Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo ameiomba Serikali ya India ishirikiane na Tanzania katika jitihada zake za kukuza sekta ya uchumi wa Buluu ambayo ni moja ya sekta ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita inayongoozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema hayo wakati wa Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika masuala ya uchumi, ufundi na sayansi kati ya Tanzania na India uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 26 Juni 2023.
Napendekeza Serikali ya India ianzishe ushirikiano na Tanzania katika kuendeleza sekta ya uchumi wa buluu hususan, uvuvi kwenye bahari kuu, uendelezaji wa viwanda vya kusindika samaki, utafutaji na uokoaji, utengenezaji wa boat na vifaa vya kutengenezea boat”, Balozi Shelukindo alisema.
Balozi Shelukindo aliitaja India kama Mshirika mkubwa na muhimu wa Tanzania katika sekta mbalimbali kama za biashara, uwekezaji, uendelezaji wa miundombinu, ulinzi, elimu na elimu ya ufundi. Alithibitisha hilo kwa kubainisha kuwa India ni nchi ya tatu kwa kufanya biashara na Tanzania, ambapo takwimu zilipo zinaonesha kuwa biashara kati ya nchi hizo mbili kwa mwaka 2021 – 2022 ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 6.
Aidha, Dkt. Shelukindo alisema India ni moja ya nchi 5 zinazoongoza kwa uwekezaji nchini kwa kuwa na miradi yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.68, huku takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania zikionesha nchi hiyo kwa mwaka 2021 – 2022 imeandikisha miradi 630 iliyotoa ajira mpya zaidi ya 60,000.
Katibu Mkuu alitumia kikao hicho kuishukuru India kwa misaada mbalimbali inayoipatia Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta ya maji. Alisema Serikali ya Tanzania inathamini mchango wa India kwa kutoa mikopo ya masharti nafuu ya Dola za Marekani Bilioni moja kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maji nchini ambapo mwezi Juni 2022, kampuni sita zilisaini ujenzi wa miradi ya maji yenye thamani ya Dola milioni 500 kwenye miji 28 itakayofaidisha zaidi ya watu milioni sita, ujenzi wake utakapokamilia.
Wajumbe wa Mkutano huo ambao walikuwa Makatibu Wakuu wa Wizara, Naibu Makatibu Wakuu au wawakilishi wao walipendekeza maeneo mapya ya ushirikiano na India katika sekta za kilimo, TEHAMA, maji, michezo na utamaduni, biashara na uwekezaji ambapo sekta husika zimeelekezwa kuandaa rasimu za Mikataba ya Makubaliano (MoUs) ili ijadiliwe na ikiridhiwa iweze kusainiwa na pande zote mbili.
Kwa upande wake, Kiongozi wa ujumbe wa India katika Mkutano huo ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, Balozi Punnet Roy Kundal aliahidi kuwa Serikali ya India itaendelea kushirikiana na Tanzania na kusisitiza umuhimu wa pande zote mbili kukamilisha MoUs ambazo bado hazijasainiwa ili ziweze kusaininiwa kwa ajili ya utekelezaji.
Alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa wakati Serikali mbili zikisubiri taratibu zikamilike ili zisaini MoU kuhusu kilimo, nchi hiyo imetoa ruhusa kwa Tanzania kuuza nchini India tani 200,000 za mbaazi kwa mwaka.
|
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akitoa hotuba ya ufunguzi kwenye Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika masuala ya uchumi, ufundi na sayansi kati ya Tanzania na India uliofanyika kwa njia ya mtandao |
|
Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika masuala ya uchumi, ufundi na sayansi kati ya Tanzania na India uliofanyika kwa njia ya mtandao ukiendelea |
|
Sehemu ya Ujumbe wa Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 10 wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika masuala ya uchumi, ufundi na sayansi kati ya Tanzania na India uliokuwa ukiendelea kwa njia ya mtandao |