Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alipoongea na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola uliofanyika jijini Kigali, nchini Rwanda tarehe 19 hadi 25 Juni 2022
Hotuba kamili ya Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
TAARIFA YA MHESHIMIWA BALOZI LIBERATA MULAMULA
(MB.), WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI KWA VYOMBO VYA
HABARI KUHUSU USHIRIKI WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA 26 WA WAKUU WA SERIKALI WA
JUMUIYA YA MADOLA TAREHE 29 JUNI 2022.
Ndugu wanahabari, Nawasalimu kwa jina la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ............. Kazi iendelee!!
Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi
Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo tukiwa na afya
njema. Pia nitumie fursa hii kuwashukuru kwa namna ya pekee kwa kufika kwenu.
Ni matarajio yangu kuwa kupitia vyombo vya habari mnavyoviwakilisha, watanzania
na dunia kwa ujumla itaweza kufahamu nilichopanga kukiwasilisha kwenu leo.
Ndugu Wanahabari, nimewaita hapa leo kuwapa taarifa kuhusu ushiriki wa Tanzania katika
Mkutano wa 26 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM)
uliofanyika Kigali, Rwanda kuanzia tarehe 19 hadi 25 Juni 2022.
Kama mnavyofahamu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ni mwanachama hai wa Jumuiya ya Madola toka nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961
na imeendelea kuwa mwanachama baada ya Muungano mwaka 1964. Kufuatia uanachama
huo, Tanzania imekuwa ikinufaika na kushiriki shughuli zote za Jumuiya hiyo.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliofanyika
Kigali uliongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Philip Isdor Mpango ambaye alimwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mkutano huu wa 26 umefanyika baada ya kuahirishwa
mara mbili (2020 na 2021) kutokana na janga la UVIKO-19 ambalo linaendelea
kuitesa dunia hadi sasa. Mojawapo ya mijadala ya mkutano huu ilikuwa ni namna
gani dunia itakavyoweza kujikwamua kiuchumi na kijamii kutokana na janga hili.
Ndugu Wanahabari, Mkutano huu wa 26 ulihudhuriwa na Wakuu wa Serikali 27 kati ya nchi
54, ambapo wakuu wengine wa Serikali wapatao 27 waliwakilishwa. Mkutano
ulifanyika chini ya kaulimbiu, “Delivering a Common Future: Connecting,
Innovating and Transforming” ambayo ilijikita kwenye maeneo makuu ya
kipaumbele ya utawala bora, utawala wa sheria na haki za binadamu; vijana;
afya; teknolojia na uvumbuzi; na uendelevu kwenye masuala ya uchumi, biashara,
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na utunzaji wa mazingira.
Ukichunguza vizuri maeneo hayo ya vipaumbele
yanalingana kabisa na vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita, kitu ambacho
kilitusukuma kushiriki kwa nguvu kubwa katika mkutano huu.
Ndugu Wanahabari, Mkutano wa CHOGM ulikuwa na matukio mengi ambayo kutokana na muda,
haitakuwa rahisi kuyaeleza hapa yote, hivyo, naomba mnipe ruhusa, ni yataje
machache. CHOGM 2022 ilitanguliwa na mikutano kadhaa iliyohusisha Majukwaa ya
Jumuiya ya Madola; mikutano ya Mawaziri wa Mambo ya Nje, mikutano ya pembezoni
(side events) na mikutano ya uwili (bilaterals meetings).
Jukwaa la Biashara
Ujumbe wa Tanzania kwenye Jukwaa la biashara
ambalo pamoja na mambo mengine lilijadili fursa za biashara na uwekezaji kwenye
Jumuiya ya Madola na Bara la Afrika na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta
hizo zikiwemo athari zitokanazo na janga la Uviko-19 na mgogoro kati ya mataifa
ya Ukraine na Urusi, uliongozwa na Dkt. Hashil Twalib Abdallah, Naibu Katibu
Mkuu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.
Wajumbe
wengine walitoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji
Zanzibar (ZIPA), Benki za CRDB na KCB na Chama cha Wakulima wa Maua, Mbogamboga
na Matunda (TAHA) na (CTI). Ujumbe wa Tanzania pamoja na kutangaza fursa za
uwekezaji kwenye Jukwaa hili, uliwasilisha kwa wawekezaji orodha ya miradi 115
iliyopo katika sekta mbalimbali nchini kwa ajili ya kutafuta wabia kwenye
miradi hiyo kwa utaratibu wa Public Private Partnerships (PPP).
Jukwaa la Wanawake
Ujumbe wa Tanzania kwenye Jukwaa la Wanawake
(Commonwealth Women’s Forum) uliongozwa na Bibi Abeida Rashid Abdallah, Naibu
Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Pamoja na ushiriki wa Serikali Asasi mbalimbali
za Kiraia kutoka Tanzania nazo zilishiriki. Jukwaa hili lilijadili usawa wa
kijinsia na kuwainua wanawake kwenye nyanja zote; kuongeza nafasi za uongozi
kwa wanawake; kutoa elimu bora kwa watoto wa kike na namna mabadiliko ya
tabianchi yanavyoathiri haki za wanawake.
Jukwaa la Vijana
Vijana saba
kutoka Tazania walishiriki Jukwaa la Vijana lililojadili masuala ya ajira kwa
vijana, kuendeleza ujuzi na vipaji kwa vijana; elimu kwa vijana; kusaidia vijana
wajasiriamali; matumizi ya teknolojia kwa vijana; kujiajiri; na kuongeza
udhamini kwenye shughuli za vijana.
MIKUTANO YA MAWAZIRI
Ndugu
Wanahabari, katika Mikutano hii, Mawaziri
wa Mambo ya Nje, walikutana kwenye mikutano miwili: mmoja ulijadili Mkutano wa
Wakuu wa Serikali na mwingine ulizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu nchi
ndogo (small states).
Kwa upande
wa Mkutano wa Mawaziri kuhusu nchi ndogo uliofanyika chini ya Uenyekiti wenza
wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda na St. Vincent and Grenadines ulijadili
changamoto za nchi ndogo hususan kufuatia janga la UVIKO-19, athari
zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na mgogoro unaoendelea kati ya Urusi na
Ukraine pamoja na upatikanaji mdogo wa fedha za maendeleo.
Baada ya
mkutano huo, iliazimiwa kutumia mkakati ujulikanao kama United
Nations-Commonwealth Advocacy Strategy, kujenga ubia wa kukabiliana na
changamoto zinazokabili nchi ndogo.
Mkutano
mwingine wa Mawaziri wa Mambo ya Nje ulikikita kwenye kuandaa Mkutano wa Wakuu
wa Serikali (Pre-CHOGM Commonwealth Foreign Ministers’ Meeting) kwa kujadili
nyaraka mbalimbali za mkutano zilizopokelewa kutoka kwenye mikutano ya Maafisa
Waandamizi na mkutano wa watendaji wakuu wa Serikali ambao ulihusisha Makatibu
Wakuu-viongozi (Chief Secretaries).
Nyaraka hizo
ni: matamko kuhusu usimamizi bora wa matumizi ya ardhi (Commonwealth Living
Lands Charter – A Call to Action on Living Lands (CALL)), ukuaji endelevu wa
miji (Declaration on Sustainable Urbanization) na huduma na ulinzi kwa watoto
(Kigali Declaration on Childcare and Protection Reform). Vikao hivyo vilijadili
pia Tamko la Mwisho la Mkutano(Communiqué).
MKUTANO WA WAKUU WA SERIKALI WA JUMUIYA YA MADOLA
Ndugu Wanahabari, Ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola
ulifanyika tarehe 24 Juni, 2022. Sherehe hizo zilihudhuriwa na Mwana wa Mfalme
wa Uingereza, Charles, The Prince of Wales, aliyemwakilisha Malkia Elizabeth II
wa Uingereza ambaye ndiye Mkuu wa Jumuiya hiyo; Mhe. Rais Paul Kagame,
Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Madola kwa kipindi cha mwaka 2022-2024; Mhe.
Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madola tangu mwaka 2018; Wakuu wa Serikali wa nchi wanachama wa Jumuiya ya
Madola walioshiriki CHOGM 2022; na baadhi ya wajumbe wa nchi wanachama
walioshiriki Mkutano huo.
Baada ya ufunguzi wa Mkutano huo, ulifanyika
uchaguzi wa Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola. Wagombea waliojitokeza
walikuwa ni Bi. Kamina Johnson Smith, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamaica na
mgombea kutoka Tuvalu, Sir Iakoba Italeri, ambaye aliingia dakika za mwisho.
Baada ya raundi mbili za kura, Bi. Patricia
Scotland alishinda kwa kupata kura 27 wakati Bi. Smith alipata kura 24 na Bw.
Italeri alipata kura 3. Kwa matokeo hayo Bi. Scotland anaendelea kuwa Katibu
Mkuu wa Jumuiya kwa kipindi cha miaka miwili iliyobaki ya kukamilisha kipindi
cha pili cha uongozi wake hadi mwaka 2024.
Ndugu Wanahabari, baada ya uchaguzi, Wakuu wa Serikali au wawakilishi wao walifanya
vikao vya utendaji chini ya uenyekiti wa Mhe. Rais Kagame. Niliiwakilisha Jamhuri
ya Muungano ya Tanzania baada ya Mhe. Makamu wa Rais kurejea nyumbani kuendelea
na majukumu mengine. Vikao hivyo
vilijadili mada zifuatazo:
Mjadala kuhusu Mada ya Utawala Bora na Utawala wa
Sheria
Ndugu Wanahabari, chini ya mada hii, mkutano ulijadili umuhimu wa nchi wanachama wa
Jumuiya ya Madola kuimarisha demokrasia, utawala bora, na kuheshimu mipaka kati
ya mihimili mitatu ya dola ili kufikia mustakabali wenye usawa kwa wote. Ajenda
hii ni muhimu kwa nchi za Jumuiya ya Madola ikiwemo Tanzania kwa kuwa
zinakabiliwa na changamoto katika maeneo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii
zinazohitaji misingi mizuri ya demokrasia, amani na utawala bora kupata utatuzi
wake.
Katika
mjadala huu, Tanzania ilieleza umuhimu inaotoa kwa kanuni za utawala bora na
utawala wa sheria tangu kupata uhuru. Vilevile, Tanzania ilisisitiza umuhimu wa
Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola kusaidia nchi wanachama kutekeleza programu
za kukuza uelewa miongoni mwa watendaji wa taasisi za umma na binafsi ili
kutambua majukumu waliyonayo katika kuhudumia wananchi, hivyo kuepuka rushwa na
vitendo ambavyo vinakinzana na kanuni za utawala bora na utawala wa sheria.
Mjadala wa Maendeleo Jumuishi na Endelevu
Ndugu Wanahabari, mjadala chini ya eneo hili ulihusu kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi
yanahusisha vipengele muhimu kuhusu utunzaji wa mazingira na ujumuishwaji wa
makundi mbalimbali ya jamii nzima. Chimbuko la mada hii ni namna ambavyo
mabadiliko ya tabianchi yanavyoweza kuathiri mafanikio ya nchi yaliyopatikana
kupitia uwekezaji; pamoja na umuhimu wa makundi yote ya jamii kujumuishwa
kwenye mipango ya maendeleo ya nchi.
Tanzania ilisisitiza umuhimu wa vijana, wanawake
na walemavu kujumuishwa kwenye sera za kitaifa na kimataifa kwenye kutunza
mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza biashara na
uwekezaji. Vile vile ilieleza ulazima wa
nchi maskini zaidi duniani kushirikishwa kikamilifu na kwa usawa kwenye mfumo
wa kibiashara wa kimataifa; na umuhimu wa nchi zinazoendelea kujengewa uwezo,
kupatiwa teknolojia na fedha ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
MIKUTANO YA PEMBEZONI
Ndugu Wanahabari, Wakati wa Mkutano wa CHOGM, kulifanyika mikutano mingine mingi ya
pembezoni ambayo ilijadili nada mbalimbali. Mikutano miwli kati ya hiyo
ilijadili Malaria na Magonjwa yasiyopewa kipaumbele. Malengo ya Mkutano huu yalikuwa
ni kupokea mikakati ya viongozi katika kukabiliana na malaria na magonjwa
yasiyopewa kipaumbele. Mhe. Makamu wa Rais alieleza changamoto kwa nchi
zinazoendelea ikiwemo Tanzania kukabiliana na magonjwa haya wakati ambapo
mapambano dhidi ya UVIKO-19 yanaendelea. Aidha, alieleza uzoefu, mafanikio na
mikakati ya Tanzania kukabiliana na magonjwa hayo.
Mkutano wa Kuzuia na Kupambana na Viashiria vya
Ugaidi
Dkt. Moses
Kusiluka, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu aliongoza ujumbe wa Tanzania
ulioshiriki kwenye mkutano wa pembezoni kuhusu kuzuia na kupambana na viashiria
vya ugaidi. Mkutano huu ulijadili athari kwa vijana na wanawake kutoka nchi za
jumuiya, ambayo ni makundi yanayoathirika kwa kiasi kikubwa na madhara
yanayotokana na masuala ya ugaidi. Mkutano huo ulianisha mikakati kadhaa ya
kupambana na changamoto hiyo ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidigitali na
kupambana na uenezaji wa propaganda za itikadi kali na ugaidi, hususani kwa
vijana.
Tanzania
ilishiriki mkutano huu kwa kuzingatia kuwa Sekretatarieti ya Jumuiya ya Madola
imekuwa ikishirikiana na Jeshi la Polisi, Magereza na Kituo cha Kupambana na
Ugaidi nchini kukuza uelewa na kujengea uwezo vyombo hivyo vya usalama
kukabiliana na viashiria vya ugaidi nchini Tanzania na eneo la Afrika Mashariki
kwa ujumla.
MIKUTANO YA UWILI
Ndugu Wanahabari, Mheshimiwa Makamu wa Rais na mimi mwenyewe tulifanya mikutano ya
uwili na viongozi mbalimbali waliohudhuria mikutano hiyo. Lengo letu lilikuwa
ni kuitangaza nchi pamoja na kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo
za utoaji wa huduma kwa jamii.
Mhe. Makamu
wa Rais alifanya mazungumzo na Bi. Melinda Gates, mwanzilishi mwenza wa taasisi
ya Melinda and Bill Gates. Wakati wa mazungumzo hayo, Mhe. Makamu wa Rais
aliishukuru taasisi hiyo kwa kuendelea kusaidia Tanzania katika kuboresha sekta
ya afya ikiwemo kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza kupitia tafiti na
kujengewa uwezo.
Vilevile,
Mhe. Makamu wa Rais alieleza ukubwa wa changamoto ya malaria nchini Tanzania
ambapo alifafanua kuwa zaidi ya asilimia 94 ya wananchi wapo kwenye hatari ya
maambukizi ya ugonjwa huo. Kadhalika, Mhe. Makamu wa Rais alifafanua jitihada
za kukabiliana na malaria ikiwemo Mkakati wa Taifa wa Mwaka 2021-2025 unaolenga
kupunguza maambukizi ya malaria hadi kufikia chini ya asilimia 3.5 ifikapo mwaka
2025 na kutokomeza kabisa ugonjwa huu ifikapo mwaka 2030. Aidha, alieleza upungufu
wa bajeti uliopo wa kiasi cha dola za Marekani milioni 540 ili kutekeleza
mpango huo kikamilifu.
Ndugu
Wanahabari, mimi mwenyewe pia
nilikuwa na mkakati maalum wa kutumia fursa ya mkasinyiko huo wa viongozi
kufanya nao mazungumzo. Nilifanikiwa kufanya mazungumzo rasmi na Waziri wa
Mambo ya Nje wa Singapore, Mhe. Dkt. Vivian Balakrishnan; Waziri wa Mambo ya
Nje wa India, Mhe. Subrahmanyam
Jaishankar; Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Mhe. Hina Rabbani Khar, Naibu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Amina Mohammed na Mke wa Waziri Mkuu wa
zamani wa Uingereza na Mwanzilishi wa Mfuko wa Cherie Blair, Bibi Cherie Blair.
Viongozi
Wakuu niliokutana nao sio kwa mazungumzo rasmi, lakini nilifanikiwa kuwapa
salamu za Rais Samia ni pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza, Mhe. Boris Johnson,
Waziri, Mkuu wa Canada, Mhe. Justin Trudeau; Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame;
Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichilema; Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta; na
Rais wa Nigeria, Mhe. Muhammadu Buhari.
Ujumbe wangu
katika mazungumzo hayo ni kuhusu maboresho yanayofanywa na Serikali ya awamu ya
sita katika mazingira ya biashara na uwekezaji na kwamba Tanzania ni eneo
salama kwa wawekezaji. Maeneo niliyosisitiza ni kilimo, utalii, afya na usafiri
wa anga na Uchumi wa buluu hasa katika usimamizi na uendeshaji wa bandari na
mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Ndugu
Wanahabari, baada ya kusema hayo,
ninawashukuru sana kwa mwitikio wenu, na ni matarajio yangu kuwa mtatumia
vyombo vyenu vya habari kueneza tarifa hii ili iwafikie wananchi.
Ndugu
Wanahabari, nimalizie kwa
kuwasalimu tena kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania……Kazi iendelee!!! |