Saturday, November 16, 2024

WAZIRI KOMBO APOKEA TAARIFA YA KAMATI MAALUM YA MAPITIO YA KITUO CHA DKT. SALIM AHMED SALIM


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo, (Mb), amepokea Taarifa ya  Kamati Maalum ya Wizara kuhusu mapitio ya kituo cha uhusiano wa kimataifa cha  Dkt. Salim Ahmed Salim cha Jijini Dar es Salaam. iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Balozi Khamis Sued Kagasheki. 

Katika Taarifa hiyo, Balozi Kagasheki aliwasilisha matokeo ya uchambuzi uliofanywa na Kamati na kuainisha mapungufu yaliyobainika kwenye maeneo mbalimbali na kutoa mapendekezo husika kuboresha Kituo hicho ili kikidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye katika nyanja za diplomasia na uhusiano wa Kimataifa.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo Mhe. Waziri Kombo aliishukuru Kamati hiyo kwa ufanisi, uzalendo, taaluma, ukweli na uwazi katika kutekeleza jukumu ililopewa.

Mhe Waziri alibainisha kuwa mapendekzo ya Kamati yatachangia kuboresha Kituo hicho na hivyo kufikia malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanadiplomasia Namba Moja Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukifanya Kituo hicho kuwa kituo cha umahiri, fikra na rejea katika kukuza wanadipolomasia wa Tanzania ili waweze kutoa mchango unaotarajiwa katika nyanja ya diplomasia na uhusiano wa kimataifa nchini na ukanda wa Afrika.

Mhe. Waziri pia aliainisha utayari wa Wizara katika kutekeleza mapendekezo ya Kamati ili kukifanya Kituo hicho kiakisi taswira na  kuenzi kazi na mchango mkubwa wa Mwanadiplomasia Nguli nchini Balozi Dkt. Salim Ahmed Salim alizofanya na kuutoa katika diplomasia ya Tanzania, Bara la Afrika, Umoja wa Mataifa na ulimwenguni kwa ujumla. 

Balozi Kombo aliwahakikishia wajumbe wa Kamati hiyo kuwa, Wizara chini ya uongozi wake itaandaa mpango kazi wa kutekeleza mapendekezo yao kwa kuaza na maandalizi ya Mfumo wa Kisheria ambao utakamilika mapema ili kuleta mageuzi ya kweli.

Kamati hiyo iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ina wajumbe sita ikiongozwa na Balozi Khamis Sued Kagasheki kama Mwenyekiti, wajumbe wengine ni Balozi Dkt. Ramadhan Kitwana Dau; Balozi Dkt. Salim Othman Hamad; Profesa Marcellina Mvula Chijoriga; Bw. Kadari Lincoln Singo na CPA. Asumpta Marcel Muna ilianza utekelezaji wa Majukumu yake Mwezi Aprili, 2024.

Kamati hiyo ilianisha masuala yanayopaswa kufanyiwa kazi kuwa ni umuhimu wa kuweka mfumo mpya wa kisheria na umiliki wa Kituo; Malengo, Programu za Mafunzo na  Wadau wa Kituo. Aidha, mapendekezo mengine yaligusa Uhusiano kati ya Wizara Mama na Kituo; Uongozi, Ajira na Maendeleo ya Watumishi; Mfumo wa Bajeti na Utawala; Miundombinu na Mazingira ya Kujifunzia na Kufundishia. 

Mengine ni Kuimarisha Ushirikiano na Ubia (partnerships) baina ya Kituo wadau wengine ndani na nje; Mpango  wa Biashara wa Kituo (Business Model ) utakoondoa utegemezi wa Serikali na kuboresha muundo wa Wizara Mama na Kada ya Maafisa Mambo ya Nje na Kada Nyingine.

 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.