Wednesday, February 25, 2015

Rais Kikwete awasili Zambia kwa ziara ya kikazi ya siku mbili

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete (kushoto) kwa pamoja na mwenyeji wake Rais wa Zambia, Mhe. Edgar Lungu akisikiliza Wimbo  wa Taifa ukipigwa kwa heshima yake mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Keneth Kaunda nchini Zambia kwa ajili ya kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili.
Mhe. Rais KIkwete akikagua Gwaride la Heshima wakati wa ziara hiyo

Mama Salma Kikwete (mwenye kilemba chekundu) akiwa na  Mke wa Rais Lungu, Mama Esther pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe (mwenye tai nyekundu) wakifuatilia kwa furaha mapokezi.

Mhe. Rais Kikwete na Mhe Rais Lungu wakifurahia jambo kabla ya kuondoka uwanjani hapo baada ya mapokezi
Mhe. Rais Kikwete akiwasili katika eneo la Embassy Park Jijini Lusaka yalipo makaburi ya Viongozi Wakuu wa nchi hiyo kwa ajili ya kuweka mashada ya maua kuwakumbuka Viongozi hao akiwemo Hayati Fredrick Chiluba, Hayati Levy Mwanawasa na Hayati Michael Satta.
Mhe. Rais Kikwete kwa pamoja na Mama Salma wakiweka shada la maua kwenye moja ya kaburi la viongozi hao.
Mhe. Rais Kikwete akisaini Kitabu cha Wageni mara baada ya kuweka mashada ya maua kuwakumbuka Marais watatu wa Zambia waliozikwa kwenye eneo hilo
Waziri Membe (kulia) akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Grace Mujuma pamoja na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Bw. Salva Rweyemamu.
============================================
            Rais Kikwete awasili Zambia kwa ziara ya kikazi


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amewasili nchini Zambia leo tarehe 25 Februari, 2015 kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ikiwa ni mwaliko kutoka kwa Rais wa Zambia, Mhe. Edgar Lungu.

Mara baada ya kuwasili, Mhe. Rais Kikwete amepokelewa rasmi na mwenyeji wake Mhe. Rais Lungu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Keneth Kaunda ambapo alikagua Gwaride la Heshima na kupigiwa mizinga 21.

Baada ya mapokezi hayo, Mhe. Rais Kikwete alitembelea Eneo la Emmbasy Park, Jijini Lusaka ambalo ni maalum kwa maziko ya Viongozi Wakuu wa Taifa hilo na kuweka mashada ya maua kwenye makaburi ya Marais watatu ambao ni Hayati Rais Fredirick Chiluba, Hayati Rais Levy Mwanawasa na Hayati Rais Michael Satta.

Vile vile, Mhe. Rais Kikwete atafanya mazungumzo ya faragha na Rais Lungu yakifuatiwa na mazungumzo rasmi na baadaye dhifa ya Chakula cha Jioni iliyoandaliwa maalum kwa ajili yake na Rais Lungu.

Mhe. Rais Kikwete atamtembelea mwasisi wa Taifa la Zambia na Rais wa kwanza wa nchi hiyo Mhe. Keneth Kaunda tarehe 26 Februari 2015 na baadaye kukutana na Jumuiya ya Watanzania waishio Zambia.

Mhe Rais Kikwete ambaye amefuatana na Mama Salma Kikwete, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe, Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Mkuya Salum, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Charles Tizeba, Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Grace Mujuma, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Abbas Kandoro na Viongozi Waandamizi kutoka Serikalini na Mamlaka mbalimbali, atarejea nchini tarehe 26 Februari, 2015.

_Mwisho-





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.