Mhe. Waziri Bernard K. Membe (MP), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akiongea na waandishi wa habari jana mchana katika Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje. Kulia ni Balozi Vincent Kibwana, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Baadhi ya waandishi wa habari waliokusanyika kumsikiliza Mhe. Waziri Membe.
Balozi Celestine Mushy (kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Bw. Elibariki Maleko (kulia), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje wakimsikiliza Mhe. Waziri Membe.
Balozi Dora Msechu (kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Bw. Omari Mjenga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje nao wakimsikiliza Mhe. Waziri Membe.
Mhe. Waziri Membe akifafanua jambo wakati wa mazungumzo yake na waandishi wa habari alipokutana nao jana Wizarani.
Waandishi wa habari waliokusanyika kumsikiliza Mhe. Waziri Membe. (picha hii na Reginald Philip)
Picha nyingine zote na Tagie Daisy Mwakawago
Membe: Tanzania haijamfukuza mtu yoyote
nchini
Na Ally Kondo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard K.
Membe (Mb) ameuambia Umma wa Tanzania na dunia kwa ujumla kuwa Serikali ya
Tanzania haijamfukuza mtu yeyote nchini mwenye sifa za ukiimbizi kama
inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Mhe. Waziri aliyasema hayo alipokutana na waandishi wa habari ofisini
kwake jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa tarehe 06 Septemba, 2013.
“Serikai haikumfukuza mkimbizi yeyote isipokuwa iliwafukuza wahamiaji
haramu, Aidha, wahamiaji haramu hao walipewa onyo la kuondoka nchini na wengi
wao wametii kabla ya operesheni maalum ya kuwatia mbaroni haijaanza” Waziri
Membe alisikika akisema.
Kuhusu hoja kuwa operesheni ya kuwafukuza wahamiaji haramu inawalenga
Wanyarwanda, Waziri Membe alisema kuwa hoja hiyo sio ya kweli. Alisema kuwa
hadi kufikia wakati huu zaidi ya wahamiaji haramu 31,000 wameondoka nchini.
Kati ya hao Warundi ni 21,000, Wanyarwanda ni 6,000 tu na waliobaki ni kutoka
nchi nyingine..
Mhe. Membe aliwaambia waandishi wa habari kuwa Tanzania imekuwa
kimbilio la wakimbizi kwa muda mrefu na hadi sasa inahifadhi wakimbizi zaidi ya
laki 4. Wakati wote wakimbizi wamekuwa wakipewa huduma nzuri na haijawahi
kusikika kuwa Tanzania inalaaniwa na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa
au Jumuiya ya Kimataifa kwamba Serikali inawanyanyasa wakimbizi.
Sambamba na taarifa hiyo, Mhe. Waziri aliwaambia waandishi wa habari
kuhusu mikutano inayofanywa na baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki (Kenya, Uganda na Rwanda) bila kuhusisha nchi nyingine wanachama wa
jumuiya hiyo.
Mhe. Membe alisema kuwa yeye binafsi hana tatizo na mikutano hiyo
endapo tu, imepata kibali cha Wakuu wa Nchi wa EAC pamoja na kutoa ripoti ya
masuala yanayozungumzwa katika vikao vya jumuiya. “Mimi binafsi sioni tatizo
kwa nchi hizo kukutana endapo zimepewa Baraka na Wakuu wote wa Nchi wa EAC na
ripoti za mikutano yao kuwasilishwa katika vikao rasmi vya jumuiya” alisema
Mhe. Membe.
Aliwatoa shaka Watanzania kutokuwa na hofu na mikutano hiyo kwa kuwa
Tanzania ni nchi muhimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo hainabudi
nchi nyingine kuitegemea kutokana na rasilimali zilizopo na jiografia
yake.
Alihitimisha mazungumzo yake kwa kusema kuwa anaamini vikao
vinavyofanywa, vinafanywa kwa nia njema pasipo kuwa na dhamira ya kuleta
mgawanyiko ndani ya jumuiya. Na endapo vinafanywa kwa dhamira ya kuleta
mgawanyiko basi muda wa kurekebisha hali hiyo upo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.