TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MHESHIMIWA MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA WAKUU WA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI (EAC) KUHUSU MIUNDOMBINU JIJINI NAIROBI, KENYA
Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal jana Novemba 29, 2014 aliiwakilisha Tanzania katika mkutano wa siku moja wa Wakuu wa Nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini Nairobi, Kenya. Mkutano huo, kwa mujibu wa utaratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, unafanyika kila baada ya miaka miwili na lengo lake kuu ni kufanya tathmini juu ya miradi ya miundombinu inayoshirikisha nchi washirika, sambamba na kutazama fursa ya kutanua miundombinu mipya katika nchi hizi kwa lengo la kukuza uchumi wa pamoja kwa nchi za Afrika Mashariki.
Tathmini hii ya Miundombinu inafanyika kwa kuwa mataifa ya Afrika Mashariki yanatambua umuhimu wa kuwa na miundombinu bora katika nchi hizi ili kuharakisha ukuaji wa uchumi, sambamba na kutanua mtengamano wa nchi hizi na hivyo kuwafanya wananchi wanaoishi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuzidi kuwa wamoja.
Mkutano wa jana uliongozwa na Kaimu Rais wa Kenya Mheshimiwa William Ruto na kuhudhuriwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi, Waziri Mkuu wa Rwanda pamoja na Waziri wa Afrika Mashariki wa Uganda. Viongozi wengine waliopata nafasi ya kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na Mheshimiwa Balozi Richard Sezibera, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Waziri wa Wizara hiyo kutoka Tanzania, Mheshimkiwa Samwel Sitta, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Donald Kaberuka, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Ukanda wa Afrika, Bwana Makhtar Diop, Katibu Mtendaji wa UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi na Baalozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Balozi Filiberto Sebregondi. Pia mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilishi wa nchi za China, Marekani, Japan na nyinginezo ambazo ni wadau wakubwa wa ujenzi wa miundombinu katika nchi za Afrika Mashariki.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Kaimu Rais wa Kenya, William Ruto alifafanua juu ya umuhimu wa kuhakikisha Afrika Mashariki inaunganishwa kwa miundombinu imara ili kukuza uchumi na akapongeza jitihada mbalimbali zinazofanyika katika kufanikisha azma hiyo huku pia akiomba nchi wanachama wa Afrika Mashariki kuendelea kuungana katika kutekeleza miradi ya miundombinu na kujitahidi kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo.
Mkutano huu pia uliambatana na kupokea ripoti ya utekelezaji wa maagizo ya Wakuu wa Nchi za EAC kuhusu Miundombinu kutoka kwa Mawaziri wa Nchi za Jumuiya. Wakuu wa Nchi katika Mkutano huu walipokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo waliyoyatoa katika mkutano wa pili uliofanyika mwezi Novemba, 2012 na kuidhinisha miradi 72 ya miundombinu ya kipaumbele ya Barabara, Reli, Nishati na Bandari.
Kwa upande wa utekelezaji; miradi 16 imekamilika, 39 inaendelea kutekelezwa na 17 ipo katika hatua za awali za kutafutiwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.
Kwa upande wa Tanzania miradi minne imekamilika ambayo ni Umeme katika mji wa Kibondo, mradi wa barabara ya Mbezi-Shule-Tangibovu-Makutano ya Nelson Mandela na barabara ya Tabata. Barabara nyingine iliyokamilika ni Nyangunge – Musoma – Sirari na sehemu ya Simiyu - Musoma inayounganisha Kenya na Tanzania huko ujenzi unaendelea.
Akizungumza katika Mkutano huo Makamu wa Rais amezitaka nchi wanachama kuharakisha utekelezaji wa miradi ya Miundombinu ili kusaidia utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja, ambayo inalenga kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na abiria. “Tusiishie kubakiza mipango hii katika karatasi, tusiishie kuzungumza tu bali huu ni wakati wa kuhakikisha tunarahisisha ufanyaji biashara katika nchi zetu na kupunguza vikwazo visivyo vya lazima,” alisema Mheshimiwa Makamu wa Rais.
Katika mkutano huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais pia aliambatana na Mheshimiwa Dkt. Mahadhi J. Maalim, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Zanzibar, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui. Mheshimiwa Makamu wa Rais na msafara wake tayari wamerejea nyumbani Tanzania ambapo kesho anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, maadhimisho yanayofanyika Kitaifa Mkoani Njombe.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Novemba 30, 2014
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.