mazungumzo na Mhe. Lamola




 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.