Thursday, August 13, 2015

Waziri Membe afungua Kongamano la Pili la Diaspora nchini

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaina Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Pili la Watanzania waishio nje (Diaspora) ambalo limebeba kaulimbiu isemayo "Tanzanian Diaspora and SMEs in Partnership for Development and Job-Creation".  Kongamno hilo la siku mbili limefanyika katika Hoteli ya Serena  Jijini Dar es Salaam 


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula (Kulia) pamoja na Balozi wa Umoja wa Ulaya Mhe. Filiberto Sebregondi (kushoto) wakimsikiliza Waziri Bernard Membe (hayupo pichani).
Juu na Chini ni Waziri Membe akiendelea kuzungumza na Wanadiaspora na wadau mbalimbali walioudhuria Kongamano hilo 
Sehemu ya washiriki wa kongamano hilo wakiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Joseph Sokoine (wa kwanza kushoto), akifuatiwa na Mkurugenzi Idara ya Asia na Australasia pamoja na washiriki wengine wakifuatilia hotuba kutoka kwa  Mhe. Membe (hayupo pichani)
Sehemu nyingine ya washiriki wa Kongamano wakisikiliza kwa makini hotuba iliyotolewa na Mhe. Membe (hayupo pichani).
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Bw. Assah Mwambene (kulia) kwa pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati Elibariki Maleko (wa kwanza kushoto), Kaimu Mkurugenzi Idara ya Afrika, Bi. Zuhura Bundala (wa pili kutoka kushoto), Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Itifaki, Bw. James Bwana (wa tatu kutoka kushoto) nao wakimsikiliza Waziri Membe alipo kuwa akitoa Hotuba kwa niaba ya Rais  Jakaya Kikwete.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula naye akizungumza katika Kongamano hilo.
Juu na chini ni washiriki katika Kongamano hilo wakimsikiliza Mhe. Balozi Mulamula (hayupo pichani). 
Mke wa wa Waziri Membe, Bi. Dorcas Membe (katikati) kwa pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Uswisi, Mhe. Modest Mero (kulia) nao wakifuatilia ufunguzi wa Kongamano la Diaspora. 
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora, Bi. Rosemary Jairo naye akizungumza katika kongamano la Diaspora wakati wa ufunguzi wa Diaspora. 
Msanii wa kizazi kipya Bw. Peter Msechu akiwaongoza mgeni rasmi, Mhe. Membe, meza kuu na washiriki wengine wa kongamano kuimba  Wimbo wa Taifa kabla ya ufunguzi rasmi wa Kongamano.
Maafisa Mambo ya Nje nao wakiimba wimbo wa Taifa.
Sehemu ya washiriki katika Kongamano la Diaspora  nao wakiimba wimbo wa taifa 
Waziri Membe na Bi Dorcas Membe wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Kongamano la Diaspora mara baada ya shughuli ya ufunguzi kukamilika.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Benard Membe akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Liberata Mulamula (wa kwanza kulia), Balozi wa Umoja wa Ulaya, Mhe. Sebregond (wa pili kutoka kulia), Mwakilishi wa Baraza la wa Wakilishi Zanzibar, Ali Mzee Ali (wapili kutoka kushoto), Kaimu Mkurugenzi Idara ya Diaspora, Bi Rosemary Jairo (wa kwanza kushoto) na Mwakilishi wa (DICOTA) Bw. Abdul Majid. 
Mhe. Membe pamoja na wageni katika mezaa kuu wakiwa katika picha ya pamoja na Watanzania waishio Ughaibuni

Picha na Reginald Philip


============================================

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ametoa rai kwa Watanzania wanaoishi ughaibuni (Diaspora) kushirikiana kwa karibu  na Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (SME’s) ili kuchangia maendeleo ya nchi na hatimaye kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Kongamano la Pili la Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora) lililofanyika leo kwenye Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam , iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali yake imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara (SME’s) inashamiri ili kuchangia maendeleo ya nchi na kukuza ajira kwa wananchi wa Tanzania wakiwemo vijana na kuwahimiza Diaspora kushirikiana na sekta hiyo ili kuleta tija.

Rais Kikwete amesema kuwa, lengo la kongamano hili la pili  ni kuwahimiza Watanzania waishio ughaibuni kuuangana na  Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (SME’s) kwa ajili ya kuleta maendeleo nchini na kutengeza ajira.

“Napongeza kaulimbiu ya kongamano hili la mwaka huu ambayo inahimiza SME’s kufanya kazi kwa pamoja na Wanadiaspora kwa ajili ya kuiletea nchi yetu maendeleo na pia kutengeneza ajira kwa wananchi”, alisema Rais Kikwete.


Aidha, alisema kuwa Kongamano hili ni moja ya jitihada zinazofanywa na Serikali yake katika kuhakikisha Watanzania wanaoishi ughaibuni (Diaspora) wanaunganishwa na kunufaika na sekta  mbalimbali za hapa nchini ikiwemo hiyo ya SME’s  ambayo inachangia asilimia 35 ya pato la taifa.

Mhe. Rais, aliongeza kuwa dhamira ya  serikali  ni kuweka mazingira mazuri Diaspora ili waweze kuja kuwekeza nyumbani na kwamba jitihada hizo ni pamoja na kuifanyia maboresho Sekta ya SME’s kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali za Wanyonge Tanzania (MKURABITA)  ili  wafanyabiashara wadogo wapate uwezo wa kufanya biashara rasmi ikiwemo kuwawezesha kufanya biashara nje kwa kushirikiana na  Watanzania wanaoishi ughaibuni  (Diaspora) ambao watasaidia upatikanaji wa  masoko kwa bidhaa  na kuhamasisha wawekezaji wa nje kuja nchini.

Vilevile aliwahimiza Diaspora kuendelea kutoa mchango wao kwa maendeleo ya nchi ikiwemo ujuzi, elimu, mitaji, huduma na kujenga nyumbani kupitia miradi mbalimbali inayotolewa na mashirika ya nyumba likiwemo Shirika la nyumba la Taifa (NHC).

Kwa upande wake, Mhe. Waziri Membe alisema kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ilianzisha Idara ya Diaspora mwaka 2009 kwa lengo la kuwatambua Watanzania wanaoishi ughaibuni na kuwahamasisha kuchangia maendeleo ya nchi kwa kutumia mitaji, ujuzi na elimu wanayoipata wakiwa nje ya nchi.  Aidha, akitoa maoni yake kuhusu suala la uraia wa nchi mbili (Dual Citizenship) Mhe. Membe alisema kuwa bado ana imani kuwa suala hilo litaendelea kujadiliwa ili kuwawezesha Wanadiaspora kuleta  maendeleo ya kweli  nchini.

Awali, akimkaribisha Waziri Membe kuzungumza, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa dhumuni la kongamano la pili la Diaspora  ambalo limeratibiwa na Wizara kwa  kushirikiana na Ofisi ya Rais-Zanzibar na Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuhimiza na kuendelea kutambua mchango wao katika ukuaji wa uchumi nchini na kuwaunganisha Diaspora na Sekta ya Viwanda Vidogo na biashara Ndogo (SME’s).

Kongamano hilo la  siku mbili, linawahusisha Watanzania wanaoishi ughaibuni, wadau mbalimbali kutoka sekta za umma na binafsi na wawakilishi kutoka mikoani.

-Mwisho-



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.