Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Serikali imeahidi itaendelea kuboresha mazingira wezeshi ili wanadiaspora wengi zaidi waweze kuwekeza nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Januari Makamba (Mb) ambaye alimwakilisha Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Nne wa Diaspora
unaofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff mjini Zanzibar.
Mhe. Makamba alibainisha kuwa mwaka jana pekee, Bara la Afrika
lilipokea kiasi cha Dola za Marekani bilioni 33 kutoka kwa Diaspora, kiasi
ambacho ni kikubwa kuliko misaada ambayo bara hilo inapokea kutoka nchi
wahisani.
Alisema hiyo inadhihirisha kuwa endapo nchi zitaweka mazingira mazuri
ya kuvutia wanadiaspora watakuwa na mchango mkubwa wa kuinua uchumi wa nchi
zao.
"Nchi nyingi duniani zinatumia diaspora yao kuendeleza
mipango ya maendeleo na kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi
zinazojitokeza kama vile uhaba fedha za kigeni" Waziri Makamba alisema
Alitolea mfano wa Zimbabwe ambayo mwaka jana ilipokea kiasi cha
Dola milioni 750 kutoka Diaspora ya nchi tatu ambazo ni Afrika Kusini, Marekani
na Uingereza na kufanikiwa kupunguza tatizo la uhaba wa fedha za kigeni.
Akionesha zaidi umuhimu wa diaspora katika uchumi wa nchi, Mhe.
Makamba alisema nchi ya Kenya kwa mwaka jana pekee, iliingiza Dola bilioni 1.7
kupitia diaspora, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko ilichopata kupitia sekta ya
utalii na kilimo cha maua ambazo ndio sekta zinazoingiza fedha nyingi kwa nchi
hiyo.
Alieleza namna baadhi ya nchi zinavyotumia mbinu mbalimbali
kuwawezesha diaspora wao kuwekeza. Baadhi ya mbinu hizo ambazo zinaweza
zikatumiwa hata na nchi yetu ni pamoja na kutoa hati fungani maalum kwa ajili
ya diaspora. Alisema mbinu hiyo inatumiwa na nchi nyingi duniani kama India na
Nigeria kukusanya fedha kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ikiwemo ya
miundombinu.
Mhe. Makamba aliwahimiza wanadiaspora kuwekeza nchini na kwamba
Serikali itatoa ushirikiano unaohitajika kwa yeyote mwenye dhamira ya dhati ya
kuwekeza. Aidha, alieleza kuwa yeyote anayetaka kuwekeza nchini na akakumbana
na vikwazo atoe taarifa mapema kwenye mamlaka husika ili hatua stahiki ziweze
kuchukuliwa.
Baadhi ya watoa mada ambao ni pamoja na Geofrey Simbeye wa TPSPF;
Joseph Simbakalia wa EPZA; Geofrey Mwambe wa TIC na Edwin Rutagerura wa
TANTRADE waliwashauri wanadiaspora kuunda kampuni ya uwekezaji katika maeneo
yao wanayoishi. Kampuni hiyo itakuwa ni fursa kwa kila mwanadiaspora kuchangia
mtaji angalau wa Dola 200 kila mwezi ili fedha hizo zitumike kuwekeza katika
miradi mbalimbali nchini.
Wabobezi hao wa masuala ya uchumi na biashara walishauri pia
wanadiaspora wawekeze katika miradi isiyohitaji mitaji mikubwa kama vile miradi
ya kuzalisha bidhaa zinazotumia ngozi kama viatu, mabegi na mipira.
Mwisho wanadiaspora wanaoshiriki mkutano huo wenye kaulimbiu
isemayo "Mtu kwao ndio Ngao" walielezwa kuwa hali ya kisiasa nchini
ni tulivu, hivyo wasiwe na shaka yeyote wawekeze kwa wingi miradi yao itakuwa
salama.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Zanzibar, 23 Agosti 2017
|