Tuesday, March 11, 2025

Wanafunzi NDC watembelea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akizungumza wakati wa kuwakaribisha Wanafunzi wa kozi ya 13 kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) na Uongozi wa Chuo hicho Wizarani jijini Dodoma. 

Wanafunzi wa kozi ya 13 kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) na uongozi wa Chuo hicho umetembelea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Ziara hiyo ya mafunzo imelenga kutoa nafasi kwa Wanafunzi hao kujifunza kuhusu historia ya Wizara , Sera ya Mambo ya Nje na majukumu yanayotekelezwa na Wizara kwa wakati huu.

Akizungumza wakati wa kuwakaribisha Wanafunzi hao Wizarani Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo alielezea juu ya mabadiliko ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 ambayo alieleza kuwa yamefanyika ili kuiwezesha Sera hiyo kuendana na mahitaji ya wakati uliopo na huku ikikidhi mahitaji ya wakati ujao.

“Tunayo Sera ya Mambo ya Nje ambayo tulitengeneza mwaka 2001 lakini sera hiyo sasa tumeifanyia maboresho ili iweze kuendana na mabadiliko mbalimbali ambayo yametokea duniani" alisema Balozi Shelukindo.

Alisema maboresho hayo yataiwezesha Sera ya Mambo ya Nje kukidhi mahitaji ya wakati huu na wakati ujao.

Balozi Shelukindo pia alisisitiza kuwa pamoja na maboresho hayo bado Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania imeendelea kusimamia katika misingi yake ile ile ya ujirani mwema, kutokufungamana na upande wowote, kutokuonea wanyonge, kuwa na Afrika yenye Umoja, na kutekeleza malengo ya Maendeleo ya Umoja wa mataifa. 

Balozi Shelukindo ametumia nafasi hiyo kuihakikishia NDC kuwa Wizara itaendelea kushirikiana nao wakati wote ili kuhakikisha NDC inaendelea kuwa kituo bora cha mafunzo nchini na kutoa Wanafunzi mahiri kwa manufaa ya Taifa.

Akizungumza wakati wa utambulisho wa wanachuo hao Mkuu wa Chuo cha NDC Meja Jenerali Balozi Wilbert Ibuge alisema wanafunzi waliotembelea Wizarani ni wa kozi ya 13 kwa mwaka 2024/2025 ambapo 40 wanatoka Jeshini na katika Wizara, Idara na Taasisi za Umma nchini na Wengine 21 wanatoka katika nchi rafiki za Bangladesh, Botswana, Burundi-2, Ethiopia, Misri-2, India, Kenya-2, Malawi, Namibia,Nigeria,Rwanda-2, Sierra Leone, Afrika Kusini, Uganda, Zambia-2 na Zimbabwe.

Amesema ziara ya wanafunzi hao Wizarani imelenga kuwapatia wanachuo hao mafunzo kwa vitendo ikizingatiwa kuwa masuala ya mambo ya nje na sera ya mambo ya nje ni miongoni mwa masuala Makuu ambayo wanafundishwa chuoni hapo.

“Chuo chetu katika kozi hizo za Ulinzi na Strategia focus yetu kubwa ni kuhusu masuala ya ulinzi na mambo ya nje na hapa wamekubaliana Leo ili asilia kutoka kwa wahusika ambao wanatekeleza majukumu hayo kwa vitendo".

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) Meja Jenerali Balozi Wilbert Ibuge akizungumza wakati alipoongoza ujumbe wa chuo kutembelea Wizara ya  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dodoma.

Picha ya pamoja
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa (DMC) katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Noel Kaganda akiwasilisha mada  kwa Wanafunzi wa kozi ya 13 kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) na Uongozi wa Chuo hicho Wizarani jijini Dodoma
Sehemu ya Wanafunzi wa kozi ya 13 kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) 
Sehemu ya Wanafunzi wa kozi ya 13 kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) 

Sehemu ya Wanafunzi wa kozi ya 13 kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) 



Mkurugenzi wa Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi John Ulanga kiwasilisha mada  kwa Wanafunzi wa kozi ya 13 kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) na Uongozi wa Chuo hicho Wizarani jijini Dodoma





Saturday, March 8, 2025

WANAWAKE DODOMA WAUNGANA KUSHEREHEKEA SIKU YA WANAWAKE KIMATAIFA





Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Makao Makuu Dodoma pamoja na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, wameungana na wanawake kutoka ofisi mbalimbali za umma na binafsi jijini Dodoma kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake duniani kwa mwaka 2025.

 Maadhimisho hayo, ambayo hufanyika kila Machi 8, yameandaliwa kwa lengo la kutambua mchango wa wanawake katika jamii na kuhimiza usawa wa kijinsia.

Maadhimisho hayo kimkoa yamefanyika katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, yakiwa na kaulimbiu isemayo: "Wanawake na Wasichana Tuimarishe Haki, Usawa na Uwekezaji."

Kaulimbiu hiyo inalenga kusherehekea mafanikio ya wanawake, kujadili changamoto wanazokabiliana nazo, na kutafuta njia za kuimarisha haki, usawa, na uwekezaji kwa maendeleo endelevu.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mheshimiwa Alhaj Jabir Shekimweri, ambaye alisisitiza umuhimu wa haki za wanawake na ushiriki wao katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Aidha, alieleza kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa katika elimu, uchumi, na uongozi.

Mheshimiwa Shekimweri alitoa wito kwa jamii kuendelea kupinga ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi stahiki kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa taifa. “Tukiwekeza kwa wanawake na wasichana, tunaiwekeza jamii katika maendeleo endelevu. Haki na usawa si jambo la hiari bali ni msingi wa maendeleo ya taifa letu,” alisema Shekimweri.

Pia, amewahimiza wadau kushirikiana kuwawezesha wanawake kiuchumi na kielimu na kusisitiza kuwa haki inapaswa kwenda sambamba na wajibu, akiwataka wanawake na wasichana kuwa mstari wa mbele kutumia fursa zinazotolewa kwa nidhamu, bidii, na maadili mema.

Aliongeza kuwa matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ni muhimu katika kudumisha maadili ya Kitanzania, huku akihimiza jamii kutumia teknolojia kwa maendeleo chanya.

Katika maadhimisho hayo, wanawake kutoka sekta mbalimbali walishiriki uzoefu wao na kutoa hamasa kwa wenzao juu ya njia bora za kufanikisha malengo yao. Pia, vikundi vya ujasiriamali vilipata nafasi ya kuonyesha bidhaa zao, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uwekezaji kwa wanawake na kuwawezesha kiuchumi.

Maadhimisho hayo yaliambatana na michezo mbalimbali, ambapo washindi walitunukiwa medali na vikombe kama ishara ya kutambua juhudi zao na mchango wao katika jamii. Kaulimbiu ya mwaka huu inaendelea kuwa mwangaza kwa wanawake na wasichana kote nchini, ikiwahimiza kuimarisha haki, usawa, na uwekezaji kwa ustawi wa jamii na maendeleo endelevu ya taifa.

 

Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mheshimiwa Alhaj Jabir Shekimweri, akitoa hotuba kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika kimkoa, jijini Dodoma, katika viwanja vya Chinangali Park.
 




















Friday, March 7, 2025

UJUMBE WA SERIKALI YA FINLAND WATEMBELEA MJI WA SERIKALI MTUMBA.

 



Ujumbe wa Serikali ya Finland umetembelea Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma na kukagua kiwanja kilichotengwa kwa ujenzi wa ubalozi wa nchi hiyo katika eneo hilo la Mji wa Serikali.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Finland katika kuhakikisha inaimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati yake na Tanzania.

Ujumbe huo umeongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika, Mashariki ya Kati na Amerika ya Kusini katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, Bi. Helena Airaksinen, ambaye aliambatana na Balozi wa Finland nchini Mhe. Theresa Zitting.

Baada ya ukaguzi wa eneo hilo, Bi. Airaksinen alieleza kuridhishwa kwake na mazingira ya kiwanja hicho, akibainisha kuwa kinatoa fursa kwa Finland kuendelea kuimarisha uwepo wake nchini Tanzania.

Aidha, alisifu jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuboresha miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba ili kuwezesha shughuli za kidiplomasia na utoaji wa huduma mbalimbali za serikali.

Kwa upande wake, Mhe. Balozi Zitting alisisitiza dhamira ya Finland ya kuendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali, hususani katika sekta za maendeleo, biashara, na diplomasia.

Alieleza kuwa hatua ya nchi yake kujenga ubalozi makao Makuu ya Serikali Dodoma ni ishara ya ushirikiano imara kati ya nchi hizo mbili.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa Finland pia ulitembelea maeneo mbalimbali katika Mji wa Serikali Mtumba zikiwemo ofisi za serikali na maeneo yanayoendelea kuendelezwa na hivyo kupata  fursa ya kujionea kwa kina mwelekeo wa serikali katika kuimarisha utendaji wa taasisi zake.

Ujumbe wa Tanzania katika ziara hiyo ulijumuisha maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Ofisi ya Jiji la Dodoma.

Maafisa hao waliwasilisha taarifa kuhusu maendeleo ya Mji wa Serikali na juhudi zinazoendelea kufanywa ili kuhakikisha unakuwa kitovu cha shughuli za serikali na kidiplomasia nchini.

Ziara hii inaashiria hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Finland, huku ujenzi wa ubalozi wa Finland jijini Dodoma ukitarajiwa kuimarisha zaidi ushirikiano wa kidiplomasia na maendeleo kati ya nchi hizo mbili.



 

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Afrika, Mashariki ya Kati na Amerika ya Kusini katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, Bi. Hellena Airaksinen(Kushoto) na Balozi wa Finland nchini Mhe. Theresa Zitting (kulia).