Wednesday, June 11, 2014

Misri yapata Rais Mpya



Na Ally Kondo, Cairo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) amemwakilisha Rais Kikwete katika sherehe za kumuapisha Mkuu wa Majeshi wa zamani, Field Marshal Abdel Fattah al Sisi kuwa Rais mpya wa Misri. Rais Sisi aliapishwa na Jaji Mkuu katika viwanja vya Mahakama Kuu ya Misri siku ya Jumapili tarehe 08 Juni, 2014 ambayo ilitangazwa kuwa ni siku ya mapunziko.
Sherehe za uapisho zilihudhuriwa na Viongozi wa nchi mbalimbali duniani, hususan kutoka nchi za Kiarabu na Afrika. Nchi za Kiarabu ziliwakilishwa vizuri katika sherehe hizo kwa kutuma Viongozi wa ngazi ya Juu ukilinganisha na nchi za Afrika ambazo nyingi zilituma Mawaziri wa Mambo ya Nje isipokuwa chache kama vile Somalia, Chadi na Equatorial Guinea ambazo Marais wao walishiriki wenyewe.
Sherehe za uapisho zilipambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo gwaride la kijeshi, hotuba za Rais anayengia madarakani na anayetoka na kila mwakilishi kupata fursa ya kusalimiana na kufanya mazungumzo ya muda mfupi na Rais Sisi.
Sherehe hizo ambazo zilifanyika huku kukiwa na ulinzi mkali zilishuhudiwa pia, wafuasi wa Rais Sisi wakizunguka katika mitaa ya jiji la Cairo wakiwa katika magari, pikipiki au kutembea kwa miguu wakiwa wamebeba bendera za nchi hiyo huku wakifyatua fataki, kupiga mayowe na honi.
Wachambuzi wa mambo walieleza kuwa Rais mpya wa Misri anatarajiwa kuituliza nchi hiyo ambayo imekuwa ikikumbwa na machafuko ya kisiasa ya mara kwa mara tangu mapinduzi ya wananchi yaliyomuondoa madarakani Rais Hosni Mubarak mwaka 2011.
Hata hivyo, walikiri kuwa Rais Sisi anakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufufua uchumi wa nchi hiyo ambao umedorora kwa kiasi kikubwa kutokana na machafuko hayo. Changamoto nyingine ambayo Rais Sisi anakabiliwa nayo ni kurejesha mshikamano na umoja wa wananchi wa Misri ambao kwa kiasi kikubwa wametofautiana mitazamo kutokana na hali ya mambo inavyokwenda katika nchi hiyo. 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.