Friday, May 16, 2025

TANZANIA NA FINLAND ZAJIDHATITI KUSHIRIKIANA KATIKA BIASHARA NA UWEKEZAJI

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.)


 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Thabit Kombo (Mb.), amesisitiza dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na Jamhuri ya Finland kwa manufaa ya pande zote.

 

Msimamo huo ameutoa jijini Dar es Salaam alipozungumza katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Finland, lililowakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi za Tanzania na Finland.

 

Mhe. Kombo amewahakikishia wawekezaji kutoka Finland kuwa Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini na kuongeza kuwa maboresho hayo yanalenga kurahisisha utoaji wa leseni, kupunguza urasimu na kuboresha mifumo ya forodha ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wawekezaji.

 

Amebainisha kuwa Serikali iko tayari kushirikiana na kuhudumia wawekezaji kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

 

Waziri Kombo ametaja teknolojia ya habari na mawasiliano, afya, dawa, na teknolojia za kilimo kuwa ni miongoni mwa sekta zenye fursa kubwa za uwekezaji na ushirikiano.

 

Amesema Tanzania haitaki kuwa soko tu la bidhaa kutoka Finland, bali inataka kuwa mshirika wa muda mrefu na wa kuaminika katika biashara na uwekezaji.

 

Aidha, amewahimiza wafanyabiashara wa Kitanzania kuchangamkia  fursa zilizopo katika soko la Finland na kubainisha kuwa Finland inathamini ubora, uendelevu na uwazi ambapo bidhaa za asili kutoka Tanzania zina uwezo wa kuvifikia na hivyo kuimarisha biashara kati ya nchi hizo.

 

Naye Rais wa Jamhuri ya Finland, Mheshimiwa Alexander Stubb, amepongeza jitihada za Tanzania za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuelezea kuwa Finland iko tayari kushirikiana bega kwa bega na Tanzania katika maeneo ya Elimu na Ufundi, nishati, afya, kilimo na mazingira kwa manufaa ya pamoja.

Mheshimiwa Rais Stubb amesisitiza kuwa Finland inaiona Tanzania kama lango muhimu kuelekea masoko ya Afrika Mashariki.

 

Rais wa Finland yupo nchini kwa ziara ya kitaifa na ameambatana na ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji  kutoka Finland.

 

Rais wa Jamhuri ya Finland, Mheshimiwa Alexander Stubb

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.)
 

 


Rais wa Jamhuri ya Finland, Mheshimiwa Alexander Stubb


Rais wa Jamhuri ya Finland, Mheshimiwa Alexander Stubb

Naibu Waziri wa Biashara za Kimataifa wa Finland, Mhe. Jarno Syrjälä.

Mkurugenzi idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga.


 

Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Gilead Teri









 



Saturday, April 12, 2025

SERIKALI YATOA WITO KWA DIASPORA KUWEKEZA NYUMBANI


Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb)



Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ametoa wito kwa Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora) kuchangamkia fursa ya kuwekeza nyumbani, akisema kuwa mchango wao ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.

Mhe. Chumi ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa Akaunti ya Mzawa, huduma maalum ya kifedha kwa diaspora iliyozinduliwa na Benki ya Absa Tanzania.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mhe. Chumi ameipongeza Benki ya Absa kwa ubunifu wa huduma hiyo ambayo inalenga kupunguza changamoto wanazokutana nazo Watanzania wanaoishi ughaibuni, hususan katika kupata huduma za kifedha, kutuma fedha, na kushiriki katika uwekezaji wa ndani.

“Akaunti hii ni suluhisho la changamoto za kifedha kwa diaspora. Inawaruhusu kufungua akaunti, kutuma fedha, kuwekeza, na kutumia sarafu 5 tofauti wakiwa popote duniani.
” Amefafanua mhe. Chumi

Amefafanua kuwa mchango wa diaspora umekuwa ukiongezeka kila mwaka, akitaja kuwa mwaka 2022 pekee, Watanzania waishio nje walituma nchini fedha za kigeni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi trilioni 1.4. Amesema fedha hizo zimechangia maendeleo ya sekta mbalimbali kama elimu, afya, biashara, na ujenzi wa makazi.

“Serikali inatambua nafasi muhimu ya diaspora. Ndiyo maana tumekamilisha mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje inayojumuisha masuala ya diaspora, tumeanzisha mfumo wa kidijitali wa usajili wa diaspora, tumepitisha hadhi maalum kwa Watanzania wasio raia, na kuanzisha vitengo mahsusi serikalini vya kushughulikia masuala yao,” ameongeza Mhe. Chumi

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laizer, amesema huduma hiyo imebuniwa kwa kuzingatia maoni ya Watanzania waishio nje, na kwamba benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza uwekezaji wa ndani na biashara jumuishi.

Hafla hiyo pia imehudhuriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Salvator Mbilinyi, mabalozi wastaafu, na wadau mbalimbali wa sekta ya kifedha na uwekezaji.

 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb)

 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. David Cosato Chumi (kulia) akiwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laizer (kushoto)
 
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laizer

 

Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Salvator Mbilinyi