Friday, September 30, 2016

Makamu wa Rais wa Cuba kufanya ziara ya siku tatu nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba Nchini, Mhe.Salvador Antonio Valdes Mesa anayetarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya siku tatu kuanzia tarehe 2 hadi 4 Septemba 2016.

Mhe. Waziri Mahiga akiendelea kuzungumza na Waandishi wa Habari kama wanavyoonekana pichani.

=============================================




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba nchini Tanzania

Makamu wa Rais wa Baraza la Taifa la Jamhuri ya Cuba, Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa anatarajiwa kuwasili nchini tarehe 02 Oktoba, 2016 kwa ziara rasmi ya siku tatu. Lengo la ziara hiyo ni kukuza na kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Cuba pamoja na kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano. Nchi nyingine anazotarajiwa kuzitembelea ni pamoja na Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Botswana na Zimbabwe.

Shughuli mbalimbali zitakazofanyika wakati wa ziara
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mhe. Valdes Mesa atapokelewa na mwenyeji wake Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Tarehe 03 Oktoba, 2016 Mhe. Mesa atakutana kwa mazungumzo ya faragha na Mhe. Samia Suluhu Ikulu yakifuatiwa na mazungumzo rasmi kati yao na wajumbe waliofuatana nao.

Aidha, Mhe. Mesa atakutana kwa mazungumzo mafupi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli.

Baada ya mazungumzo hayo, Mhe. Mesa na Mhe. Suluhu watakuwa na mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari kuzungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mesa atakutana kwa mazungumzo mafupi na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Y. Ndugai katika Hoteli ya Hyatt Regency. Baadaye siku hiyo hiyo, atakutana na Ujumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Hotelini hapo kabla ya kushiriki Chakula rasmi cha Mchana, Ikulu kilichoandaliwa kwa heshima yake na Mwenyeji wake Mhe. Suluhu.

Mhe. Mesa ataondoka Dar es Salaam tarehe 03 Oktoba, 2016 alasiri kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kuendelea na ziara yake Visiwani humo. Akiwa Zanzibar, Mhe. Mesa ambaye atapokelewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi atakutana kwa mazungumzo rasmi na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt.  Ali Mohamed Shein, Ikulu ya Zanzibar.

Tarehe 04 Oktoba, 2016 Mhe. Mesa akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba atarejea Dar es Salaam akitokea Zanzibar kwa ajili ya kuendelea na ziara yake ambapo atatembelea Makumbusho ya Taifa.

Uhusiano wa Tanzania na Cuba
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Cuba ulianzishwa zaidi ya  miaka 50 iliyopita  na Viongozi Waasisi wa mataifa haya mawili, Rais Mstaafu wa Cuba, Mheshimiwa Fidel Castro na Baba wa Taifa, Hayati Julius K. Nyerere. Tangu Tanzania ipate uhuru Cuba imekuwa ikitusaidia katika maeneo mbalimbali ikiwemo afya, utamaduni, elimu, michezo, utalii, nishati, teknolojia na kilimo.

Ushirikiano katika Sekta ya Afya
Tanzania na Cuba zimekuwa zikishirikiana kwenye sekta ya afya ambapo hadi sasa kuna jumla ya Madaktari 30 kutoka Cuba wanaofanya kazi kwenye Hospitali mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar. Kati ya Madaktari hao 10 wapo Bara na 20 wapo Zanzibar wakiwemo wanaofundisha katika Kitivo cha Tiba, Chuo Kikuu cha Zanzibar na kutibu katika Hospitali mbalimbali Zanzibar.

Aidha, katika jitihada za Serikali za kupambana na malaria Serikali ya Cuba na Tanzania zilikubaliana kujenga Kiwanda cha Viuatilifu vya Kuua Viluwiluwi vya Mbu ambacho kimejengwa kwenye eneo la Viwanda Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani na kuzinduliwa mwezi Julai, 2015.

Kiwanda hicho ambacho kilijengwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya LABIOFAM ya Cuba kimekamilika na kwa sasa kinazalisha dawa za majaribio. Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 6 za viuatilifu kwa mwaka ambazo zinatosheleza kwa matumizi ya Tanzania na hata kuuzwa nchi nyingine za Afrika.

Sekta ya Elimu
Katika Sekta ya Elimu Tanzania na Cuba zimekuwa zikishirikiana kwenye programu mbalimbali ikiwemo nafasi za ufadhili wa masomo nchini Cuba kwa wanafunzi kutoka Tanzania. Kuanzia mwaka 2008 hadi 2014 jumla ya Watanzania 64 walipata ufadhili wa mafunzo nchini Cuba katika fani mbalimbali ikiwemo udaktari, uchumi, TEHAMA na Michezo.

Pia Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Cuba ilianzisha Programu ya Elimu kwa Vijana na Watu Wazima ambayo hutolewa kwa kutumia vifaa vya kufundishia vinavyomwezesha mwanafunzi kusikia na kuona (audiovisual). Inatarajiwa kwamba zaidi ya vijana na watu wazima milioni 3 watakuwa wameshiriki programu hii ifikapo mwaka 2017. Mradi wa majaribio ya program hii ulizinduliwa mwaka 2014 katika Manispaa za Ilala, Temeke, Kinondoni, Ilemela, Mwanga, Bagamoyo, Mkuranga na Songea.

Sekta ya Michezo
Katika Sekta ya michezo Serikali ya Cuba wametupatia Wakufunzi wa Ngumi, Judo na Riadha. Hivi sasa wanatoa nafasi za mafunzo nne kila mwaka kwenye mafunzo ya michezo na utaalamu wa mazoezi ya viungo.

Hivyo, pamoja na kutumia fursa ya ziara hiyo kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizi mbili Tanzania itatumia nafasi hiyo kujikita katika kuanzisha ushirikiano kwenye maeneo mapya hususan biashara na uwekezaji.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 30 Septemba 2016.


Waziri Mkuu apokea msaada wa Waathirika wa tetemeko la ardhi Kagera

Waziri Mkuu akipokea hundi ya Shilingi milioni 80 ikiwa ni msaada kutoka Serikali y Pakstan uliokabidhiwa na Kaimu Balozi wa Nchi hiyo Nchini Bw. Amir Khan kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.Hafla iliyofanyika Hotel ya Hyatt Jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako.
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako wakipokea hundi ya shilingi Milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi Mkoani Kagera kutoka Kampuni ya Simu ya Huawei ya nchini China. Wakwanza kushoto ni Mkurugezi wa Kampuni hiyo Nchini Bw. Bruce Zhang
Kaimu Balozi wa Pakstan nchini, Bw. Amir Khan akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi misaada ya wahanga wa tetemeko la ardhi Mkoani Kagera
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akizungumza katika hafla hiyo
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri, Mabalozi na wadau wengine waliohudhuria makabidhiano hayo
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia ,Balozi Mbelwa Kairuki akifuatilia hafla ya makabidhiano ya msaada wa wahanga wa tetemeko la  ardhi Mkoani Kagera iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Jijini Dar es Salaam


Wednesday, September 28, 2016

Mhe. Rais apokea Hati za Utambulisho za Balozi wa Uingereza nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. Sarah Catherine Cooke, Ikulu Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba akisalimiana na Mhe. Balozi Sarah Catherine Cooke mara baada ya kuwasilisha hati za utambulisho.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima akisalimiana na Mhe. Balozi Sarah Catherine Cooke mara baada ya kuwasilisha hati za utambulisho.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Mhe. Balozi Sarah Catherine Cooke. Katika mazungumzo yao Mhe. Balozi amewasilisha ahadi ya  Uingereza ya kuchangia kiasi cha paundi milioni 2.3 kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la Ardhi Mkoani Kagera.
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Balozi Joseph Sokoine akisalimiana na Mhe. Balozi Sarah Catherine Cooke mara baada ya kuwasilisha hati ya utambulisho
Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. Sarah Catherine Cooke  akitoa heshima wakati wimbo wa Taifa lake ukipigwa mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwasilisha hati za utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Itifaki, Bw. James Bwana
Mhe.Rais John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Serikali, Mhe. Balozi Sarah Catherine Cooke na baadhi ya Maofisa kutoka ubalozi wa Uingereza Nchini

Ubalozi wa China nchini waadhimisha miaka 67 ya Taifa lao

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage akizungumza katika hafla ya kuadhimisha miaka 67 ya Taifa la Jamhuri ya Watu wa China. Katika hotuba yake Mhe. Mwijage aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuendeleza mahusiano mazuri baina ya Tanzania na nchi yao pia kuendelea kushirikiana katika kuboresha sekta mbalimbali nchini. Hafla hiyo imefanyika katika Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China Jijini Dar es Salaam.
Naibu Balozi wa Ubalozi wa China hapa nchini naye akizungumza na kuwakaribisha wageni waalikwa wote.
Sehemu ya Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini walioshiriki maadhimisho hayo
Naibu Balozi akiendelea kuzungumza huku wageni waalikwa wakimsikiliza.
Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki (kushoto), akizungumza na kubadilishana mawazo na wageni waalikwa waliohudhuria hafla hiyo
Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Sospeter Mhongo (kulia), akimsikiliza Balozi wa Kenya hapa nchini Mhe. Chirau Ali Mwakwere alipokuwa akizungumza nae walipokutana katika hafla hiyo

Tuesday, September 27, 2016

OMAN YAONESHA NIA YA KUKARABATI “HOUSE OF WONDERS” -ZANZIBAR

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sultanate of Oman, Dkt Augustine Mahiga ( kushoto) na Yusuf bin Alawi bin Abdullah wakizungumzia kuhusu namna ya kuendelea kuimarisha uhusiano mzuri baina ya nchi hizo mbili. Katika mazungumzo hayo Waziri Mahiga ameiomba serikali ya Oman kupitia Waziri Abdullah kuangalia uwezekano wa kushirikiana katika uhifadhi ya nyaraka na kumbukumbu muhimu pamoja na ukarabati ya jengo la House of Wonders lilojengwa na ufalma wa Oman mwaka 1883.

Jengo maarufu la Beit Al Jaib ( House of Wonders) ambalo Serikali ya Tanzania inaiomba Serikali ya Oman kuangalia uwezekano wa kulikarabati kama sehemu ya mradi wa kuhifadhi nyaraka, kumbukumbu na majengoa ya kihistoria visiwani Zanzibar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mshariki, Augustine Mahiga akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayehusika na masuala ya Afrika, Mazungumzo yao yalijielekeza zaidi katika uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.

=================================

Na Mwandishi Maalum, New  York

Ufalme wa Oman umeonesha nia ya  kukarabati  majengo  ya makubusho ya kale   ya  Beit Al Jaib  maarufu kama “ House  of  Wonders” yaliyopo  mjini  Unguja – Zanzibar.

Nia hiyo imeoneshwa na   Waziri wa Mambo ya   Nje wa  Oman,  Bw. Yusuf bin Alawi bin Addullah wakati   alipokutana na kufanya  mazugumzo na  Waziri wa Mambo ya Nje  na  Ushirikiano wa  Afrika Mashariki, Dkt, Augustine Mahiga.

Mazungumzo  baina ya  viongozi  hao wawili  yalifanyika  pembezoni mwa  Mkutano wa 71 wa  Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa, ambapo  Mawaziri hao walikuwa wakiongoza ujumbe wa Nchi  zao.

Mazungumzo   ya   Mawaziri  hao  yalijikita  katika   uimarishwaji wa uhusiano  na ushirikiano mzuri  uliopo  baina ya  Oman na  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika majadilaino hayo ambapo   pamoja  na  mambo mengine,  Waziri  Mahinga  aliomba  serikali ya Oman kuangalia uwezekano  wa kuanzishwa  kwa miradi wa kutunza mambo ya kale zikiwamo nyaraka muhimu zinazohusu uhusiano  baina ya nchi  hizo mbili.

Waziri Mahiga  alieelezea  pia hali uchakavu wa  majengo ya   Beit Al Jaib ( House of wonders)   majengo yaliyokuwa  Ikulu ya  utawala wa Kifalme, Zanzibar.  Makubusho hayo  yamesheheni historia ya  uhusiano  na ushirikiano kati  ya  Zanzibar na   Sultanate of Oman na  Afrika  Mashariki kwa Ujumla.

Na kutokana na historia hiyo na  umuhimu wa  jengo hilo ambalo limejengwa mwaka 1883, Waziri ameiomba  Serikali ya  Oman kuangalia  uwezekano wa kulihifadhi jingo hilo ambalo pia ni kivutio kikubwa cha utalii.

Akijibu  ombi  hilo na  mengine yaliyowasilishwa na   Waziri Mahinga,  Waziria wa Mambo ya Nje wa Oman,  Bw .   Yusuf bin Alawi bin Addullah amemtaka  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa  Afrika   Mashariki kuandaa andiko  na  kuliwasilisha  katika Serikali ya  Oman ili  pendekezo  hilo liweze  kufanyiwa kazi pamoja na mapendekezo mengine.

Katika  hatua nyingine,  Waziri wa Mambo ya Nje  na  Ushirikiano wa   Afrika Mashariki,  Augustine  Mahiga amekuwa na   kuwa  na mazungumgo na   Bi. Linda Thomas Greenfield,   Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayehusika na  masuala ya   Afrika.

Mazungumzo ya  Waziri Mahinga na   Bi.  Linda Greenfield yalijikita zaidi  katika uhusiano na  ushirikiano  baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marekani.