Mazungumzo yakiendelea
=================================
TANZANIA NA ALGERIA KUIMARISHA USHIRIKIANO
Katibu Mkuu
wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula
amesema kuwa Tanzania na Algeria zitaendelea kushirikiana katika masuala
mbalimbali ya maendeleo ili kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliopo baina
ya nchi hizi mbili.
Balozi
Mulamula ameyasema hayo alipokutana na Balozi wa Algeria hapa nchini, Mhe. Saad
Belabeb ambaye alimtembelea Wizarani leo kwa lengo la kumpongeza kwa kuteuliwa
kuwa Katibu Mkuu.
Katika
mazungumzo yao, Balozi Mulamula alisema kuwa Tanzania na Algeria zimekuwa na
ushirikiano wa karibu na wa kihistoria tangu kipindi cha waasisi wa mataifa
haya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Rais Ahmed Ben Bella na
kwamba kuuimarisha ushirikiano huo ni kuendelea kuwaenzi.
Aliongeza
kusema kuwa, katika kipindi chote Tanzania na Algeria zimekuwa zikishirikiana
katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya na katika masuala
yanayohusu Bara la Afrika chini ya Umoja wa Afrika.
“Tanzania
itasimama na Algeria pamoja na marafiki zetu wengine ili
kuhakikisha ushirikiano uliopo unaimarika na unaendelea mbele zaidi,”
alisisitiza Balozi Mulamula.
Kwa upande
wake, Balozi Belabeb alimpongeza Balozi Mulamula kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu
wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambapo alimhakikishia
ushirikiano wa hali ya juu kutoka kwake.
Balozi
Belabeb alisema kuwa Tanzania ni rafiki muhimu kwa Algeria na hilo
linathibitishwa na ziara mbalimbali za viongozi wakuu wa nchi hizi ikiwemo
ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete mapema mwaka huu nchini Algeria.
-Mwisho-
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.