Mabalozi wetu wawe
chachu ya kuwavuta wawekezaji
NA Maoni ya MHARIRI wa Gazeti la NIPASHE
JUMAPILI,
22 Septemba
2013
Moja
ya sera na mikakati ya kuinua uchumi wa nchi ni pamoja na kuwahamasisha
wawekezaji wa ndani na wa nje katika miradi mbalimbali ya kiuchumi ambayo
itasaidia kuinua pato la taifa.
Ni
rahisi zaidi kuwahamasisha wawekezaji wa ndani kwa vile wao nao ni sehemu ya
jamii inayopambana na kujikwamua kutoka uchumi uliopo ambao ni tegemezi na
unaoonekana kuwa dhaifu.
Kikwazo
kinachojitokeza kwenye sera ya uwekezaji ni pamoja na umaskini wa wananchi
wengi ambao kimsingi wanakosa mitaji mikubwa ya kuwafanya wawekeze katika sekta
zinazohitaji mitaji mikubwa.
Wenye
uwezo wa kuwekeza kwa mitaji inayoweza kuzalisha faida kubwa ni wageni wa nchi
mbalimbali za duniani, ambako pia kuna wawakilishi wetu ambao ni mabalozi
wanaoiwakilisha Tanzania kwa masuala ya kidiplomasia.
Rais
Jakaya Kikwete akiwa katika ziara ya Marekani jijini Washington mwishoni mwa
wiki hii, alisema kazi kubwa ya mabalozi wa Tanzania katika nchi za nje, ni
kutetea maslahi na kuijengea marafiki katika nchi na maeneo ambako
wanaiwakilisha nchi.
Rais
alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila balozi wa Tanzania popote alipo, kuonyesha
sura nzuri ya Tanzania, kuvutia wawekezaji katika maeneo mbalimbali na
kutangaza nafasi nyingi za uwekezaji nchini.
Tanzania
ina utajiri mkubwa wa utalii duniani, na mojawapo ya majukumu ya mabalozi wetu
hao ni kutangaza utajiri huo, na hasa Marekani ambayo kwa sasa ndiyo nchi
inayoongoza kwa kuleta watalii wengi nchini.
Rais
Kikwete alipata fursa ya kuongea na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nchi za
nje, ilikuwa wakati alipozungumza kwenye hafla ya kutiwa saini kwa makubaliano
kati ya Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Liberata Mulamula na mabalozi saba
wa heshima ambao wataiwakilisha Tanzania katika maeneo mbalimbali nchini
Marekani.
Katika
hafla hiyo, Rais Kikwete aliwaasa mabalozi hao wa heshima kuwa wanawajibika
kulijenga jina la Tanzania katika maeneo yao, na kuitengenezea nchi yetu
marafiki wa kila aina ikiwa ni pamoja na kuwavutia wawekezaji kuja nchini
kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Watu
wenye fedha na rasilimali za kuwekeza wanatakiwa waelimishwe kuwa Tanzania ni
nchi nzuri kupeleka mitaji yao na kuwa mitaji hiyo itabakia kuwa salama. Rais
aliwasisitizia mabalozi hao wa heshima kuwa pia watangaze utajiri mkubwa wa
utalii uliopo nchini.
Tuna
imani kubwa kuwa wito alioutoa Rais Kikwete kwa mabalozi wetu utatekelezwa kwa
umakini, na pia tuaamini kuwa muda si mrefu Tanzania itanufaika na fedha za kigeni
ambazo zitatokana na utalii pamoja na uwekezaji kutoka nchi mbalimbali duniani.
Wapo
wawekezaji wazalendo ambao baadhi wamewekeza katika sekta mbalimbali kama za
hoteli za kitalii, mashamba ya mazao ya biashara na chakula, viwanda vidogo
vidogo pamoja na katika masuala ya elimu. Bado jitihada zinatakiwa zifanyike
ili kutanua wigo wa uwekezaji katika maeneo mengine ya kiuchumi.
Faida
kubwa za uwekezaji si kwa ajili ya serikali kuongeza pato peke yake, bali hata
ajira kwa vijana huongezeka. Uchumi wa nchi unapokua, unatoa pia fursa nyingi
za ajira kwa vijana, na vijana ndiyo nguvu kazi inayotegemewa na nchi.
Mabalozi
popote w alipo duniani, wanawajibu kutambua jukumu hili kubwa ambalo ni msingi
mkubwa wa kuongeza pato la taifa na kuinua uchumi wa nchi. Wawekezaji wengi
walioko nchini wamejikita katika uchimbaji wa madini, na sasa wameanza
kuonyesha nia ya kuwekeza katika maliasili nyingine kama gesi asilia na mafuta.
Tunampongeza
Rais Kikwete kwa kuwahamasisha mabalozi kuinadi Tanzania katika maeneo ya
uwekezaji pamoja na utalii, tunaamini kasi ya kujituma kwa kazi hiyo ikifanyika
kwa uadilifu, Tanzania itakuwa moja ya nchi itakayojizolea fedha nyingi za
kigeni zitakazosaidia maendeleo ya taifa.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.