Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe,
Mhe. Dkt. Emmerson Mnangagwa amezindua
ujenzi wa Makumbusho ya Urithi wa Afrika na kukabidhi eneo la hekta moja (1) kwa
ajili ya uhifadhi wa historia ya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika
linalotambulika kama Kituo cha Ukombozi wa Nchi za SADC au “SADC Liberation
Square”
Mhe. Mnangagwa alikabidhi
Kituo hicho rasmi kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya
SADC, ambapo kilipokelewa kwa niaba na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo
Kusini mwa Afrika (SADC) Mhe. Elias Magosi na kueleza kuwa Kituo hiko
kitachangia juhudi za Kanda za kuenzi michango ya Wapigania uhuru katika
harakati za ukombozi na pia ni miongoni mwa utekelezaji wa mkakati wa kuenzi
Waanzilishi wa SADC.
Kwa upande wake, Mhe.
Mnangagwa alikiri kuwa Kituo cha Ukombozi wa Nchi za SADC kitachangia uhifadhi
wa historia muhimu za ukombozi ambazo zinaendelea kuandaliwa chini ya mpango wa
kujenga Makumbusho ya SADC jijini Gaborone na ule wa kujenga Makumbusho ya
Urithi wa Afrika nchini Tanzania. Hali kadhalika, Mhe. Mnangagwa alizialika
nchi wanachama za SADC kuchangia katika kuboresha Kituo hicho kwa kuwasilisha
zana za Sanaa kutoka nchini mwao zinazoelezea historia ya ukombozi wa nchi za
kusini mwa Afrika.
Makabidhiano ya eneo hilo
yameenda sambamba na ziara ya kutembelea eneo la mradi pamoja na zoezi la kupanda
mti ambao ulipandwa na Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Magosi na kushuhudiwa na
Wakuu wa Nchi na Serikali walioshiriki ziara hiyo akiwemo, Mhe. João Lourenço, Rais wa Jamhuri ya
Angola, Mtukufu Mswati III, Mfalme wa Eswatini, Mhe. Andry Rajoelina, Rais wa
Jamhuri ya Madagascar, na Mhe. Mokgweetsi Masisi, Rais wa Jamhuri ya Botswana.
Ziara hiyo ilikuwa ni
muendelezo wa ratiba ya Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika
tarehe 17 Agosti 2024. Akihutubia katika hafla ya makabidhiano ya eneo hilo, Mhe.
Mnangagwa ameeleza kuwa mradi huo unalenga kuwaenzi wanaharakati wa kweli na
wana wa Afrika waliojitoa muhanga katika kupigania ukombozi wa nchi zao. Hivyo,
ni heshima kubwa kwa mataifa yetu kutambua mchango wao na kuona fahari kuienzi
historia yetu.
Aidha, Wakuu hao wa nchi na
Serikali walitembelea pia Kituo cha uchakataji taka cha Geo Pomona cha jijini
Harare ambacho awali kilikuwa dampo na baadae kuanza kuchakata taka kwa ajili ya kuzalisha
nishati ya umeme sambamba na kutoa ajira mbalimbali kupitia shughuli za kituo
hicho.
Mradi huo una uwezo wa
kukusanya taka ngumu zenye uzito wa tani 1000 na kuzaliwa kiasi cha Megawati 16
hadi 22 za umeme kwa ajili ya kuunganisha kwenye gridi ya Taifa kwa matumizi ya
umma wa Zimbabwe.
Akihutubia katika uzinduzi
huo, Mhe. Mnangagwa ameeleza kuwa eneo hilo awali lilikuwa limekithiri kwa
uchafu na wingi wa taka na hivyo kupatikana kwa teknolojia bora na ya kisasa ya
kuchakata taka imesaidia kutunza mazingira kwa kuteketeza taka hatarishi pasipo
kuleta madhara ya kiafya kwa bianadamu, mimea, wanyama na mazingira kwa ujumla.
“Zimbabwe imeweka ahadi ya
kukiendeleza na kukisimamia kituo hiki ili kiwe cha mfano katika kuitengeneza
kanda ya kijani kwa kutunza mazingira na kuzalisha umeme” alisema Mhe.
Mnangagwa.
Aidha, alieleza kuwa miradi
kama hii ni sehemu ya jitihada za ubunifu unaohitajika ili kuiletea Jumuiya ya
SADC maendeleo na akasisitiza ni vyema kuendelea kuwa wabunifu katika kila
sekta kwa kuwa ni wazi kuwa kila nchi itajengwa na wenye nchi na sio kinyume chake.
====================================
Habari katika picha; Matukio yaliyojiri wakati wa uzinduzi wa eneo la Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika
|
Sehemu ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC walioshiriki katika ziara ya kutembelea eneo la mradi wa Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika na Kituo cha kuchakata taka vilivyopo Harare, Zimbabwe tarehe 8 Agosti, 2024. |
|
Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa akihutubia katika ziara ya ujumbe wa SADC kwenye kituo cha kuchakata taka tarehe 8 Agosti, 2024 Harare, Zimbabwe |
|
Mhe. Mnangagwa akimkabidhi Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Magosi eneo la ujenzi wa Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika ambaye alipokea kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.
|
|
Mhe. Magosi akipanda mti katika eneo la mradi wa Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika. |
|
Mratibu wa Masuala ya SADC kitaifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri akimwagilia mti uliopandwa katika eneo hilo la mradi unaoashirikia "umoja na mshikamano katika kanda" wakati wa hafla ya uzinduzi wa eneo hilo.
Matukio mengine yaliyojiri katika kituo cha kuchakata taka
|