Friday, August 28, 2015

Balozi Mulamula, awaaga Mabalozi wa Misri na Uturuki.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, akimkabidhi zawadi Balozi wa Uturuki anayemaliza muda wake hapa nchini, Mhe. Ali Dovutoglu, wakati wa hafla ya kumuaga, iliyofanyika leo 28-08-2015,katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, akimkabidhi zawadi Balozi wa Misri anayemaliza muda wake hapa nchini, Mhe. Hossam Eldine Moharam, wakati wa hafla ya kumuaga, iliyofanyika leo 28-08-2015,katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Liberata Mulamula, akizungumza katika hafla hiyo.
Balozi wa Uturuki anayemaliza muda wake hapa nchini, Mhe. Ali Dovutoglu, akitoa neno la shukrani wakati wa hafla hiyo ya kumuaga, iliyofanyika leo 28-08-2015,katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Misri anayemaliza muda wake hapa nchini, Mhe. Hossam Eldine Moharam, akitoa neno la shukrani wakati wa hafla hiyo ya kumuaga, iliyofanyika leo 28-08-2015,katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, Mhe. Juma Alfan Mpango (wa pili kushoto), Balozi wa Kenya hapa nchini Mhe. Chirau Ally Makwere (wa kwanza kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula (kulia) na Balozi wa Uturuki anayemaliza muda wake hapa nchini, Mhe. Ali Dovutoglu wakifuatilia hafla hiyo.
Balozi wa Umoja wa Ulaya hapa Nchini Mhe. Filiberto Sebregond (katikati), Balozi wa Misri anayemaliza muda wake hapa nchini, Mhe. Hossam Eldine Moharam (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Afrika wa Wizara ya Mambo ya Nje, wakimsikiliza Balozi wa Uturuki anayemaliza muda wake hapa nchini, Mhe. Ali Dovutoglu (hayupo pichani)
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bi.Mindi Kasiga, akisherehesha hafla hiyo.
Waheshimiwa Mabalozi wengine wakimsikiliza Balozi wa Uturuki anayemaliza muda wake hapa nchini, Mhe. Ali Dovutoglu (hayupo pichani)
Waheshimiwa Mabalozi mbali mbali wakimsikiliza katibu Mkuu, Balozi Mulamula (mbele katikati,aliyesimama) wakati wa hafla hiyo.
Baadhi ya maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wakimsikiliza Katibu Mkuu.
Baadhi ya Mabalozi na Maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,wakifuatilia hafla hiyo.
Maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje Redemta Tibaigana (kushoto) na Mudric Soraga,wakifuatilia hafla hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bi.Mindi Kasiga (kushoto), Ofisa wa Wizara hiyo, Bi. Felista Rugambwa (katikati), pamoja na Balozi wa Burundi hapa Nchini Mhe. Issa Ntambuka, wakifuatilia hafla hiyo.
JUU NA CHINI:
Balozi Liberata Mulamula, akiwanyanyua washiriki wa hafla hiyo kwaajili ya kugonganisha glasi na kutakiana heri katika hafla hiyo.
====================

PICHA NA REUBEN MCHOME.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberarata Mulamula  amezihakikisha nchi za Uturuki na Misri kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi hizo kwa ajili ya kuletea maendeleo ya wananchi wake. Balozi Mulamula alitoa kauli hiyo katika hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kwa ajili ya kuwaaga Mabalozi wa nchi hizo  Mhe Ali Davutoglu na  Mhe. Hossam Moharam, waliomaliza muda wao wa uwakilishi nchini Tanzania. 

Balozi Mulamula alieleza kuwa Serikali ya Tanzania inafahari kuona matunda ya mahusiano mazuri yaliyopo na kati ya Tanzania na nchi hizo ambayo yanaendelea kukua siku hadi siku kutokana na jitihada za Balozi Davutoglu na Moharam. Baadhi ya maeneo ya ushirikiano yaliyofanikishwa na Mabalozi hao ni uratibu wa ziara za viongozi wa kitaifa baina ya nchi hizo. Aidha, alishukuru misaada mbalimbali ambayo nchi hizo imekuwa ikitoa kwa Tanzania ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuboresha maisha ya Watanzania.

Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki, Mhe. Ali Davutoglu akiongea katika hafla hiyo alieleza kuwa Serikali ya Uturuki ilipofanya maamuzi ya kufungua Ofisi za Ubalozi Kusini mwa Bara la Afrika, Tanzania ilichaguliwa kuwa nchi ya kwanza. Alisema tokea Ubalozi huo ufunguliwe nchini Tanzania umefanikisha mambo mengi ya kimaendeleo ikiwemo kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Istanbul, Uturuki hadi Dar es Salaam na Kilimanjaro. Alisema safari hizo zimeongeza kiwango cha biashara kati ya Uturuki na Tanzania. Mhe. Balozi alisema pia kuwa nchi hiyo ipo katika mikakati ya kufungua kituo kikubwa kwa ajili ya kuwahifadhi watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi (albinos). Kituo hicho pamoja na mambo mengine, kitakuwa na shule, hospitali na chuo cha ufundi.

Kwa upande wake, Balozi wa Misri, Mhe. Hossam Moharam alishukuru ushirikiano aliokuwa anapatiwa na watumishi wote wa Serikali ya Tanzania ambao ulimwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kipindi chake chote cha uwakilishi nchini Tanzania. Aidha alisema msingi wa uhusiano baina ya nchi hizi mbili uliwekwa na waasisi wa mataifa hayo Hayati Mwalimu NJulius Nyerere wa Tanzania na Gamal Abdel Nasser wa Misri, hivyo kazi yake wakati wa uwakilishi wake nchini ilikuwa ni kuyaendeleza mahusiano hayo. Hafla ya kuwaaga mabalazi hao ilifanyika jijini Dar es Salaam tarehe 28 Agosti 2015.

Mkoa wa Kigoma kunufaika na Umeme wa nishati ya jua wa MW 5


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula  akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya NextGen Solawazi Ltd ya kutoka Marekani, Bw. Mayank Bhargava. Katika mazungumzo hayo ambayo yalifanyika katika Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Bhargava alimjulisha Balozi Mulamula kuwa kampuni hiyo imeshaanza kazi ya kufunga mitambo ya kuzalisha umeme wa nishati ya jua wa MW 5 kwa ajili ya mkoa wa Kigoma. Aidha, alitoa taarifa kuwa hivi karibuni kampuni hiyo itaanza mchakato wa kufunga umeme wa nishati ya jua wa MW 16 kwa ajili ya mkoa wa Shinyanga.























































































































Bw. Bhargava akisisitiza jambo huku Balozi Mulamula akisikiliza kwa makini. Wa kwanza kushoto ni Bw. Cyril Batalia ambaye ni Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya NextGen Solawazi Ltd.


mazungumzo yakiendelea.

Umoja wa Ulaya kuleta Waangalizi kwenye Uchaguzi Mkuu Tanzania.

Katibu Mkuu  wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, na Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania, Mhe. Filiberto Sebregondi, wakibadilishana Hati ya Makubaliano ya kuruhusu waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kuingia nchini kufuatilia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Hati hiyo ya makubaliano imesainiwa leo, 28-08-2015, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo.
 Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Filiberto Sebregondi, akisaini Hati ya Makubaliano ya kuruhusu waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kuingia nchini kufuatilia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, naye akisaini Hati hiyo.
Zoezi la kusaini likiendelea.
Katibu Mkuu,Balozi Mulamula akisisitiza jambo, huku Maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje, wakifuatilia kwa makini mazungumzo hayo.
 Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bi. Mindi Kasiga,(kulia) akizungumza katika hafla hiyo ya kusaini hati ya Makubaliano ya kuruhusu waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kuingia nchini kufuatilia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
Bi. Mindi Kasiga akiwatambulisha waandishi wa Habari, waliohudhuria hafla hiyo (hawapo pichani).
 Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Filiberto Sebregondi, akijibu maswali ya Waandishi wa habari. 
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari.
Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe.Filiberto Sebregondi, akiagana na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, muda mfupi mara baada ya kusaini hati hiyo.
=================
NA REUBEN MCHOME.
Umoja wa Ulaya (EU) utatuma timu ya waangalizi yenye wajumbe 128 nchi nzima katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 25 Oktoba 2015. Hayo yalibainishwa wakati wa uwekaji saini wa Makubaliano ya awali ya kuruhusu timu hiyo kati ya EU na Serikali ya Tanzania uliofanyika kwenye Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa tarehe 28 Agosti 2015. Uwekaji saini huo umefanywa na Balozi Liberata Mulamula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na kwa upande wa EU ulifanywa na Mhe. Filiberto Ceriani Sebregondi, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania.


Akizungumza baada ya uwekaji saini wa Makubaliano hayo,  Balozi Sebregondi alieleza kuwa EU imekuwa ikituma timu hiyo kwa nchi washirika ambazo zina historia nzuri ya demokrasia. Aidha, nchi hizo zina dhamira ya dhati ya kukuza mahusiano na EU kwa kuruhusu waangalizi wafanye majukumu yao katika hatua zote za uchaguzi kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa wa haki na huru.


Balozi Sebregondi aliendelea kueleza kuwa timu kama hiyo ambayo wajumbe wake wanakuwa Wabunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya, ilitumwa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ambapo iliutangaza kuwa ni huru na haki.   Timu pia ilitoa ushauri na maelekezo ya namna ya kufanya maboresho katika hatua mbalimbali za uchaguzi.

Kwa upande wake, Balozi Mulamula aliikaribisha timu hiyo kuja Tanzania na alisema kuwa  jukumu la Wizara yake ni kuratibu na kuhakikisha kuwa wajumbe wa timu hiyo wanatekeleza majukumu yao kama ilivyokubalika kwenye Makubaliano ya Kimataifa. Aliongeza kuwa maelezo ya undani wa shughuli ya timu hiyo wakati wa uchaguzi yatatolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ambao pia watasaini makubaliano ya utekelezaji wa kazi ya timu hiyo. 

Taasisi zingine za Kimataifa zinazotarajiwa kutuma timu za uangalizi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 ni pamoja na Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR).

Wizara ya Mambo ya Nje yashiriki kusafisha Soko la Temeke kuadhimisha miaka 70 ya UN

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Sofia Mjema akitoa hotuba yake kwenye maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa nchini yaliyoambatana na usafishaji wa soko la Temeke Sterio lililopo Jijini Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho hayo yaliyoanzia mkoani Kilimanjaro kwa kupanda miti ipatayo elfu mbili (2000). Katika Hotuba yake Mhe. Mjema aliwaasa wafanyabiashara katika soko hilo kutunza mazingira ili kudhibiti na kuzuia magonjwa ya mlipuko kama Kipindupindu. Katika maadhimisho hayo Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Alvaro Rodriguez (kushoto) alikabidhi vifaa vya kufanyia usafi kwa Mhe. Mjema  kwa ajili ya kufanyia usafi katika soko hilo ikiwa ni moja ya kuchochea utunzaji wa mazingira katika maeneo ya biashara 
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy akizungumza kwenye maadhimisho hayo
Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Alvaro Rodriguez naye akizungumza katika maadhimisho hayo
Juu na Chini: Sehemu ya Watumishi wa Serikali na Umoja wa Mataifa wakisikiliza hotuba mbalimbali zilizokuwa zikitolewa katika maadhimisho hayo. 
Sehemu ya wadau walioudhuria usafishaji katika soko hilo wakiwa tayari kwa kuanza zoezi la usafi katika soko hilo.
wananchi waliojitokeza wakifuatilia hotuba mbalimbali zilizokuwa zikiendelea 
Mkuu wa Wilaya ya Temeke akipokea sehemu ya vifaa vya kufanyia usafi kutoka kwa Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Alvaro Rodriguez, akishuhudiwa na Balozi Mushy (kulia) 
Sehemu ya wananchi waliojitokeza kwenye maadhimisho hayo wakishuhudia Mkuu wa Wilaya yao Mhe. Mjema (hayupo pichani) akikabidhiwa vifaa hivyo. 
Mhe. Sofia Mjema, Bw. Alvaro ( kushoto) na Balozi Mushy (wa pili kulia) wakishiriki kusafisha soko la Temeke Sterio.
Watumishi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje wakishiriki katika zoezi la usafishaji wa soko la Temeke Sterio.
Balozi Celestine Mushy (kulia) akizungumza na vijana wanaofanya biashara katika Soko hilo juu ya umuhimu wa kufanya usafi katika mazingira yanayowazunguka.  
Usafi ukiendelea
Balozi Mushy akizungumza na Waandishi wa Habari waliohudhuria katika maadhimisho hayo.


Picha na Reginald Philip

Wednesday, August 26, 2015

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na Balozi wa Japan

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Libarata Mulamula akizungumza na Balozi wa Japan nchini, Mhe. Masaharu Yoshida. Mazungumzo hayo yalijikita katika Mkutano wa Sita (6) wa Tokyo wa kujadili maendeleo ya Afrika, pia kukuza na kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na Japan katika sekta mbalimbali zikiwemo miundombinu kama vile barabara na reli.
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki (kushoto) na Afisa Mambo ya Nje, Bi Bertha Makilagi wakifuatilia mazungumzo kati ya Balozi Mulamula na Balozi Yoshida (hawapo pichani) 
Balozi Yoshida (kushoto) akielezea jambo kwa Balozi Mulamula
Mazungumzo yakiendelea
 Balozi  Mulamula (kulia) akiagana na Balozi wa Japan nchini, Mhe. Masaharu Yoshida mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.

Picha na Reginald Philip

=====================================

JAPAN YAAHIDI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA TANZANIA

Serikali ya Japan imeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha sekta ya miundombinu kama barabara, reli na bandari kwa maendeleo ya haraka nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Balozi wa Japan nchini, Mhe. Masaharu Yoshida wakati akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.

Balozi Yoshida amesema kuwa Serikali yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika kuhakikisha uchumi unakua kwa kasi zaidi kwa kuboresha sekta muhimu ya miundombinu ambapo Serikali hiyo ipo tayari kuendeleza miradi mbalimbali ambayo serikali hiyo inashirikiana na Tanzania ikiwemo barabara, reli na bandari.

Balozi Yoshida alibainisha kuwa miradi ambayo tayari inaendelea hapa nchini chini ya usimamizi wa Serikali yake ukiwemo ule wa kuboresha Reli ya Kati na barabara za juu (fly-over) katika eneo la TAZARA Jijini Dar es Salaam itajadiliwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania, Ubalozi na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) ili kuangalia namna miradi hiyo itakamilishwa.

“Serikali ya Japan kwa sasa inaondoka katika mfumo wa kutoa misaada na kwenda kwenye uwekezaji, hivyo Tanzania ni mdau muhimu sana katika kufanikisha azma hiyo ili kila upande unufaike”, alisema Balozi Yoshida.

Akizungumzia Bandari, Balozi Yoshida alisema kuwa nchi yake ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuboresha Bandari ya Dar es Salaam pamoja na ile ya Kigoma ili kuimarisha biashara na nchi jirani.

Akitoa taarifa kuhusu Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD VI) ambao umepangwa kufanyika mwezi Agosti 2016 nchini Kenya, Balozi huyo alisema mkutano huo pamoja na mambo mengine utazungumzia Maendeleo ya Miundombinu ya Kikanda ikiwemo mradi wa kuimarisha miundombinu ya Nchi za Kanda ya Kati ambao Japan ipo tayari kushirikiana kikamilifu na nchi za Afrika Mashariki kwa maendeleo ya nchi hizo.

Kwa upande wake, Balozi Mulamula alimshukuru Balozi Yoshida kwa niaba ya Serikali ya Japan kwa kuisadia Tanzania kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo kwa kiasi kikubwa imechangia kuboresha maisha ya Watanzania.

“Naipongeza Serikali ya Japan kwa kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi yake ya maendeleo ambayo imelenga mahitaji halisi ya jamii na kuleta maendeleo ya haraka kuanzia ngazi za chini” alisisitiza Balozi Mulamula.

Kuhusu Mkutano wa TICAD VI, Balozi Mulamula aliipongeza Japan kwa kuwezesha mkutano huo kufanyika Afrika kwa mara ya kwanza na kupongeza agenda za mkutano huo ambazo mojawapo itahusu Maendeleo ya Miundombinu ya Kikanda ambapo Tanzania itatumia fursa hiyo kuzungumzia mradi wa kuimarisha Miundombinu ya Nchi za Kanda ya Kati (Central Corridor) kwa vile Serikali imeweka umuhimu mkubwa kwenye miradi ya aina hiyo.


-Mwisho-