Thursday, November 14, 2024

NAIBU WAZIRI LONDO AKUTANA NA NAIBU WAZIRI WA UBELGIJI

Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Misaada ya Kibinadamu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Falme ya Ubelgiji Mhe. Heidy Rombouts. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.


Katika mazungumzo yao viongozi hao wamepongeza ushirikiano wa maendeleo uliopo kati ya Tanzania na Ubelgiji ambao tarehe 14 Novemba, 2024 umetimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake.


Miaka 40 ya ushirikiano huo imeshuhudia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika nyanja mbalimbali za Elimu, Afya na Usafirishaji. Mhe. Londo pia ameishukuru Serikali ya Ubelgiji kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini na kutumia kikao hicho kuihakikishia Ubelgiji  dhamira na hatua za Serikali ya Tanzania kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati.


Mhe. Londo ametoa rai kwa Serikali ya Ubelgiji kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa nchini.


Kwa upande wake Mhe. Rombouts ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na kuishukuru Tanzania kwa kuwa ndau mkubwa wa ushirikiano wa kimaendeleo.


Viongozi hao  wameahidi kuendelea kudumisha ushirikiano na kuzungumza mara kwa mara  katika masuala mbalimbali.
 

    No comments:

    Post a Comment

    Note: Only a member of this blog may post a comment.