Monday, September 26, 2016

TANZANIA YATAKA USHIRIKIANO KATIKA VITA DHIDI YA RUSHWA NA UKWEPAJI KODI


Tanzania imeeleza kwamba juhudi za serikali ya awamuya Tano za kukabiliana na  vitendo vya rushwa  hazitawezakufanikiwa kama havita ungwa mkono na  jumuiya ya kimataita.

Ni kwa sababu hiyo, Tanzania, inazitaka nchi zilizoendelea kuwawajibisha wawekezaji wao na makampuni yao ili  yalipe kodi.

Hayo yameelezwa jana  jumatatu na  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa  Afrika Mashariki, Dkt. Agustine Mahiga (Mb)  wakati alipolihutubia  Baraza Kuu la 71la Umoja wa Mataifa na kutumia  fursa hiyo kuelezea vipaumbele vya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Mahinga akafafanua kwamba, lengo nambakumi na sita la  maendeleo endelevu linatambua kuwa,  rushwa inakandamiza juhudi za kumbana na  umaskini na   usawa wa jinsia,  inazuia fursa na inakuwa na kama kodi kwa familia maskini pale wanapotafuta  haki.

Ni katika muktadha  huo,   akasema, serikali  ya Tanzania imeamua kuanzisha vita dhidi ya rushwa  kwa kuhuisha uwazi, uwajibikani  na usahihi katika utoaji wa huduma  kwenye taasisi za  umma.

Akasisitiza kwamba serikali  imeweka misingi mizuri ya uwajibikaji inayomtaka mtumishi wa umma kutambua kwamba  wajibu wake wa kwanza ni  kutoa huduma bora na kwa wakati kwa umma.

“Juhudi hizi za serikali za kupambana na rushwa hazitaweza kuzaa matunda bila ya kuungwa mkono wa jumuiya ya kimataifa. Nchi zilizoendelea zinatakiwa  kuwawajibisha wawekezaji wao  pamoja na makampuni yao ili  waweze kulipa kodi stahiki.” Akaeleza zaidi  Waziri  Mahinga

Na  kuongeza. “Ni lazima wawe tayari kurudisha mali na fedha  zilizoibwa kutoka nchi zinazoendelea na kuzificha katika nchi zao ili mali  na fedha hizo ziweze kusaidia maendeleo  yetu”.

Kuhusu fursa za jinsia na uwezeshwaji wa wanawake, Waziri Mahinga ameelezea juhudi mbalimbali ambazo zimefanywa na serikali katika kuwawezesha  wawanake ikiwamo kushika ngazi za juu za maamuzi kuanzia serikali kuu  hadi bunge na uwezeshwaji wa kiuchumi.

katika kudhibitisha kuwa Tanzania  inazingatia usawa wa jinsia katika uteuzi wa ngazi  mbalimbali za maamuzi, Waziri Mahinga  ameeleza kwamba kwa mara ya kwanza  wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Mhe. Dkt. Rais John Pombe Magufuli  alimchangua mwanamke  kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Uteuzi  huu unathibitisha nia ya nchi yangu ya kuona wanawake  wengi zaidi wanakuwa katika   nafasi za ngazi za  juu  za maamuzi. Na ajenda hii ya uwezeshwaji wa wanawake wa Tanzania sasa inamilikiwana wanawake wenyewe” akasisitiza  Waziri

 Kwa upande wa vijana, Kiongozi huyu wa Ujumbe wa Tanzania ambaye amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  amesema. Vijana ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote lile, siyo tu kwamba ni viongozi wa kesho lakini pia ni viongozi wa sasa.

Akatahadharisha kwamba kwa  kutowapa kiupaumbele vijana  ni kujitafutia  matatizo makubwa kutokana na kile alichosema ni rahisi  kurubuniwa na makundi ambayo ni
hatari kwa ustawi wa jamii na taifa .

“ Kutoka na  kwamba idadi ya vijana ni kubwa,  Serikali inachukua hatua mbalimbali za  kuliwezesha kundi hili la jamii ambalo ni muhimu katika utekelezaji wa ajenda 2030. Na ili vijana   waweze kutekeleza  jukumu hilo  Serikali imeanzisha  mfuko wa maendeleo wa  vijana mfuko ambao hadi mwezi March mwaka huu jumla ya  shiling 1.6 bilioni
zilipelekwa  kwa vikundi 284 ya  vijana”.

 Kuhusu elimu, eneo ambalo ni kipaumbele kingine cha Tanzania,   Waziri ameeleza kuwa   upatikanaji wa elimu jumuishi  na ya viwango ndicho kipaumbele cha serikali
kwa  kuwa    Serikali inaamini kuwa, elimu ni  ni nyenzo muhimu   kwa maendeleo endelevu

Akafafanua  kwamba serikali  inatekeleza bila kuchoka kuhakikisha kwamba  watoto wote wa kike na wa kiume wanapata  elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Pamoja na kutoka   Elimu bure, Serikali imeboresha mitaala yake kwa kuzingatia mahitaji ya karne ya 21.

“Alipoingia madarakani,  Mhe.  John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitangaza kwamba kuanzia elimu ya msingi  hadi sekondari itakuwa bure. Serikali  imetenga zaidi ya  shilingi 263 bilioni ili Kuhakikisha elimu  inakuwa bure kwa wote.

Vipaumbele vingine vya  Tanzania ambavyo Mhe. Waziri amevianisha katika  hotuba  yake ni pamoja na  mikakati ambayo  serikali imejiwekea  katika utekelezaji wa mkatabawa mabadiliano ya tabia nchi ( Paris Agreement),  utekelezaji wa   malengo ya maendeleo endelevu ( agenda 2030), mapambano dhidi ya  dawa haramu za kulevya,  na kukabiliana na  ugaidi ambao  amesema  ni tatizo ambalo linaendelea kukua na kuwa tishio  hata kwa  nchi za Afrika Mashariki.




Kwa upande wa utekelezaji wa  agenda 2030, Waziriamesema agenda hiyo imeanishwa  katika mipango ya kitaifa ya  miaka  mitano ya maendeleo  kwa pande zote za muungano.  Hata hivyo  amesema kuwa Tanzania  imebaini kwamba haitaweza kukamilisha kwa  wakati agenda 2030 pasipo kushirikiana na wadau  mbalimbali  wa maendeleo. 

Kuhusu  migogoro inayoendelea katika nchi za Burundi na Sudani ya Kusini, Waziri Mahiga amezitaka pande zote zinazopingana  nchi Burundi kutambua kwamba majadiliano ambayo ni jumuishi kwa pande zote ndiyo  njia sahihi ya kutatua matatizo ya nchi yao.

Kwa upande wa Sudani ya Kusini,  Waziri  amesema Tanzania inaungana na   nchi nyingine kulaani matukio ya hivi karibuni ya kujirudia kwa machafuko nchini humo.

Na kuongeza,  Tanzania ambaye ni  Mwenye -Kiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,  iliitisha Kikao kisicho cha kawaida ili  kuzungumzia hali ya kisiasa ya Burundi na Sudani ya Kusini. “ Tunatumaini kwamba nchi  zote mbili  zitaweka maslahi  ya wananchi wao mbele ili kumaliza machafuko”.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa  Afrika Mashariki pia aligusia kuhusu marekebisho ya mfumo wa   Baraza  Usalama la Umoja wa Mataifa,  ili liwe jumuishi. 


Kwa upande wa   Uchaguzi wa Katibu Mkuu, Waziri amesema,Tanzania  inaunga mkono  hoja ya kuendelea  kuheshimu utaratibu wa kupokezana nafasi ya  Katibu Mkuu kwa kuzingatia mzunguko wa   kijiographia. 


Waziri wa Mambo ya Nje  na  Ushirikiano wa  Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga  anayemwakilisha  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. John Pombe Magufuli katika  Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu  la Umoja wa Mataifa akiwasilisha mbele  ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo  ( hawapo pichani) vipaumbele vya Tanzania.
 Balozi wa Tanzania nchi Marekani  Wilson  Masilingi akimpa  mkono wa pongezi Waziri  Mahiga  baada kumaliza hotuba yake mbele ya   wajumbe wa  mkutano wa  71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mhe.  Anna Lupembe   Mbunge wa Viti Maalum (CCM) naye akimpongeza Mhe, Waziri kwa hotuba yake iliyopokelewa vizuri.


Dk. Tausi Kida Mkurugenzi  Mtendaji wa  ESRF naye  akimpongeza  Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania  katika Mkutano wa  71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Baadhi ya Wajumbe wa  Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakiwa  katika mstari tayari kumpa mkono  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Augustine Mahiga  mara baada ya kumaliza hotuba yake
 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.