Saturday, February 22, 2025

WAANDISHI WAENDESHA OFISI WAHIMIZWA KUTUMIA MFUMO WA UNUNUZI WA KIELEKTONIKI KWA UFANISI.

Waandishi Waendesha Ofisi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wametakiwa kutumia ujuzi walioupata kupitia mafunzo ya Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kielektroniki (NeST) kwa ufanisi na uwajibikaji ili kuboresha utendaji kazi wao, kuongeza uwazi na kuimarisha mifumo ya ununuzi wa umma. 

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Bw. Kawina Kawina alipofunga mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara Mtumba jijini Dodoma.

Bw. Kawina amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha mfumo wa NeST unatumika ipasavyo katika mchakato wa ununuzi wa vifaa na huduma mbalimbali wizarani.

Amefafanua kuwa serikali imewekeza katika mifumo ya kidijitali ili kurahisisha utendaji kazi, kuongeza uwazi, na kupunguza mianya ya upotevu wa rasilimali.

Vilevile amesisitiza kuwa maarifa waliyopewa hayapaswi kubaki kama nadharia pekee bali wanapaswa kuyatumia kwa vitendo katika majukumu yao.

"Serikali imewekeza katika mifumo hii kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji na kurahisisha utendaji kazi. Hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa maarifa haya mliyoyapata mnayatenda kwa vitendo ili kuongeza ufanisi wa ununuzi wa umma," alisema Bw. Kawina

Aidha amesisitiza kutumia mfumo huo kwa weledi, na kuwasihi kuwa mabalozi wazuri wa NeST ndani ya wizara kwa kushirikiana na wenzao na kuhakikisha kuwa kila hatua ya ununuzi inafuata taratibu na miongozo ya serikali. 

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru wizara kwa kuwawezesha kupata ujuzi huo, na kuahidi kuutumia kwa ufanisi ili kuboresha utendaji wao wa kazi.

Washiriki hao pia wamebainisha kuwa mafunzo hayo yamewapa uelewa wa kina kuhusu taratibu za manunuzi kwa njia ya mtandao na namna ya kuhakikisha kila hatua inafuata sheria.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika katika ukumbi wa Wizara, Dodoma kuanzia tarehe 18 hadi 20 Februari 2025.


Mkurugenzi Msaidizi wa idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Kawina Kawina akizungumza kwa niaba ya Menejimenti ya wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati wa hitimisho la mafunzo ya Manunuzi ya Umma ya Kielektroniki kwa Waandishi Waendesha Ofisi wa Wizara hiyo.

Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.