Sunday, November 24, 2024

WAZIRI KOMBO: TANZANIA ITAENDELEA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA KULETA AMANI NA USALAMA UKANDA WA MAZIWA MAKUU


Waziri Mambo ya Nje na Uashirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akifuatilia Mkutano wa Kawaida wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje (RIMC) wa Nchi Wanachama wa ICGLR uliofanyika jijini Luanda, Angola tarehe 24 Novemba 2024. 

Waziri Mambo ya Nje na Uashirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameeleza kuwa Tanzania ikiwa ni mwasisi wa Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Mkuu (ICGLR) itaendelea kushirikiana na nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo na Jumuiya ya Kimataifa katika juhudi za kutafuta amani ya kudumu kwenye ukanda huo. 

Waziri Kombo ameeleza hayo alipozungumza katika Mkutano wa Kawaida wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje (RIMC) wa Nchi Wanachama wa ICGLR uliofanyika jijini Luanda, Angola tarehe 24 Novemba 2024. 

Akizungumzia kuhusu msimamamo, mchango na nafasi ya Tanzania katika kufatua amani na usalama kwenye ukanda wa Maziwa Makuu Waziri Kombo ameeleza kuwa, Tanzania chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan itafanya kazi bila kuchoka kwa kushirikiana na nchi wanachama na Jumuiya ya Kimataifa kutatua migogoro iliyopo ili kuwa na ukanda wenye amani, ustawi na ustahimilivu.

“Kama mwanachama mwanzilishi wa ICGLR, Tanzania inaamini kuwa kuimarika kwa mahusiano ya kidiplomasia na kuimarishwa kwa utulivu kutaongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi ya watu wetu katika Ukanda wa Maziwa Makuu” Ameeleza Waziri Kombo. 

Aidha, Waziri Kombo licha ya kueleza utayari wa Tanzania katika kuendelea kushirikiana na wadau katika kurejesha amani na usalama kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu, ametoa wito kwa nchi wanachama kuhakikisha kuwa ushawishi wa washirika wa maendeleo hauathiri utendaji na ufanisi wa mifumo iliyowekwa ikiwemo Mfumo wa Tahadhari ya Mapema na Majibu ya Migogoro wa ICGLR (ICGLR Conflict Early Warning and Response Systems).

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa nchi Wanachama kuheshimu na kutimiza wajibu wake wa kuchangia fedha kwa Sekretarieti, ikiwa ni ishara ya mshikamano na juhudi za pamoja, katika kuhakisha Jumuiya inatekeleza mipango na mikakati inayojiwekea ili kufikia matarajio ya kuwa na ukuanda wenye Usalama, Utulivu, na Maendeleo endelevu. 

Pia ametumia fursa hiyo kuitaka Sekretareti ya ICGLR kuzingatia matumizi mazuri na usimamizi mzuri wa fedha kwa manufaa ya kanda. 

Kwa upande wake mwenyekiti wa mkutano huo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola Mhe. Balozi Téte António akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo ameleeza ameeleza kuridhishwa kwake na mazungumzo yanayo endelea yakilenga kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Rwanda na DRC. 

Aliendelea kutoa wito kwa nchi wanachama kwa umoja wao kuendelea kushughulikia changamoto zinazotishia amani, usalama, na hali ya kibinadamu katika Jamhuri ya Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini, na ghasia zinazoendelea katika Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mkutano huo umehudhuriwa na nchi zote 12 Wanachama wa Maziwa Makuu na Mjumbe Maalumu kutoka Umoja wa Mataifa anayesimamia Ukanda wa Maziwa Mkuu Balozi Huang Xia.
Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Mhe. Musalia Mudavadi Mkuu wa Baraza la Mawaziri wa Kenya (Prime Cabinet Secretary) wafurahia jambo pembezoni mwa mkutano wa Kawaida wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje (RIMC) wa Nchi Wanachama wa ICGLR uliofanyika jijini Luanda, Angola tarehe 24 Novemba 2024.
Balozi wa Tanzania nchini Angola mwenye makazi yake nchini Zambia Mhe. Lt. Gen. Mathew Edward Mkingule akifuatilia Mkutano wa Kawaida wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje (RIMC) wa Nchi Wanachama wa ICGLR uliokuwa ukiendelea jijini Luanda, Angola tarehe 24 Novemba 2024.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola Mhe. Balozi Téte António kwenye ufunguzi wa mkutano wa Kawaida wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje (RIMC) wa Nchi Wanachama wa ICGLR uliofanyika jijini Luanda, Angola tarehe 24 Novemba 2024.
Picha ya pamoja
Mkutano ukiendelea 






MHE. MAKINDA AKUTANA NA DKT. SPECIOZA WANDIRE-KAZIBWE MKUU WA MISHENI YA UANGALIZI WA UCHAGUZI YA UMOJA WA AFRIKA

Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Namibia kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM), Mhe. Anne Makinda, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Umoja wa Afrika (AUEOM) na Makamu wa Rais wa Zamani wa Uganda Dkt. Specioza Wandire-Kazibwe, tarehe 24 Novemba 2024, jijini Windhoek Namibia.

Katika kikao hicho Mhe, Makinda aliambatana na mjumbe wa Organ Troika na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa pamoja na na mwakilishi wa Secretarieti ya SADC.

Akizungumza na Dkt. Wandire-Kazibwe kuhusu maendeleo ya ufuatiliaji wa Uchaguzi Mkuu wa Namibia, Mhe. Makinda amesema SEOM imekutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi na kuzungumzia pamoja na mambo mengine, hali ya ulinzi na usalama, siasa na maendeleo ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao katika ujumla wake.

Naye Mkuu wa AUEOM Dkt. Wandire-Kazibwe, amezitaka taasisi za akademia na za utafiti katika nchi wanachama wa SADC zikiwemo Vyuo, kupanua maeneo ya kufanyia utafiti katika siku sijazo na kujumuisha maeneo ya siasa, uchumi, demokrasia na masuala yahahusu uchaguzi; ili matokeo ya tafiti hizo yatumike kuimarisha mipango ya kisiasa, kiuchumi na kijamii pamoja na kuwezesha kufanyika kwa maboresho sera, ilani za vyama vya siasa, sheria, na miongozo mbalimbali inayohusu ukuaji uchumi wa mataifa.

Katika tukio lingine , Mhe. Makinda pia alikutana na Kiongozi taasisi inayosimamia uendeshaji wa Waandishi wa Habari nchini Namibia (Media Ambudsman of Namibia) ambaye ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Namibia Dkt. John Nakuta.

Akizungumza kuhusu wajibu wa vyombo vya habari, Dkt. Nkuta amesema wakati Namibia inajiandaa kwa uchaguzi mkuu, vyombo vya habari vya Serikali na binafsi vinapaswa kuzingatia haki, usawa, na sheria za nchi katika kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kusema ukweli wakati wote. 

Na kuongeza kuwa wakifanya hivyo watasaidia kuwapa wagombea na wananchi haki yao ya msingi ya kupata habari.

Wananchi wapatao 1,449,569 wanaripotiwa kujiandikisha kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao wa nchi hiyo, yenye wakazi zaidi ya milioni tatu.


 

Friday, November 22, 2024

VIKAO KUANDAA MKUTANO WA 46 WA BARAZA LA MAWAZIRI LA EAC VYAANZA JIJINI ARUSHA

Mkutano wa 46 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Ngazi ya Wataalam umeanza jijini Arusha ikiwa ni maandalizi ya Mkutano huo utakaofanyika tarehe 28 Novemba 2024.

 

Pamoja na mambo mengine, mkutano wa wataalam unajadili agenda mbalimbali muhimu kuhusu masuala ya mtangamano wa Jumuiya hiyo ambazo baadaye zitawasilishwa kwenye Mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu kwa majadiliano na hatimaye agenda hizo zitawasilishwa kwenye Mkutano ngazi ya  Mawaziri.

 

Taarifa zilizopokelewa na kujadiliwa ni pamoja na Taarifa ya utekelezaji wa maamuzi ya awali ya Baraza la Mawaziri; Taarifa ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; Taarifa kuhusu masuala Forodha, Biashara na masuala ya kifedha; Taarifa kuhusu Miundombinu, Sekta za Uzalishaji, Sekta za Kijamii na masuala ya Kisiasa; Taarifa kuhusu masuala Fedha na Taarifa kuhusu Taasisi za Jumuiya.

 

Mkutano wa Ngazi ya Wataalam umeongozwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania, Bw. Haji Janabi kwa niaba ya Mwenyekiti, Sudan Kusini ambao wameshiriki kwa njia ya mtandao

 

Mkutano huu wa ngazi ya wataalam unafanyika kuanzia tarehe 22 hadi 25 Novemba 2024 ukifuatiwa na mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 26 Novemba 2024 na  tarehe 27 na 28 Novemba 2024 utafanyika Mkutano wa 46 wa Baraza la Mawaziri ambao utapokea agenda mbalimbali kutoka kwa Makatibu Wakuu .

 

Agenda zitakazojadiliwa katika Baraza la Mawaziri zitawasilishwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi unaotarajiwa kufanyika tarehe 30 Novemba 2024 kwa ajili ya kupitishwa na kuridhiwa kwa utekelezaji.

 

Nchi nane Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki za Burundi, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda zinashiriki mkutano huo.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania, Bw. Haji Janabi akiongoza kikao kwa niaba ya Mwenyekiti, Sudan Kusini ambao wameshiriki kwa njia ya mtandao. Kikao hicho cha ngazi ya wataalam  kimefanyika jijini Arusha kuandaa Mkutano wa 46 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 28 Novemba 2024. Kikao cha Wataalaam kitafanyika kuanzia tarehe 22 hadi 25 Novemba 2024 na kufuatiwa na Kikao cha Makatibu Wakuu mnamo tarehe 26 Novemba 2024.M

Mkurugenzi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji kutoka Wizara ya Mabo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania, Bw. Benjamin Mwesiga akichangia jambo wakati wa kikao cha Wataalam. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Abdilah Mataka akifuatilia kikao
Sehemu ya ujumbe wa Burundi wakishiriki Mkutano wa Wataalam
Ujumbe wa Kenya

Ujumbe wa Somalia

Ujumbe wa Uganda

Sehemu ya Wajumbe wakishiriki kikao cha wataalam

Sehemu nyingine ya wajumbe wakati wa kikao

Wajumbe wakishiriki kikao

Ujumbe wa Tanzania wakishiriki kikao

Kikao kikiendelea

Wajumbe wakati wa kikao



Kikao kikiendelea

Kikao kikiendelea






 

WAZIRI KOMBO KUONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KWENYE MKUTANO WA KUJADILI AMANI NA USALAMA UKANDA WA MAZIWA MAKUU



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Luanda, Angola, terehe 22 Novemba 2024.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ataongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Kawaida wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje (RIMC) wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) unatakaofanyika jijini Luanda, Angola tarehe 24 Novemba 2024. 

Mkutano huo unalenga kupokea na kujadili kuhusu hali ya kisiasa na usalama katika eneo la ukanda wa Maziwa Makuu hususan katika nchi za Jamhuri ya Sudani, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). 

Hatua hiyo inafauatia matukio mbalimbali yaliyotokea katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita kwenye ukanda wa Maziwa Makuu ambayo yamechangia kuzorota kwa hali ya amani na usalama ikiwemo mauaji ya halaiki, ukosefu wa utulivu wa kisiasa, kuwepo kwa mipaka isiyo dhibitiwa, uharifu wa kibinandamu na mivutano ya kugombea madaraka na maliasili. 

Hivyo mkutano huo una mchango mkubwa katika kurejesha amani na usalama kwenye ukanda huo kutokana na nafasi yake ya kupendekeza na kusimamia utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali inayolenga kutatua changamoto hizo ikiwemo mazungumzo, jeshi na kuimarisha utawala bora ili kuchagiza maendeleo ya kiuchumi, kijamii na ushirikiano wa kikanda.

Kadhalika, mkutano huo utapitia na kujadili kuhusu ufanisi wa mipango kazi mbalimbali iliyoandaliwa kwa lengo la kushughulikia migogoro mikubwa katika maeneo mbalimbali kwenye ukanda kiwemo Jamhuri ya Sudani, DRC na Jamhuri ya Afrika ya Kati ili kurejesha na kuimarisha amani na usalama katika maeneo hayo. 

Mkutano huo ulioitishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola na Mwenyekiti wa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) Mhe. Balozi Téte António, vilevile unalenga kuangazia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika mikutano iliyotangulia ya Mawaziri hao. 

Mbali na hayo Waziri Kombo akiwa nchini Angola anatarajiwa kufanya mazungumzo ya uwili na Viongozi mbalimbali wa Serikali kutoka nchi za Maziwa Makuu kwa lengo la kudumisha uhusiano wa kidiplomasia kwa manufaa ya pande zote.

Waziri Kombo amewasili jijini Luanda, Angola leo tarehe 22 Novemba 2024 na kupokelewa na Balozi Felisberto Martins Mkurugenzi wa Idara ya America katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Angola, Balozi wa Tanzania nchini humo Mhe. Lt. Gen. Mathew Edward Mkingule mwenye makazi yake nchini Zambia na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini humo Bw. Mbwana Mziray


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo akisalimiana na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania nchini Angola Bw. Mbwana Mziray alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kamataifa wa Luanda, Angola tarehe 22 Novemba 2024.

TANZANIA NA CHINA ZASISITIZA KUKUZA USHIRIKIANO

Serikali ya Tanzania na China zimesisitiza kuongeza ushirikiano wa kimaendeleo kupitia ziara mbalimbali zinazofanywa na viongozi wa juu wa pande zote mbili ili kuimarisha ushirikiano wa kihistoria na kidiplomasia ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo, Baba wa Taifa Hayati, Mwl. J.K. Nyerere wa Tanzania na Mwenyekiti Mao Zedong wa China.

Msisitizo huwa umetolewa wakati Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala  ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo alipokutana na Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Prof. Hao Ping na ujumbe wake katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Aidha, katika mazungumzo hayo Mhe. Londo ameueleza ujumbe huo kuwa Tanzania ina thamani ushirikiano imara uliopo kati yake na China hasa wakati huu ambapo mataifa hayo yanaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia tangu kuanzishhwa kwake.

Pia, ameipongeza Jamhuri ya Watu wa China kwa kuandaa na kuwa  mwenyeji wa Mkutano wa kilele wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika mwezi Septemba, 2024 jijini Beijing, China. 

Alisema kuwa kupitia mkutano huo Hati za Makubaliano ya Ushirikiano katika sekta mbalimbali zenye matokeo makubwa kiuchumi zilisainiwa ikiwemo ya kufufua reli ya TAZARA ambayo ilijengwa enzi za uhuru wa Tanganyika.

‘’ Maboresho ya Reli ya TAZARA inayoiunganisha Tanzania na Zambia ni hatua muhimu kwa ustawi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi hizo mbili pamoja na ukanda wa kusini mwa Afrika ambao unategemea bandari ya Dar Es Salaam katika usafirishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali’’ alisema Mhe. Londo.

Pia, alieleza mradi huo ni alama kubwa na ya kwanza ya miradi ya ushirikiano kati ya Tanzania na China iliyoacha kumbukumbu isiyofutika kwa pande zote mbili na kwamba historia hiyo imeendelea kurithishwa kwa kizazi cha sasa kupitia manufaa yake katika shughuli za kiuchumi.

Kadhalika, ameeleza imani yake juu ya ziara ya Kamati hiyo na kwamba itaenda kufungua ushirikiano zaidi wa kibunge kati ya Bunge la Tanzania na Bunge la China. 

Vilevile ameshukuru kwa ufadhili wa fursa za masomo ya muda mrefu na mfupi ambao umekuwa ukitolewa  na Serikali ya China kwa Tanzania na hivyo kuendelea kukuza ushirikiano miongoni wa wananchi wa mataifa hayo.

Kwa upande wa Prof. Ping ameeleza kuwa jitihada zinazofanywa sasa na viongozi wakuu wa nchi hizo mbili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping zinaonesha nia ya dhati ya kukuza ushirikiano huo wa kihistoria.

‘’Ushirikiano katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa utaendelea kuimarishwa na kudumishwa na tuhakikisha yale yote yaliyokubaliwa na viongozi wetu wakuu wakati wa mkutano wa FOCAC yanasimamiwa na kutekelezwa kwa maslahi ya pande zote mbili’’ alisema Prof. Ping. 

Pia ameeleza kuwa Mkutano wa 20 wa Chama cha Kikomunist cha China ulifanya mageuzi katika maeneo ya kimkakati ya ushirikiano baina ya Tanzania na China na Afrika kwa ujumla ambayo yameongeza mafanikio katika urafiki wa mataifa hayo na kuruhusu utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya kisekta.

Pamoja na masuala hayo viongozi hao pia wameahidi kuendelea kushirikiana kwa kuunga mkono sera za kitaifa na ajenda mbalimbali katika majukwa ya kikanda na kimataifa na kuimarisha ushirikiano wa wananchi wa mataifa hayo mawili ili kukuza mawasiliano yatakayorahisisha kukuza sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji na utalii.

Ujumbe huo upo nchini kwa ziara ya siku 3 ambapo unatarajia kukutana na kuzungumza na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano la Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu (Mb) na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa (Mb.).