Makabidhiano yakiendelea huku Balozi wa Tanzania nchini Oman, Mhe. Ali Ahmed Saleh akishuhudia. |
Waziri Membe akiwa kwenye
mazungumzo na Mhe. Alawi bin Abdulla, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman. =========================================== |
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ujumbe Maalum wa Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwenda kwa Sultan
Qaboos wa Oman
Mhe. Bernard K. Membe (Mb.) Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa amekabidhi ujumbe maalum kutoka kwa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda kwa Mhe. Sultani Qaboos bin Said
Al Said, Mtawala wa Oman.
Ujumbe huo maalum ulikabidhiwa kwa Mhe. Yousuf bin Alawi bin
Abdulla, Waziri wa Mambo ya Nje na mwenyeji wa ziara ya Waziri Membe nchini Oman,
kwenye ofisi za Wizara hiyo jijini Muscat, Oman Alhamisi Aprili 16, 2015.
Makabidhiano hayo ya kihistoria nchini hapa, yalishuhudiwa na Mhe.
Dkt. Mwinyihaji Makame, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, Zanzibar ,
Mhe. Ali Ahmed Saleh, Balozi wa Tanzania Oman, na viongozi wengine wa nchi zote
mbili na waandishi wa habari.
Baada ya makabidhiano, viongozi hao wawili na ujumbe wao walitumia
fursa hiyo kuzungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na
Oman.
Viongozi hao waliahidi kukuza uhusiano na utamaduni wa nchi hizi
mbili ambao unafanana kwa sababu za kihistoria. Mhe. Membe alimuelezea mwenyeji
wake nia ya Serikali kujenga Ofisi za Ubalozi kwenye kiwanja chake hapa
Mascut kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kuwa na majengo ya Tanzania
kwenye nchi mbalimbali duniani.
Aidha mradi mkubwa wa bandari ya Bagamoyo pia ulizungumzwa na
viongozi hao ambapo Serikali ya Oman ni mojawapo ya mdau wa mradi huo. Wahusika
wengine wa mradi wa Bandari ya Bagamoyo ni Serikali ya China na Tanzania.
Mhe. Yousuf bin Alawi bin Abdulla, Waziri wa Mambo ya Nje wa Omani
alimuhakikishia mgeni wake ushirikiano wa Serikali yake kwenye hatua zote hizi
muhimu za kuendeleza na kukuza uhusiano wa muda mrefu wa nchi hizi mbili.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
17 Aprili 2015
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.