Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Watu wa Algeria zimesisitiza umuhimu wa kukuza diplomasia ya
uchumi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Tume ya Pamoja ya
Kudumu ya Ushirikiano (JPC) kati ya Nchi hizo mbili ngazi ya Maafisa Waandamizi
unaoendelea jijini Algiers, Algeria.
Mkutano huo ni maandalizi ya Mkutano Ngazi ya Mawaziri
utakaofanyika tarehe 1 Agosti 2023 nchini humo ambapo ujumbe wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania unatarajiwa kuongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.).
Ujumbe wa Tanzania katika ngazi ya Maafisa Waandamizi umeongozwa
na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Dkt. Samwel Shelukindo. Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo ni:
Naibu Makatibu Wakuu kutoka sekta za Elimu, Sayansi na Teknolojia; Mambo ya
Ndani ya Nchi, na Nishati.
Aidha, kwa upande wa Serikali ya Algeria, Mkutano huo ulifunguliwa
na Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Selma Malika na kuhudhuriwa
na Viongozi Waandamizi kutoka nchini humo.
Akifungua mkutano huo Balozi Shelukindo ameeleza kuwa ushirikiano
uliopo kati ya Tanzania na Algeria ni wa kihistoria na uliojengwa katika
misingi imara na waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Mwl. Julius Kambarage
Nyerere wa Tanzania na Hayati Ahmed Ben Bella.
Pia amesema Tanzania imejikita katika mageuzi ya kisekta hususan
katika sekta za kilimo, utalii na taasisi za fedha ili kuiwezesha sekta binafsi
kukuza uchumi wa Taifa. Pia inaendelea na ujenzi wa miundombinu ili kurahisisha
mawasiliano kupitia usafiri wa barabara, reli, maji na anga.
‘’Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais,
Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo wa kuimarisha sekta za uzalishaji na
kuweka mpango wa usimamizi katika masuala ya biashara, uwekezaji na uchumi wa viwanda,’’
Alisema Balozi Shelukindo.
Naye Balozi Selma Malika katika hotuba yake ameeleza kuwa mkutano
huu wa tano unaonesha utayari wa pande zote mbili katika kukuza ushirikiano
wenye tija kwa maslahi ya watu wake.
‘’Serikali ya Algeria itaendelea kuhuisha na kuimarisha
ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika masuala ya diplomasia, biashara,
mafunzo ya kujenga uwezo na tafiti, ufadhili katika elimu ya juu na kuongeza
maeneo mapya ya ushirikiano kila inapohitajika ili kujenga uchumi imara wa
mataifa yetu,’’ alisema Balozi Selma Malika.
Aidha, kupitia mkutano huu Balozi Shelukindo amewasilisha salamu
za pole kwa Serikali ya Algeria kufuatia tukio la janga la moto lililotokea
katika mikoa ya Bejaia, Jijel, Bouira, Media, Skikda na Tiziozou
ulilosababishwa na ongezeko la joto kali.
Tanzania na Algeria zinashirikiana katika sekta za Biashara,
viwanda, kilimo, miundombinu, nishati, madini, utalii, sanaa na utamaduni,
elimu, sayansi na teknolojia, ulinzi na usalama, siasa na diplomasia,
mawasiliano, uvuvi, uwekezaji na maendeleo ya jamii.