Mama Salma Kikwete akipata picha na baadhi ya Watanzania waishio Zambia ==================================
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amewahimiza Watanzania
wanaoishi nje ya nchi kujenga nyumbani, kuwa waadilifu na kuishi kwa kufuata sheria za nchi walizopo.
Rais Kikwete alitoa
rai hiyo wakati wa mkutano wake na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini
Zambia wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya nchini humo hivi karibuni.
Mhe. Rais Kikwete ambaye
alizungumzia masuala mbalimbali yanayoendelea nchini ikiwemo hali ya siasa,
uchumi, elimu na miundombinu kwa Jumuiya hiyo alisema kuwa, imefika wakati sasa
kwa Watanzania wanaoishi nje kuzisaidia jamii zao zilizobaki nchini hususan
katika suala la elimu ili kuziinua.
“Nawahimiza ndugu zangu jengeni nyumbani,
heshima ya mwanadamu ni kupata mahali pa kukaa pia inapowezekana saidieni ndugu
zenu hususan katika elimu ili nao waimarike”, alisisitiza Rais Kikwete.
Pia Mhe. Rais
aliwaasa kuheshimu sheria za nchi walizopo kwa kuzingatia maadili na kusisitiza
kuwa sheria haibadiliki iwe ni ndani ya nchi au nje hivyo ni wajibu wao kuzifuata sheria zilizowekwa ili waishi kwa
amani na kufanya shughuli zao.
Akizungumzia masuala
ya uchumi nchini alisema kuwa hali ni nzuri
ambapo mfumuko wa bei unaendelea kupungua na pia hali ya chakula ni
nzuri na kwamba Serikali inajaribu kutafuta masoko kwa chakula cha ziada.
“Hadi sasa kuna tani
laki 6 za mchele na mahindi tani milioni 2.6 ambazo ni ziada. Hivyo kazi kubwa
sasa ni kuangalia masoko na pia namna ya kuhifadhi kwa ajili ya matumizi ya
baadaye” alisema Rais Kikwete.
Kuhusu elimu, Mhe.
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali imefanikiwa kuwawezesha watoto wote wanaofaulu
kwenda Sekondari pia wale wanaotakiwa kujiunga na darasa la kwanza wanajiunga.
Alisema Serikali imejenga Sekondari za kutosha ambapo alitoa mfano wa Wilaya ya
Kinondoni ya Jijini Dar es Salaam kuwa mwaka 2006 ilikuwa na Sekondari za
Serikali 5 pekee lakini hadi kufikia mwaka 2014 kuna jumla ya Sekondari 49.
Aidha, wanafunzi waliofaulu na kujiunga na Sekondari hizo Wilayani humo ni
Milioni 1.9 kutoka laki 525 mwaka 2005.
“Tumepiga hatua kubwa
sana katika suala la elimu, tumejenga Sekondari za kutosha na maabara na sasa
tunajitahidi kutafuta vitabu na walimu wa masomo ya sayansi ili kukidhi haja ya
masomo hayo nchini”, alifafanua Rais Kikwete.
Mhe. Rais Kikwete
alitumia fursa hiyo kuipongeza Jumuiya hiyo yenye zaidi ya Watanzania mia tatu
kwa kuanzisha chama na kuwataka wakitumie kama jukwaa la kuwaunganisha na
kuwasiliana.
Awali akijibu swali
kuhusu uraia pacha, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe alisema kuwa Wizara ya
Mambo ya Nje imeendelea na jitihada za kutambua Watanzania wote walioko nje ya
nchi (Diaspora) lakini pia suala hilo lilipelekwa na kujadiliwa na Tume ya
Katiba.
“Kama Wizara
tumejitahidi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha Watanzania wote walioko nje ya nchi
wanatambulika lakini pia tumehakikisha Katiba inayopendekezwa ina kipengele
kinachohusu diaspora. Kipengele hicho kinanaeleza kuwa Mtanzania aliyeko nje ya
nchi (diaspora) anaweza kupata haki kadhaa sawa na raia kwa kupewa hadhi maalum”,
alifafanua Waziri Membe.
Rais Kikwete ambaye alikuwa
nchini humo kwa mwaliko wa Rais wan chi hiyo Mhe. Edgar Chagwa Lungu alifuatana
na Mama Salma Kikwete, Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Saada Mkuya Salum, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt.
Charles Tizeba, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Abbas Kandoro, Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, Mhe. Grace Mujuma, Balozi wa Tanzania nchini Zambia na Viongozi
Waandamizi kutoka Serikalini na Mamlaka mbalimbali.
_Mwisho_
|