Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.)
ameahidi kushirikiana na Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC) katika kukuza uchumi wa kanda.
Hayo yamejiri wakati
akichangia mada katika Mkutano wa Mawaziri wa SADC unaofanyika nchini Zimbabwe
kuanzia tarehe 13 hadi 16 Agosti, 2024 ambapo, Mhe. Kombo anashiriki mkutano
huo kwa mara ya kwanza tangu aapishwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
‘’Naahidi
kushirikiana nanyi katika kutekeleza mikakati ya kikanda kama ilivyoainishwa
katika Mkataba wa Uanzishwaji wa SADC na Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Kanda
(RISDP) wa mwaka 2020-2030’’ alisema Waziri Kombo.
Aidha, Waziri Kombo
ameeleza kwamba Tanzania itaendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za
Jumuiya ikiwa ni pamoja na ulipaji wa michango yake ili kuyafikia malengo ya
kanda hiyo.
Mkutano wa Mawaziri
wa SADC pia umefanya makabidhiano ya nafasi ya mwenyekiti wa Baraza hilo ambapo
mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Mawaziri wa SADC na Waziri wa Mambo ya Nje wa
Jamhuri ya Angola, Mhe. Balozi Tete António amekabidhi nafasi hiyo kwa Waziri
wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Balozi
Dkt. Fredrick Shava.
Wakati wa
makabidhiano hayo Mhe, Tete António amempongeza Mhe. Shava kwa kupokea majukumu
hayo na pia amesisitiza juu ya umuhimu wa kuondolewa vikwazo vya kiuchumi
ilivyowekewa Zimbabwe, ushirikishwaji wa wanawake katika maamuzi mbalimbali ya
kijamii, kiuchumi na kisiasa na ushirikishwaji wa vijana katika shughuli za
maendeleo.
Kwa upande wake Mhe.
Shava ameshukuru kwa kuaminiwa kukabidhiwa jukumu hilo na ameeleza kuwa
Zimbabwe ipo tayari kushirikiana na nchi wanachama kufikia malengo na
vipaumbele vya jumuiya hiyo. Pia, amesisitiza umuhimu wa kuishirikisha sekta
binafsi katika kukuza uchumi na kuhimiza ulipaji wa michango ili kuiwezesha
jumuiya hiyo kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
=====================================
Meza kuu ikiongoza mkutano |
Picha ya pamoja. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.