Timu hiyo ikiwa imevalia jezi nadhifu zilizopendezeshwa kwa rangi ya njano na buluu, yenye kuvutia machoni mwa mashabiki waliojitokeza kuutazama mtanange wa kukata na shoka kati ya timu hiyo na Timu ya Ujenzi uliochezwa katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro (Mji kasoro Bahari) majira ya saa tatu asubuhi ya tarehe 24 Septemba 2024, ilijituma kikamilifu hadi kutoka sare ya 0-0 na timu hiyo hatua iliyofanikisha timu ya Nje kusonga mbele hatua ya makundi.
Akizungumza kwa njia ya simu ili kuwapa hamasa wachezaji hao, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Chiku Keguhe amewapongeza wachezaji wote wa Nje – Sports kwa kuingia 16 Bora, na kuwakumbusha kuwa Wizara ipo pamoja nao hatua kwa hatua.
“Nawapongeza kwa kufuzu kuingia 16 bora, mmeiheshimisha Wizara na hii ndio maana sahihi ya Diplomasia ya Michezo. Pongezi kwenu wachezaji kwa kuendelea kupambana na kuhakikisha mnachukua ushindi. Tusisahau matarajio ya Viongozi na Menejimenti ya Wizara ni kupata Vikombe” amesema Bi. Chiku Keguhe.
Akizungumza mara baada ya kufuzu hatua hiyo, Kocha wa Nje – Sports, Bw. Shabani Maganga amewapongeza wachezaji wake kwa kuendelea kuonesha mchezo mzuri unaoakisi Diplomasia ya Michezo na kuwasihi kuendelea kupambana na kuhakikisha wanafika fainali.
Nje Sports wanaume imeendelea kupata matokeo mazuri na kuifanya kuwa nafasi ya pili kwenye kundi H, huku wachezaji wake wakiendelea kujifua kikamilifu kwq lengo la kuchukua ushindi wa SHIMIWI kwa mwaka 2024–2025.
Ikumbukwe kuwa, mbali na mpira wa miguu, Timu ya Nje–Sports pia inashiriki Mchezo wa Kamba kwa Wanawake na Netiboli ambayo yote imeingia kwenye hatua ya makundi 16 bora.
Timu zote za Nje–Sports zitaendelea na mazoezi mepesi huku zikisubiri ratiba ya mchezo wa makundi unaotarajiwa kutolewa na viongozi wa Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI).
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.