TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali kuwarudisha Watanzania waliopo Yemen
Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa ametangaza hatua ya Serikali kuwarudisha Watanzania
waishio nchini Yemen, kufutia mapigano yanayoendelea nchini humu ya vita vya
wenyewe kwa wenyewe.
Akizunguza na Mhe. Ali Ahmed Saleh, Balozi wa Tanzania
nchini Oman siku ya Alhamis tarehe 16 Aprili 2015, Waziri Membe amesema ni
jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa Watanzania hao ambao wengi wao ni
wanafunzi, wanarejea nyumbani salama.
Zoezi la kurudisha Watanzania hao lilianza siku chache
zilizopita ambapo familia ya watu watano ilisaidiwa na kurudi nyumbani kupitia
Oman, wakati zoezi la kuwatambua na kuwaandikisha Watanzania likenddelea.
“Nimeruhusu matumizi ya fedha ya dharura ili kuhakikisha ndugu
zetu walioko kwenye hatari na machafuko ya Yemen wanarejeshwa salama nyumbani
mara moja” alisema Mhe. Membe.
Watanzania
hao ambao wengi wao hadi sasa wameshafika kwenye miji midogo ya Sarfat na
Al-Mazyouna kwenye mkoa wa Salala mpakani mwa Oman na Yemen, walituma maombi ya
dharura (distress call) kwenye Ofisi za Ubalozi Oman, kuelezea mazingira ya
hatari yanayowakabili, na kuomba kurudishwa nyumbani.
“Kulingana na maelekezo ya Waziri Membe, zoezi la
kuwarejesha Watanzania limeanza. Nimewapeleka maafisa wa ubalozi kule Salala ni
kilometa takriban elfu moja kutoka Muscut, ambapo watahakiki na kukabidhiwa
Watanzania wote sitini na nne (64) na wataruhusiwa kuingia nchini Oman na
kuelekea Tanzania” alimaliza Mhe. Ali Ahmed Saleh, Balozi wa Tanzania nchini
Oman.
Mgogoro wa Yemen unaoendelea baina ya maafisa wa polisi
waaminifu kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Ali Abdullah Saleh, na makundi ya
usalama yanayomuunga mkono rais wa sasa, Abed Rabbo Mansour Hadi, umeua mamia
ya watu na kujerui maelfu.
Mhe. Membe ametoa rai kwa Watanzania wote wenye ndugu au jamaa
nchini Yemen kuchukua tahadhari na kuwataarifu watafute msaada kupitia
Ubalozini Muscat ili kujihakikishia usalama wao. Aidha ametoa tahadhari kwa
Watanzania wanaotegemea kusafiri kwenda Yemen, kusitisha safari zao hadi hali ya
usalama itakaporejea.
-Mwisho-
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es
Salaam
16
Aprili, 2015
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.