Na Ally Kondo, Cairo
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe.
Bernard K. Membe (Mb) amemwakilisha Rais Kikwete katika sherehe za kumuapisha Mkuu
wa Majeshi wa zamani, Field Marshal Abdel Fattah al Sisi kuwa Rais mpya wa
Misri. Rais Sisi aliapishwa na Jaji Mkuu katika viwanja vya Mahakama Kuu ya
Misri siku ya Jumapili tarehe 08 Juni, 2014 ambayo ilitangazwa kuwa ni siku ya
mapunziko.
Sherehe za uapisho zilihudhuriwa na Viongozi wa nchi
mbalimbali duniani, hususan kutoka nchi za Kiarabu na Afrika. Nchi za Kiarabu
ziliwakilishwa vizuri katika sherehe hizo kwa kutuma Viongozi wa ngazi ya Juu
ukilinganisha na nchi za Afrika ambazo nyingi zilituma Mawaziri wa Mambo ya Nje
isipokuwa chache kama vile Somalia, Chadi na Equatorial Guinea ambazo Marais
wao walishiriki wenyewe.
Sherehe za uapisho zilipambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo
gwaride la kijeshi, hotuba za Rais anayengia madarakani na anayetoka na kila
mwakilishi kupata fursa ya kusalimiana na kufanya mazungumzo ya muda mfupi na Rais
Sisi.
Sherehe hizo ambazo zilifanyika huku kukiwa na ulinzi mkali
zilishuhudiwa pia, wafuasi wa Rais Sisi wakizunguka katika mitaa ya jiji la
Cairo wakiwa katika magari, pikipiki au kutembea kwa miguu wakiwa wamebeba
bendera za nchi hiyo huku wakifyatua fataki, kupiga mayowe na honi.
Wachambuzi wa mambo walieleza kuwa Rais mpya wa Misri
anatarajiwa kuituliza nchi hiyo ambayo imekuwa ikikumbwa na machafuko ya
kisiasa ya mara kwa mara tangu mapinduzi ya wananchi yaliyomuondoa madarakani
Rais Hosni Mubarak mwaka 2011.
Hata hivyo, walikiri kuwa Rais Sisi anakabiliwa na changamoto
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufufua uchumi wa nchi hiyo ambao umedorora kwa
kiasi kikubwa kutokana na machafuko hayo. Changamoto nyingine ambayo Rais Sisi
anakabiliwa nayo ni kurejesha mshikamano na umoja wa wananchi wa Misri ambao
kwa kiasi kikubwa wametofautiana mitazamo kutokana na hali ya mambo inavyokwenda
katika nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.