Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya Uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ambapo tayari Mswada kuhusu mapendekezo ya Sheria mpya ya Uwekezaji umesomwa bungeni hivi karibuni.
Mhe. Kijaji ametoa kauli hiyo leo tarehe 30 Septemba 2022 wakati akifungua Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha wadau mbalimbali wa biashara na uwekezaji kutoka Tanzania na Italia.
Mhe. Dkt. Kijaji ambaye alimwakilisha Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye ufunguzi wa Jukwaa hilo amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia inaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya biashara na uwekezaji ili kuwawezesha watanzania na wawekezaji kutoka nje kunufaika na fursa lukuki za biashara na uwekezaji zilizopo nchini.
Amesema miongoni mwa maboresho hayo ni mapendekezo ya Sheria Mpya ya Uwekezaji ambayo tayari imesomwa Bungeni hivi karibuni. Sheria hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kuwekeza kwenye miradi mikubwa ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.
Mhe. Dkt. Kijaji alitumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania na wadau mbalimbali wa uwekezaji kutoa maoni yao kuhusu mapendekezo ya sheria hiyo ambayo tayari ipo wazi kwa umma wa watanzania kwa ajili ya kutoa maoni yao.
“Watanzania wenzangu, tunapokutana kwenye jukwaa hili la uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, Serikali yetu ipo kwenye mchakato wa kuandaa Sheria mpya ya Uwekezaji na tayari tumeileta kwa wananchi. Sheria hiyo inakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania, ambapo pamoja na mambo mengine inapendekeza kushushwa kwa kiwango cha mwekezaji mzawa kutoka mtaji wa Dola za Marekani 100,000 hadi 50,000. Hivyo niwaombe watanzania wa kada zote, wawekezaji, sekta binafsi ni wakati wetu sasa wa kutoa maoni yetu kuhusu sheria hiyo” alisema Dkt. Kijaji.
Mhe. Kijaji ametaja maboresho mengine yanayofanywa na Serikali kwenye Sekta ya Biashara na uwekezaji kuwa ni pamoja na kuanzishwa mifumo ya kiteknolojia inayomrahisishia mwekezaji namna ya kuanza biashara, kupata namba ya mlipa kodi, leseni, viza na vibali vya kazi na ukaazi. Kadhalika serikali inakamilisha kuandaa mfumo wa Kielektroniki kwa ajili ya kurahisisha utoaji mizigo bandarini.
Akizungumzia ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, amesema unaendelea vizuri ambapo hadi sasa Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimesajili miradi 111 kutoka Italia yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 274.7 na kuifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa wa uwekezaji kutoka nje hapa nchini.
Pia amezitaka taasisi za Serikali na Binafsi zinazosimamia masuala ya biashara na uwekezaji hapa nchini kukutana na kuandaa taarifa ya pamoja ikijumuisha changamoto na mafanikio yaliyoainishwa wakati wa Jukwaa hili na kuzifanyia kazi changamoto hizo.
Akifunga Jukwaa hilo ambalo limefanyika Zanzibar na Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amewapongeza waandaji wa Jukwaa hilo wakiwemo Mabalozi wa Tanzania na Italia kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa kupitia jukwaa hilo na kuahidi kuendeleza jukwaa hilo ili kufikia malengo kusudiwa katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.
“Nawapongeza waandaji wa Jukwaa hili muhimu wakiwemo Mabalozi wetu na sitalifunga bali nitaliahirisha ili wakati mwingine tuendelee pale tulipoishia” alisema Balozi Mulamula.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo ameendelea kutoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za masoko kama matunda, maua nchini Italia ili kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia katika kukuza uchumi wa nchi.
Naye Balozi wa Italia hapa nchini amesisitiza kuendelea kutoa ushirikiano wowote unaohitajika ili kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kupitia majukwaa mbalimbali ya ushirikiano.
Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limefanyika Zanzibar na Dar es Salaam kuanzia tarehe 27 hadi 30 Septemba 2022. Jukwaa hili limewakutanisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na Italia.
Sehemu ya wageni waalikwa wakiwemo wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Tanzania na Italia wakifuatilia hotuba ya ufunguzi |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akihutubia wakati wa Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia |
Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabit Kombp akizungumza wakati wa Jukwaa la Pili la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia |
Balozi wa Italia nchini, Mhe. Marco Lombardi nae akizungumza wakati wa Jukwaa hilo |
Sehemu nyingine ya washiriki wakiwa kwenye mkutano |
Sehemu nyingine ya Washiriki wakati wa mkutano wa Jukwaa hilo |
Mhe. Dkt. Kijaji akiwa katika picha ya pamoja na washiriki |
Mhe. Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki |