Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) akitoa hotuba wakati wa Mahafali ya Pili ya Chuo Kikuu cha Bagamoyo yaliyofanyika katika Viwanja vya Hoteli ya Kiromo iliyopo Bagamoyo. Wahitimu 99 katika fani mbalimbali walitunukiwa shahada zao. Pembeni yake ni Prof. Costa Ricky Mahalu, Makamu Mkuu wa Chuo hicho.
=======================
WAZIRI MEMBE AANZISHA MFUKO KUSAIDIA WANAFUNZI ELIMU YA JUU
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) ameanzisha Mfuko Maalum wa kuwasaidia Wanafunzi wenye Ulemavu na Mahitaji Maalum kwa Ngazi ya Elimu ya Juu ambao utajulikana kama The Bernard Membe Scholarship Fund.
Waziri Membe aliutangaza Mfuko huo wakati akihutubia katika Mahafali ya Pili ya Chuo Kikuu cha Bagamoyo yaliyofanyika katika Viwanja vya Hoteli ya Kiromo mjini Bagamoyo hivi karibuni.
Mhe. Membe alisema kuwa Mfuko huo ambao utakuwa chini ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo unalenga kuwasaidia Wanafunzi nchini kote wenye mahitaji maalum na wenye nia ya kufikia elimu ya juu lakini hawana uwezo wa kifedha katika kutimiza malengo yao.
“Wakati umefika kwa Watanzania wenye uwezo kusaidia na kuchangia elimu nchini. Ni imani yangu kuwa kwa kushirikiana na wafadhili mbalimbali na pia kwa kutumia harambee mfuko huu utatunishwa na malengo yatatimia kama ilivyokusudiwa,” alisema Waziri Membe.
Aidha, Mhe. Membe alitumia fursa hiyo pia kuwaasa Wahitimu katika Kozi mbalimbali zinazotolewa na Chuo hicho kutumia vizuri elimu waliyoipata katika kudumisha amani, kufikia mafanikio na kuondoa umaskini katika jamii. Pia aliwaonya kujiepusha kabisa na vitendo vyovyote vya rushwa katika maisha yao na kuwataka kuwa raia wanaoishi kwa kufuata sheria za nchi.
Mhe. Membe ambaye pia alipata fursa ya kuwatunuku shahada mbalimbali Wahitimu hao kwa niaba ya Mkuu wa Chuo hicho, Askofu Mstaafu, Dkt. Elinaza Sendoro ambaye hakuweza kuhudhuria kwa sababu za kiafya, alizipongeza jitihada za Chuo katika kutoa Taaluma mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zinalenga kuwawezesha Wahitimu hao kujiajiri na kupata kazi sehemu yoyote duniani ikiwemo Mashirika ya Kikanda na Kimataifa.
“Ninaupongeza Uongozi wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo kwa kuweka mkazo katika masomo ya Sayansi na Teknolojia, pia kwa ubunifu wa kuwafundisha vijana namna ya kutengeneza ajira na si kutafuta ajira ili kutoa suluhisho kwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wetu nchini,” alisisitiza Mhe. Membe.
Awali akizungumza wakati wa mahafali hayo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Costa Ricky Mahalu alisema kuwa Chuo kimedhamiria kuwawezesha wanafunzi kuchangia Taifa katika vita dhidi ya maradhi, ujinga na umaskini na kutoa wataalam wenye uwezo wa hali ya juu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotokana na utandawazi.
Chuo Kikuu cha Bagamoyo kilianzishwa mwaka 2011 kwa lengo la kutoa elimu ya juu kwa ngazi ya Shahada, Shahada ya Uzamili, Stashahada na Cheti katika kozi zinazohusu Sheria, Sayansi na Teknolojia, Elimu, Utawala, Biashara, Usuluhishi wa Migogoro na Utunzaji wa Amani.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.