Saturday, November 16, 2024

MAAFISA MAMBO YA NJE WAFAIDIKA NA UZOEFU WA MABALOZI WASTAAFU


 Mafunzo ya siku tano kuhusu mawasiliano ya Kidiplomasia kwa watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki yamehitimishwa jijini Dodoma Novemba 15, 2024, huku watumishi wakitakiwa kutumia ujuzi waliopata kutoka kwa Mabalozi Wastaafu na Mahiri kuboresha utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Wakufunzi wa semina hiyo, walisisitiza umuhimu wa mafunzo yaliyotolewa kuzingatiwa na washiriki kwa kuwa mawasiliano ya kidiplomasia yanahusisha nchi na nchi, mashirika ya kikanda na kimataifa, hivyo ni jambo muhimu kwa sababu linagusa sura ya nchi. 

Mafunzo hayo yalilenga mbinu za kuandaa nyaraka za mawasiliano ya kidiplomaisa zenye ubora, matumizi sahihi ya lugha na kwa kuzingatia wakati, Mabalozi walibainisha kuwa, ili lengo hilo liweze kutimia, washiriki wametakiwa kuwa mbele ya muda kwa kufahamu yanayotokea duniani na kusoma vitabu na nyaraka nyingine ambazo zitawapa ujuzi wa aina mbalimbali ikiwemo utajiri wa misamiati.

Mabalozi walieendelea kwa kueleza kuwa utekelezaji wa majukumu utakaozingatia weledi utaifanya Wizara hiyo iendelee kuwa kiungo muhimu cha Serikali katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi na kuhimiza umuhimu wa diplomasia ya umma kuimarishwa ili wananchi waelewa nafasi nyeti ya Wizara katika kukuza uchumi wa nchi.

Kwa upande wao, washiriki wa mafuunzo hayo waliahidi kufanyia kazi masomo waliyoyapata ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa kwa njia ya vitendo, ili nafasi ya Wizara katika nchi iendelee kuimarika kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.

Mabalozi wastaafu walioendesha mafunzo hayo ni Balozi Bertha Semu-Somi; Balozi Mohammed Maundi; Balozi  Peter Kallaghe, Balozi Begum Taj; Balozi Tuvako Manongi na Bw. Khamisi Abdallah.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.