Wednesday, March 27, 2024

WAZIRI MAKAMBA-AFRICA50 WAJADALI NAMNA YA KUSHIRIKIANA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akisalimiana na na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Africa50, Bw. Alain Ebobisse alipowasili katika ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (MP) amefanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Africa50, Bw. Alain Ebobisse, katika ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma. 

Mazungumzo hayo yalijikita kujadili namna bora ya kushirikiana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo ujenzi wa miundombinu na miradi ya mazingira. Baadhi ya miradi iliyojadiliwa ni pamoja na mradi wa kusambaza umeme, ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani na usambazaji wa gesi jijini Dar es Salaam.

Bwana Ebobisse ameeleza kuwa Africa50 inaiona Tanzania kuwa sehemu sahihi ya uwekezaji kutokana na mazingira mazuri yaliyowezeshwa kwa sera na sheria rafiki, hivyo imehamasika kuwekeza nchini katika miradi ya maendeleo ili kuunga mkono jitihada za serikali za kuwaletea wananchi wake maendeleo. 

Waziri Makamba kwa upande wake ameeleza kuwa Serikali chini ya Uongozi imara wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatilia mkazo wa ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. Ameongeza kuwa imani hiyo kwa sekta binafsi imeongeza mwitikio wa makampuni binafsi kutoka ndani na nje ya nchi kushirikiana na serikali katika kuendeleza na kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Africa50 ni taasisi ya kifedha yenye Makao Makuu yake Casablanca, Morocco ambayo imejikita katika nyanja mbili za uwekezaji ambazo ni; Maendeleo ya Miradi na Fedha za Mradi (Project Development and Project Finance) ikiwa na lengo la kuchagiza maendeleo ya miundombinu barani Afrika kwa kuzingatia umuhimu wa mchango wa mradi husika kitaifa na kikanda.

Tanzania ilijiunga na Afrika50 tarehe 14 Februari, 2023, kwa kusaini Mkataba wa Hisa za Usajili. 

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Mhe. Tim Watts MP. 

Mazungumzo hayo yameangazia masuala mbalimbali kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Australia na Kimataifa hususan yanayolenga kutatua changamoto za amani na usalama miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya ya madola.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Africa50, Bw. Alain Ebobisse yaliyofanyika katika ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Africa50, Bw. Alain Ebobisse akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba yaliyofanyika Mtumba jijini Dodoma
Mazungumzo yakiendeleo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akiwa katika mazungumzo kwa njia ya simu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Mhe. Tim Watts MP.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akiwa katika mazungumzo kwa njia ya simu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Mhe. Tim Watts MP.

Mazungumzo yakiendelea

Saturday, March 23, 2024

WAHIMIZA UMOJA KUMALIZA CHANGAMOTO ZA KIUSALAMA MASHARIKI MWA DRC


Nchi wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) zimekumbushwa kuwa ni jukumu lao kufanya kazi kwa pamoja ili kumaliza changamoto za kiusalama zinazozikabili Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji na Mashariki mwa Jamhuri ya Kidiplomasia ya Congo (DRC).

 

Ukumbusho huo umetolewa na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Rais wa Zambia, Mhe. Hakainde Hichelema wakati anafungua Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya SADC uliohitimishwa jijini Lusaka, Zambia Machi 23, 2024.

 

Katika Mkutano huo ambapo Tanzania iliwakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.  Philip Isdor Mpango pamoja na mambo mengine, ulilenga kutathimini hali ya usalama katika Kanda ya SADC. Ilielezwa kuwa hali ya usalama Mashariki mwa DRC bado hairidhishi, hivyo umetolewa wito kwa nchi wanachama na washirika wa maendeleo kuchangia rasilimali ili vikosi vya kulinda amani vilivyopo huko na vingine vitakavyopelekwa, viweze kutimiza majukumu yake ipasavyo.

 

Ilibainishwa kuwa suala la kutafuta amani katika Kanda ni suala la kimkataba wa jumuiya hiyo na Itifaki ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama, hivyo ni wajibu kwa mataifa hayo kuungana pamoja kukabiliana na changamoto za kiusalama.

 

Wachambuzi wa mambo wamesema kuwa mahudhurio mazuri ya viongozi katika ngazi ya Rais, Makamu wa Rais na Mawaziri Wakuu katika mkutano huo yanadhihirisha kuwa nchi za SADC zimedhamiria kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto ya usalama nchini Msumbiji na DRC.

 

Marais walioshiriki Mkutano huo ni Mhe. Hakainde Hichelema wa Zambia, Mhe. Emmerson Mnangwa wa Zimbabwe: Mhe. Félix Tshisekedi was DRC; Mhe. Lazarus Chakwera wa Malawi; Mhe. Filipe Nyusi wa Msumbiji na Mhe. João Lourenço wa Angola. Nchi za Tanzania na Namibia ziliwakilishwa na Makamu wa Rais, Lesotho, Waziri Mkuu na Afrika Kusini na Botswana ziliwakilishwa na Mawaziri wa Ulinzi

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.  Philip Isdor Mpango akisoma makabrasha ya Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Lusaka, Zambaia Machi 23, 2024. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Mhe. January Makamba (Mb)

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.  Philip Isdor Mpango, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (kulia) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashaiki, Mhe. January Makamba wakiimba nyimbo za Taifa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Lusaka, Zambaia Machi 23, 2024.


TANZANIA –KENYA ZAKUBALIANA KUONDOA VIKWAZO VYA KIBIASHARA

Tanzania na Kenya zimekubaliana na kutia saini makubaliano ya kuondoa vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiushuru ili kuruhusu raia kutoka nchi hizo kufanya biashara baina yao kwa urahisi na kwa manufaa ya pande zote mbili. 

Makubaliano hayo yamefikiwa na kutiwa saini na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Kenya Mhe. Rebbecca Miano wakati wa Mkutano wa nane (8) wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya Tanzania na Kenya katika ngazi ya Mawaziri uliofanyika Kisumu,Kenya tarehe 22/03/2024. 

Mkutano huo ulianza kwa ngazi ya watalaam kisha ngazi ya Makatibu Wakuu ambapo zaidi ya vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiushuru zaidi ya 14 vilijadiliwa na kuwekewa mpango wa kuendelea kuviondoa vyote. Tanzania na Kenya ni wabia wakubwa wa biashara na hivyo kuondolewa kwa vikwazo hivyo vitasaidia kuongezeka mara dufu kiwango cha kifanyika kwa biashara baina ya mataifa hayo.

Viongozi wengine walioshiriki katika Mkutano huo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masala ya EAC Balozi Stephen P. Mbundi, Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda wa Kenya Mhe. Peninah Malonza, Makatibu Wakuu wanaohusika na masuala ya uwekezaji, viwanda, biashara na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. Bernard Yohana Kibese na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Mhe. Isaac Njenga.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Kenya Mhe. Rebbecca Miano wakionesha hati za makubalino ya kuondoa vikwako vya biashara visivyo vya kiforodha kwenye mkutano uliofanyika mjini Kisumu baina ya Tanzania na Kenya tarehe 22/03/2024. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Stephen Byabato na Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda wa Kenya Mhe. Rebbecca Miano wakisaini makubalino ya kuondoa vikwako vya biashara visivyo vya kiforodha kwenye Mkutano wa nane (8) wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya Tanzania na Kenya katika ngazi ya Mawaziri uliofanyika Kisumu,Kenya tarehe 22/03/2024. 
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji Bw. Benjamin Mwesiga akichangia hoja kwenye Mkutano wa nane (8) wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya Tanzania na Kenya uliofanyika Kisumu,Kenya tarehe 22/03/2024. 
Wajumbe wakifuatilia Mkutano wa nane (8) wa Kamati ya Pamoja ya Biashara baina ya Tanzania na Kenya katika ngazi ya Mawaziri wa kuondoa vikwako vya biashara visivyo vya kiforodha uliofanyika Kisumu,Kenya tarehe 22/03/2024.

BILA YA AMANI, HAKUNA MTANGAMANO NA MAENDELEO

 

Nchi Wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimetakiwa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa nchi zao zinakuwa na amani, Umoja na utulivu na kutafuta ufumbuzi wa migogoro kwa kutumia njia zao wenyewe.


Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Mulambo Haimbe wakati anafungua Mkutano huo uliofanyika jijini Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.

 

Tanzania inatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi hiyo baada ya Zambia na katika Mkutano huo, Tanzania inawakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb).

 

Mkutano huo pamoja na mambo mengine unapokea ripoti ya utekelezaji wa vikosi vya kulinda amani katika Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji na mchakato unaoendelea wa kupeleka vikosi vya kulinda amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

 

Nchi Wanachama zimehimizwa kuimarisha zaidi mshikamano na kuchangia rasilimali walizonazo ili kuviangamiza vikundi vya waasi vinavyotishia amani kwenye Kanda ya SADC. Imeelezwa kuwa bila ya amani na Usalama katika Kanda hiyo, wananchi wasitarajie kufikiwa kwa mtangamano na maendeleo ya kweli.

 

Mkutano huo wa Mawaziri ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya SADC utakaofanyika Machi 23, 2024 ambapo Tanzania itawakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb) akisoma makabrasha yake wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024. Kulia kwake ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) na kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo

Mwenyekiti wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Mulambo Haimbe akisoma hotuba wakati ufunguzi wa Mkutano huo uliofanyika jijini Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.

Wajumbe wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe January Makamba (Mb), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kulia) wakiimba nyimbo za taifa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.

Friday, March 22, 2024

NCHI ZA SADC ZAJIPANGA KUMALIZA CHANGAMOTO ZA KIUSALAMA MASHARIKI MWA DRC NA JIMBO LA CABO DELGADO


Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika Lusaka, Zambia Machi 22, 2024.

Mkutano huo ni maandalizi ya Mikutano ya ngazi ya Mawaziri na Wakuu wa Nchi na Serikali itakayofanyika tarehe 22 na 23 Machi 2024 mutawalia.

Wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Zambia, Bi. Etambuyu Anamela Gundersen alisema mwitikio mkubwa wa wajumbe kushiriki mkutano huo ni ishara ya wazi kuwa nchi wanachama zimedhamiria kumaliza changamoto za kiuslama katika kanda ya SADC, hususan Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashsriki, Mhe. January Makamba (Mb) na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) watashiriki Mkutano wa ngazi ya Mawaziri ambao umepangwa kufanyika mchana na utakamilisha agenda zitakazojadiliwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Philip Isdor Mpango atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huo.

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akiwa katika Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika unaofanyika Lusaka, Zambia 

Mwenyekiti wa Mkutano wa Makatibu Wakuu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Zambia, Bi. Etambuyu Anamela Gundersen akisoma hotuba ya ufunguzi ya Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika unaofanyika Lusaka, Zambia 

Wajumbe wa Mkutano wakifuatilia hotuba ya ufunguzi ya Mkutano wa Makatibu Wakuu wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika unaofanyika Lusaka, Zambia 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo na wajumbe wengine wa mkutano wakiomba dua kwa dakika moja kufuatia vifo vya Rais wa Nambia, Hayati 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kulia) akiongea na Maj. Gen. Mbaraka Naziad Mkeremy kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania kabla ya kuanza mkutano 




Thursday, March 21, 2024

NAIBU WAZIRI WA USHIRIKIANO WA MAENDELEO WA SWEDEN AZURU NCHINI


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisalimiana na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse alipomlaki katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma

Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse amewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 21 – 22 Machi, 2023 na kupokelewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa jijini Dodoma.

Lengo la ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi uliopo kati ya Tanzania na Sweden. Pia kupitia ziara hiyo Serikali ya Sweden inatarajiwa kueleza dhamira ya kuongeza muda wa Mpango wa Maendeleo unaotarajiwa kafikia ukomo mwaka huu 2024.

Baada ya kuwasili Mhe. Janse amefanya mazungumzo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.) ambapo katika mazungumzo yao wamejadili juu ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za viwanda, biashara, uwekezaji na ujenzi wa miundombinu hususan uendelezaji wa mradi wa mabasi yaendayo kasi (Bus Rapid Transit Project).

Viongozi wengine aliofanya nao mazungumzo jijini Dododma ni pamoja na, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (Mb.) na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb.)

Vilevile, Mhe. Janse anatarajia kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk tarehe 22 Machi 2022 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Tanzania na Sweden zilianzisha ushirikiano tangu mwaka 1960 ambapo nchi hizo zimekuwa zikishirikiana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za nishati, tafiti, elimu, usimamizi wa mazingira, uchangiaji wa bajeti ya Serikali, biashara, viwanda, uwekezaji na miundombinu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisalimiana na Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mhe. Charlotta Ozaki Macias wakati wa mapokezi ya Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse jijini Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akisalimiana na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse alipomlaki katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma. Kando yao ni Balozi Swahiba Mndeme, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na America
Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa akijadili jambo na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana Janse alipowasili jijini Dodoma
Picha ya Pamoja
Mazungumzo baina ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.) na  Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana yakiendelea jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana  Janse akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb.) yaliyofanyika jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi akielezea jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Sweden, Mhe. Diana  Janse yaliyofanyika jijini Dodoma
Picha ya pamoja

Tuesday, March 19, 2024


 


 

TAARIFA KWA UMMA

 

 

SEMINA MAALUM KUHUSU MPANGO WA BIASHARA WA NCHI YA UINGEREZA NA NCHI ZINAZOENDELEA KUFANYIKA TAREHE

 28 MACHI 2024, DAR ES SALAAM.

 

Dodoma, tarehe 19 Machi, 2024.

 

Semina maalum kuhusu Mpango wa Biashara wa nchi ya Uingereza na Nchi Zinazoendelea (UK Developing Countries Trading Scheme – DCTS) inatarajiwa kufanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa jijini Dar es Salaam, tarehe 28 Machi 2024, kuanzia saa 3:00 asubuhi.

 

Semina hiyo ya siku moja itafunguliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) na kufungwa na Mhe. Omar Said Shabaan, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Zanzibar.

 

Semina hiyo ina lengo la kufahamisha wadau wa biashara  nchini juu ya fursa ya mauzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la Uingereza kupitia Mpango wa Serikali ya Uingereza wa Kufanya Biashara na Nchi Zinazoendelea uliozinduliwa mwezi Mei mwaka 2023. Tanzania ni miongoni mwa nchi 65 ambazo Uingereza imezijumuisha katika mpango huo ili kuweza kuuza bidhaa zake bila kulipa ushuru na imeingia pia katika kundi la nchi ambazo asilimia 99 ya bidhaa zake zitanufaika na msamaha wa kodi.

 

Walengwa wa semina hiyo ni wadau wa biashara wenye nia ya kuuza bidhaa za aina mbalimbali katika soko la Uingereza. Wadau wanaweza pia kushiriki katika Semina hiyo kwa njia ya mtandao, kupitia link maalum ya mtandao wa “Teams” itakayotolewa kwa watakaojisajili kupitiahttps://docs.google.com/forms/d/e/1FAIpQLSdjoGDLwkXfu9PWlV7Oc3LOnn5tRyELsimZVUaMaFhCGFB1Mw/viewform

 

Aidha, wananchi wote wanaweza kuifuatilia Semina hiyo kupitia na chaneli ya YouTube ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza ijulikanayo kama Ubalozi London (http://www.youtube.com/@ubaloziLondon).

 

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali

Sunday, March 17, 2024

TANZANIA NA ITALIA KUIMARISHA USHIRIKIANO SEKTA ZA KIMKAKATI

Serikali ya Tanzania na Italia zimeahidi kuimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati ambazo ni kilimo, nishati, elimu pamoja na uchumi wa buluu kwa maslahi ya pande zote mbili.

Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbaouk (Mb.) alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Balozi Riccardo Guariglia wakati wa Iftari iliyoandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania jana jioni.

Balozi Mbarouk ameipongeza Serikali ya Italia kwa kuipa Serikali ya Tanzania kipaumbele cha kuwa moja kati ya nchi nne za Bara la Afrika zitakazonufaika na mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan). “Tanzania tunaamini kuwa kupitia mpango wa Mattei ushirikiano wa kiuchumi kati yetu na Italia utazidi kuimarika,” alisema Balozi Mbarouk.

Balozi Mbarouk aliongeza kuwa mpango wa mattei utainua sekta za kimkakati ambazo ni kilimo, nishati, elimu na uchumi wa buluu kwa upande wa Zanzibar, Sekta hizi zimepewa kipaumbele kufuatia umuhimu wake  katika kukuza uchumi.

Pamoja na masuala mengine Tanzania imeihakikishia Italia ushirikiano katika kuunda kamati ya kuratibu mpango wa mattei ambayo itahakikisha sekta za kimkakati zilizoainishwa katika mpango huo zinananufaika kama ilivyopangwa kwa maslahi ya pande zote mbili. 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Balozi Riccardo Guariglia alisema kuwa Italia ni rafiki wa Tanzania wa muda mrefu na mataifa hayo yamekuwa yakishirikiana katika sekta mbalimbali. Hivyo mpango wa Mattei ni moja ya njia za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya Italia na Tanzania na Afrika kwa ujumla.

“Tupo hapa kuonesha na kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika na mpango wa mattei, lakini pia kuiona Afrika ikifanikisha kuweka vipaumbele vya malengo na kutekeleza majukumu yake kupitia mpango wa mattei kwa ufanisi,” alisema Balozi Guariglia

Balozi Guariglia aliongeza kuwa lengo la mpango wa mattei ni kuendelea kuimarisha uchumi wa Bara la Afrika kwa kuzishirikisha sekta za umma na binafsi za Italia katika kufadhili mpango huo kwa maslahi ya pande zote mbili.

Mwezi Januari 2024, baada ya kumalizika kwa mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia, serikali ya nchi hiyo iliahidi kutuma ujumbe wa wataalam kutoka Chemba ya Biashara ya Italia kuja Tanzania kwa ajili ya kukutana na timu ya wataalam ya upande wa Tanzania kwa lengo la kukamilisha hatua za awali za utiaji saini wa ushirikiano za kutekeleza mpango wa mattei.

Aidha, katika kutekeleza hilo, mwezi Machi 15, 2024 Ujumbe wa Italia ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia, Mhe. Stefano Gatti ulikutana na timu ya wataalamu wa Tanzania na kuainisha sekta za kipaumbele zitakazo nufaika na mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan).

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbaouk akisalimiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Balozi Riccardo Guariglia wakati wa Iftari iliyoandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania jana jioni Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Italia, Balozi Riccardo Guariglia akiteta jambo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbaouk (kulia) wakati wa Iftari iliyoandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania jana jioni Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi 
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbaouk akisalimiana na viongozi mbalimbali kutoka Serikali ya Italia wakati wa Iftari iliyoandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania jana jioni Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbaouk akistoa hotuba yake wakati wa Iftari iliyoandaliwa na Ubalozi wa Italia nchini Tanzania jana jioni Jijini Dar es Salaam


Friday, March 15, 2024

TANZANIA, ITALIA ZAAINISHA SEKTA ZA KIPAUMBELE MPANGO WA MATTEI

Serikali ya Tanzania na Serikali ya Italia zimekutana na kuainisha sekta za kipaumbele zitakazo nufaika na mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan). 

Sekta zinazotarajiwa kunufaika na Mpango wa Mattei ni kilimo, nishati, elimu afya na uchumi wa buluu. Akizungumza wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo (Mb,) amesema mkutano huo umelenga kujadili utekelezaji wa mpango mpya wa kimkakati wa Mattei kati ya Tanzania na Italia.

Prof. Mkumbo amesema katika mpango huo vipaumbele vikubwa vimetolewa katika sekta za elimu, kilimo, maji na nishati na kuongeza kuwa maeneo waliyobainisha yanaendena na vipaumbele vya Serikali ya Tanzania ambavyo ni elimu, afya, nishati, miundombinu na kilimo.

“Tumekubalina kuanza kutengeneza miradi kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu. Miradi hiyo inatekelezwa katika nchi nne za Afrika ambazo ni Tanzania, Ethiopia, Kenya na Uganda. Tumekubaliana kujikita katika maendeleo ya zao la kahawa,” amesema Prof. Mkumbo

Prof. Mkumbo ameongeza kuwa Tanzania imekuwa ikipambana kuongeza uzalishaji wa mazao hususan kahawa, kuongeza masoko hasa katika bara la Ulaya pamoja na kuongeza thamani katika mazao. “Hivyo kupitia Mpango wa Mattei Tanzania  itasafirisha mazao yenye thamani nje ya nchi na kuliwezesha Taifa kupata fedha za kigeni,” amesema Waziri Mkumbo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia, Mhe. Stefano Gatti amesema Mpango wa Mattei umetoa kipaumbele kwa Tanzania katika sekta ya Kilimo hususan zao la kahawa ambapo nchi hizo mbili zitaendelea kushirikiana kuendeleza zao la Kahawa.

“Sisi kama Serikali tutashirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha zao la Kahawa kutoka Tanzania tunaliongezea thamani pamoja na kuwanufaisha wakulima wa zao hilo licha ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Mhe. Gatti

Mhe. Gatti aliongeza kuwa Mpango wa Mattei utaihusisha sekta ya uchumi wa buluu – Zanzibar pamoja na kutoa elimu katika sekta zitakazo nufaika na Mpango wa Mattei.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Italia katika kukuza na kuimarisha ushirikiano baina ya pande zote mbili.

Mpango wa Mattei umelenga kuimarisha malengo ya maendeleo endelevu yenye lengo la kuboresha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Italia.  

“Kupitia Mpango wa Matei, Italia na bara la Afrika sasa wamekuja na dhana mpya ya ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ambayo yatakuza kiuchumi kwa viwango vya juu zaidi,” alisema Balozi Mussa.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na usshirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.), Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Marco Lombardi, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme na maafisa mbalimbali waandamizi wa serikali kutoka wizara za kisekta.

Mwezi Januari 2024, Tanzania ilichaguliwa kuwa moja ya nchi za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan) ambapo kiasi cha Euro bilioni 5 za awali kilitengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo. Miradi hiyo ya kipaumbele kupitia Mpango mpya wa Kimkakati wa Mattei (Mattei plan) ipo katika sekta ya nishati, elimu na kilimo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na usshirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mwenye Suti ya Kijivu) akizungumza wakati wa Mkutano wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia Jijini Dar es Salaam

Mkutano kati ya ujumbe wa Tanzania na Italia ukiendelea jijini Dar es Salaam. Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo

Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia, Mhe. Stefano Gatti akiongea wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Italia na Tanzania Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo akitioa hotuba ya ufunguzi wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia jijini Dar es Salaam 

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida akichangia jambo wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia Jijini Dar es Salaam 

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa akichangia jambo wakati wa mkutano uliokutanisha ujumbe wa Tanzania na Italia Jijini Dar es Salaam 

Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akiwasilisha mchango wake kuhusu mradi wa Mattei

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof Kitila Mkumbo pamoja na Ujumbe wa Italia ulioongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Maendeleo katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia, Mhe. Stefano Gatti wakiwa katika pichaa ya pamoja Jijini Dar es Salaam