Tuesday, August 27, 2013

TAARIFA KWA UMMA


Mhe. Waziri Membe akielezea kuhusu suala la uraia wa nchi mbili. 



TAARIFA KWA UMMA

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inapenda kuujulisha Umma kuwa jana tarehe 26 Agosti, 2013, Mheshimiwa Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alikutana na Uongozi wa Tume ya Marekebisho ya Katiba.  Lengo la kukutana na Tume ilikuwa ni kuwasilisha pendekezo la haki ya Uraia wa nchi mbili kutamkwa na kutambuliwa kwenye Katiba mpya.

Mheshimiwa Waziri alikutana na Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Augustino Ramadhani, Makamu Mwenyekiti wa  Tume pamoja na Katibu wa Tume na Naibu Katibu wa Tume.

Akiwasilisha hoja yake mbele ya Tume ya Marekebisho ya Katiba, Mheshimiwa Waziri alisema yafuatayo:-

1.    Suala la Uraia wa Nchi mbili haliko kwenye rasimu ya sasa iliyotolewa.  Lengo la kufika Tume ni ni kuomba suala hilo liingizwe kwenye rasimu.

2.    Amependekeza Katiba itamke kwamba, Raia wa Tanzania aliyeko nje hatafutiwa uraia wake na mtu yeyote, chombo chochote sheria au Katiba, eti tu kwa sababu raia huyo amechukua uraia nje ya nchi.

3.    Katiba ikitamka hivyo, itungwe Sheria itakayofafanua haki, wajibu na masharti ya Mtanzania mwenye uraia wa nchi mbili.

4.    Katika kujenga hoja hizo tatu, Tume ilielezwa faida zitakazopatikana kwa kuitambua na kuishirikisha jamii ya Watanzania waliopo ughaibuni (Diaspora).  Tume pia iliondolewa wasiwasi juu ya madai kuwa uraia wa nchi mbili unahatarisha usalama wa taifa au utawafanya baadhi ya watu kupiga kura wakiwa nje. Tume iliambiwa kuwa Sheria za Uchaguzi hutawala upigaji kura kwa raia walio ndani  na nje na hauwi  holela.  Kuhusu suala la usalama, Waziri alisisitiza kama ni mashaka, basi mashaka hayo yawe kwa wageni wanaoomba uraia  nchini kuliko watanzania walioko nje.


Katika kumalizia, Mheshimiwa Waziri alisisitiza, “bado naamini watanzania walioko nje sio wasaliti, They are just as smart citizen”.



IMETOLEWA NA:


 WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA 

KIMATAIFA


27 Agosti, 2013





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.