Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb) akizungumza na wajumbe wa Tanzania wanaoshiriki Mkutano wa sita wa JPCC kati ya Tanzania na Malawi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, amezitaka taasisi za umma na sekta binafsi kushirikiana kwa karibu na kuchangamkia fursa mbalimbali za maendeleo kwa lengo la kukuza uchumi na kuhakikisha maendeleo endelevu.
Akizungumza na ujumbe wa Tanzania unaoshiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi, Waziri Kombo alisisitiza kuwa mshikamano wa wadau wa sekta zote ni nguzo muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
"Maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila mshikamano thabiti kati ya taasisi zetu. Ushirikiano wa karibu, mbinu bunifu, na matumizi sahihi ya fursa zilizopo ni nyenzo muhimu kwa mafanikio ya pamoja," alisema Waziri Kombo.
Aidha, alihimiza
washiriki wa mkutano huo kutumia majukwaa kama JPCC kuimarisha ushirikiano wa
sekta mbalimbali ili kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo
inayolenga kuinua uchumi wa mataifa yote mawili.
Kwa upande wake,
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Said Shaib Mussa, alisisitiza umuhimu wa taasisi za umma kushirikiana
kwa karibu kupitia vikao kama ili kubaini maeneo mapya ya ushirikiano, kutatua
changamoto kwa pamoja, na kuboresha utekelezaji wa miradi iliyopo.
"Ni muhimu kushirikiana kwa karibu, hasa tunapokuwa kwenye majukwaa kama haya, ili kutatua changamoto zinazotukabili kwa pamoja na kufanikisha malengo ya maendeleo," alisema Balozi Mussa.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umejumuisha viongozi na maafisa kutoka taasisi za umma, ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wengine ni Wizara ya Nishati, Wizara ya Miundombinu, Mawasiliano na Usafirishaji ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Ulinzi na Usalama, Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na Idara ya Uhamiaji.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.