TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania na Misri kushirikiana katika viwanda
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema kuwa Misri
ina historia kubwa katika Nyanja mbalimbali za maendeleo yaliyofikiwa na mwanadamu
katika dunia ya leo.
Kauli hiyo aliitoa
jana Ikulu, Dar Es Salaam akiwa pamoja na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya
Kiarabu ya Misri, Mhe. Abdel Fatah Al Sisi ambaye yupo nchini kwa ziara ya
kitaifa ya siku mbili tarehe 14 na 15 Agosti 2017.
Rais Magufuli alisema
kuwa ukizungumzia maendeleo ya uhandisi huwezi kukosa kuitaja Misri na ushahidi
hadi leo upo namna ujenzi wa piramidi ulivyofanyika. Aidha, katika masuala ya dini,
Rais Magufuli alisema kuwa maandiko yanabainisha kuwa Yesu Kristu alikimbilia nchi
hyo alipotaka kuuwawa na Herode.
“Kwa kuwa hata
Manabii walikimbilia Misri nimeona nami shida zangu nizikimbizie huko na Mhe.
Al Sisi amekubali tushirikiane ili kwa pamoja tutatue changamoto za kiuchumi
zinazotukabili”. Rais Magufuli alisema.
Viongozi hao wawili
wamekubaliana kushirikiana katika masuala mbalimbali ikiwemo ufugaji, kilimo,
afya, elimu, utalii, ulinzi na matumizi ya maji ya mto Nile.
Kwa upande wa
Ufugaji, Misri imekubali kuanzisha kiwanda kikubwa cha kusindika nyama nchini ili
kukidhi mahitaji makubwa ya nyama nchini Misri na pia kutoa ajira, mapato na
soko kwa wafugaji wa hapa nchini.
Aidha, Tanzania itaendelea
kujifunza kutoka Misri katika sekta ya kilimo, hususan utaalamu wa umwagiliaji.
“Nchi ya Misri ina eneo kubwa kidogo kuliko Tanzania lakini asilimia 95 ya eneo
hilo ni jangwa ambalo huwezi kufanya shughuli za kilimo. Licha ya eneo
linalotumika kwa kilimo kuwa dogo, lakini nchi hiyo inazalisha chakula cha kutosha
na ziada ya kuuza nje”. Rais Magufuli alisema.
Kuhusu masuala ya
afya, Misri imeahidi kuanzisha kiwanda cha kutengeneza dawa za binadamu nchini
Tanzania ambapo Rais Magufuli alisema kiwanda hicho kitakapokamilika na kuanza
kazi, kitaokoa fedha nyingi za Serikali zinazotumika kwa ajili kuagiza dawa nje
ya nchi.
Suala la matumizi ya
maji ya mto Nile, Rais Magufuli alieleza kuwa wamekubaliana na mgeni wake kuwa
wataendelea kujadiliana ili kupata utaratibu mzuri wa kutumia maji hayo
utakaokuwa na maslahi kwa nchi zote zinazopitiwa na mto huo.
Viongozi hao pia
wamekubaliana kubadilishana uzoefu katika sekta ya utalii ambapo Misri imepiga
hatua kubwa katika sekta hiyo. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, Misri inapokea
watalii zaidi ya milioni 10 kila mwaka ukilinganisha na idadi ya watalii milioni
2 ambayo Tanzania inapata kwa mwaka. Hivyo, Tanzania ina mambo mengi ya
kujifunza kutoka Misri ili kuongeza idadi ya watalii wa kutembelea Tanzania kwa
mwaka.
Rais Nagufuli
alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa Ziara ya Mhe. Al Sisi imeimarisha
uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili ambao uliasisiwa na Baba wa
Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa zamani wa Misri, Marehemu Gamal Abdel Nasser.
Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana kibiashara kati ya nchi hizo mbili ambapo
kwa takwimu zilizopo kiwango cha biashara kwa mwaka ni Dola milioni 778 na uwekezaji
wa Misri nchini ni Dola milioni 887, viwango ambavyo bado ni vya chini mno.
Kwa upande wake, Rais
wa Misri alipongeza hatua mbalimbali zinazochokuliwa na Rais Magufuli za kuiendeleza
nchi kiuchumi pamoja na kupambana na rushwa na ufisadi. Aidha, aliahidi
kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mtangamano ndani ya Afrika
na kupata msimamo mmoja wa Bara la Afrika katika masuala mbalimbali ya
kimataifa.
Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 15
Agosti 2017
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.