TAARIFA KWA UMMA
MAAZIMIO YA BARAZA
LA KATIBA LA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa lilikutana tarehe 26 Agosti, 2013 kujadili Rasimu ya
Katiba mpya. Mkutano huo ulifanyika
kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es
Salaam.
Mkutano ulifanyika chini ya Uenyekiti wa Mhe.
Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na
kufunguliwa na mgeni rasmi, Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Salim Ahmed Salim ambaye
pia ni Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo
ya Nje na Balozi wa Tanzania nchini Misri na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania
katika Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mabalozi Wastaafu,
Wafanyakazi wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake.
Wizara iliamua kuunda Baraza la
Katiba kwa kuzingatia kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
ni Wizara ya Muungano; Rasimu ya Katiba imependekeza masuala ya Sera ya Nje
kuendelea kuwa miongoni mwa masuala ya Muungano; na kuwa yako masuala
yaliyopendekezwa kwenye rasimu ya Katiba ikiwemo mipaka, uraia na muundo wa
muungano ambayo yanagusa majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa.
Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, liliazimia mapendekezo yafuatayo katika
maeneo ya Mipaka, Muundo wa Jamhuri, Uraia wa Jamhuri na Sera ya Mambo ya Nje:-
1)
Mipaka ya nchi iwekwe wazi mwishoni mwa Ibara ya 2 ili
isomeke kama ifuatavyo: “Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania
Bara na Zanzibar ikijumuisha ardhi, maziwa na sehemu yake ya bahari (Territorial Waters) pamoja na anga kwa
mujibu wa sheria za kimataifa;
2)
Baraza pia lilipendekeza mabadiliko katika Muundo wa Jamhuri
ya Muungano kwamba Muundo wa Serikali Mbili uliopo, uendelee na kuboreshwa kwa
kuwekewa mifumo imara ya kisheria itakayoakisi maslahi ya pande zote mbili za
Muungano ili kupunguza changamoto na manung’uniko kutoka kwa wadau wa Muungano.
3)
Kuhusu suala la uraia katika Jamhuri ya Muungano; Baraza lilipendekeza
kuwa suala la uraia wa nchi mbili kwa Mtanzania wa kuzaliwa litamkwe Kikatiba
na Raia huyo asipoteze uraia wake wa kuzaliwa kwa sababu ya kupata uraia wa nchi
nyingine. Uraia wa nchi mbili utatoa fursa kwa Taifa letu kufaidika kimaendeleo
kutokana na kutumia rasilimali za Watanzania walioko nje ya nchi;
4)
Kuhusu Uraia, Ibara ya 55(4) inayozungumzia kumpa uraia wa
kuzaliwa mtoto atakayekutwa ndani ya mipaka ya nchi yetu, ambaye wazazi wake hawajulikani
ni raia wa nchi gani, Baraza
linapendekeza “….Uraia huo utasitishwa endapo uraia
wa asili (wa nchi nyingine) wa mtoto huyo utagundulika na kuthibitishwa pasipo
na shaka au kama itagundulika kuwa ulifanyika udanganyifu wa kumtupa kwa
makusudi mtoto huyo kwa nia ya kupata uraia wa Jamhuri ya Muungano.”
5)
Kuhusu Uraia wa kuandikishwa, Ibara ya 56(2), mtu aliyefunga ndoa
na raia wa Jamhuri ya Muungano anaweza kutuma maombi ya kuandikishwa kuwa raia
wa Jamhuri ya Muungano baada ya kuomba uraia wa Muda wa kuishi nchini kama
mwanafamilia wa ndoa (dependant)
mpaka ndoa iwe imedumu kwa miaka kadhaa (miaka itamkwe na sheria)”.
6)
Kuhusu Sera ya Mambo ya Nje; Baraza linapendekeza mabadiliko
katika Ibara ya 12 ya rasimu kwamba Misingi (Principles) ya Sera ya Mambo ya
Nje ijumuishwe badala ya majukumu ya Wizara kwa kuwa majukumu hubadilika na
nyakati. Aidha, Katiba ilielekeze Bunge litunge Sheria itakayosimamia
utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania.
7)
Kuhusu Ibara ya 39 (3) inayohusu raia wa Tanzania
kutokupelekwa nje ya nchi kujibu mashtaka au kufanyiwa mahojiano ya aina yoyote
bila ya ridhaa yake, Baraza linapendekeza Kifungu hicho kifutwe, kwa sababu
kuna ugumu wa haki inayotajwa kwenye Kipengele hiki kutekelezeka bila kuathiri
wajibu ya kimataifa wa nchi (international obligations) katika makosa ya jinai,
kwa kuwa ni vigumu sana kupata ridhaa ya mtuhumiwa kuhojiwa kwa makosa
aliyoyatenda au anayotuhumiwa kuyatenda.
WIZARA YA MAMBO YA NJE
NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
28 AGOSTI, 2013
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.